NDOTO ZIMETIMIA; Harmonize, Davido, Tyla, Nandy kumbe wazazi waliwazimia muziki
Muktasari:
- Hakuna ubishi kila msanii anahitaji sapoti ili aanze, atoke au azidi kukua kimuziki. Hata hivyo, wapo ambao walitaka kukata tamaa kutokana na wazazi wao kushindwa kuwasapoti na hawakutaka kabisa watoto wao wafanye kazi ya sanaa (muziki), wakiamini hawatafika kokote wakiwataka wasome, lakini baada ya kuamua kulazimisha wasanii hao sasa wamekuwa moto.
SANAA ni moja ya kazi zinazoingizia wasanii pesa nyingi kutokana na vipaji vyao. Kwenye tasnia ya burudani na hasa muziki, vipaji vimekuwa vikiibuka kila kukicha na kujitangaza ndani na nje ya mataifa yao.
Hakuna ubishi kila msanii anahitaji sapoti ili aanze, atoke au azidi kukua kimuziki. Hata hivyo, wapo ambao walitaka kukata tamaa kutokana na wazazi wao kushindwa kuwasapoti na hawakutaka kabisa watoto wao wafanye kazi ya sanaa (muziki), wakiamini hawatafika kokote wakiwataka wasome, lakini baada ya kuamua kulazimisha wasanii hao sasa wamekuwa moto.
Harmonize, Nandy, Davido, Tyla na wengine wengi, hawakuachana na ndoto zao na walizipigania na sasa wanafaidi vipaji vyao.
Katika mahojiano na vyombo mbalimbali vya habari, baadhi ya wasanii hao na hata watu wa familia zao wamewahi kusimulia changamoto walizokutana nazo kabla ya kufikia mafanikio yao ya sasa.
HARMONIZE-BABA ALIPINGA NDOTO YAKE
Rajab Abdul Kahali 'Harmonize', ni miongoni mwa wasanii wa Tanzania waliowahi kuzungumzia changamoto za kufuatilia ndoto za muziki.
Katika wimbo wake Never Give Up, Harmonize anasimulia mapambano aliyopitia kabla ya kupata mafanikio, yakiwemo changamoto za kifamilia. Aliwahi kuzungumza na baadhi ya vyombo vya habari na kusema baba yake alipinga uamuzi wake wa kuingia kwenye muziki, huku mama yake akimpa moyo wa kuendelea kupambana.
Kabla ya kujijengea jina, Harmonize aliwahi kufanya biashara ndogondogo ili kujikimu huku akifuatilia ndoto yake. Mwaka 2015 alipata nafasi ya kujiunga na WCB Wasafi, hatua iliyomfungulia milango ya kutambulika zaidi katika Bongo Fleva.
Baadaye alianzisha lebo yake ya Konde Music Worldwide na kuendelea kujijenga kama mmoja wa wasanii wanaotambulika katika muziki wa Tanzania.
NANDY- VIDEO ILIYOWAKWAZA WAZAZI
Faustina Mfinanga 'Nandy', aliwahi kukumbana na upinzani wa wazazi wake kuhusu kazi yake ya muziki.
Katika mahojiano ya mwaka 2019 kwenye baadhi ya vyombo vya habari, baba yake alieleza yeye na mkewe walifikia hatua ya kutaka kumzuia binti yao kuendelea na muziki baada ya video yake iliyowakwaza kusambaa mitandaoni.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, tukio hilo lilizua wasiwasi kwa wazazi wake kuhusu mwelekeo wa kazi yake. Hata hivyo, Nandy aliendelea na muziki na kujijengea nafasi katika Bongo Fleva kwa nyimbo kama 'Ninogeshe' na kazi nyingine zilizompa umaarufu ndani na nje ya Tanzania.
DAVIDO-BABA ALIFUTA MAONYESHO YAKE
Nchini Nigeria, David Adeleke 'Davido', alikumbana na upinzani kutoka kwa baba yake, Adedeji Adeleke, ambaye alitaka mwanaye atangulize elimu.
Katika mahojiano kwenye kipindi cha The Kelly Clarkson Show mwaka 2023, Davido alisimulia baba yake aliwahi kuingilia shughuli zake za muziki, ikiwemo kufuta baadhi ya maonyesho yake alipokuwa anaanza kujijenga.
Kwa maelezo yake, familia yake iliweka uzito mkubwa kwenye elimu, lakini yeye alikuwa na ndoto ya kufanya muziki. Hali hiyo haikumfanya aachane na kipaji chake.
Baadaye Davido alikamilisha masomo yake na kuendelea kujenga uhusiano mzuri na familia yake. Leo ni miongoni mwa majina makubwa ya Afrobeats duniani kwa nyimbo kama Fall, If na Unavailable.
TYLA-WAZAZI HAWAKUUAMINI MUZIKI
Kutoka Afrika Kusini, Tyla Laura Seethal 'Tyla', pia amewahi kusimulia changamoto ya kuwashawishi wazazi wake waamini ndoto yake ya muziki.
Katika mahojiano na Power 106 FM ya Los Angeles, Marekani, yaliyoripotiwa na vyombo vya habari, Tyla alisema wazazi wake walikuwa na wasiwasi kuhusu uamuzi wake wa kujikita kwenye muziki kwa sababu hawakuuona kama kazi yenye uhakika wa maisha.
Alieleza alijitahidi kuwashawishi wampe nafasi ya kujaribu, licha ya kutokubaliana kwao mwanzoni.
Juhudi zake zilizaa matunda kutokana na wimbo Water, uliovuma kimataifa na kumletea tuzo ya Grammy ya Best African Music Performance mwaka 2024.
MR FLAVOUR-MAMA ALITAKA AWE DAKTARI
Chinedu Okoli 'Mr Flavour' au 'Flavour N'abania', ni msanii mwingine aliyekutana na matarajio tofauti ya mzazi wake.
Katika mahojiano yaliyochapishwa na TheNet mwaka 2012, mama yake, Onyinyechukwu Jane Okoli alieleza alitamani mwanaye awe daktari. Alikuwa na wasiwasi kuhusu mazingira ya tasnia ya muziki na alitamani mwanaye ajikite zaidi kwenye muziki wa kanisani kama angeendelea na sanaa.
Hata hivyo, Flavour aliendelea kukuza kipaji chake na baadaye akajijengea jina katika muziki wa Nigeria kupitia nyimbo kama Nwa Baby (Ashawo) na Ada Ada.
Simulizi hiyo inaonyesha namna matarajio ya mzazi yalivyotofautiana na ndoto ya mwanaye, ambaye hatimaye alifanikiwa kujenga taaluma katika muziki.
CKAY-ALIAMINI NDOTO YAKE
Chukwuka Ekweani 'CKay', amewahi kuzungumzia namna alivyolazimika kusimamia ndoto yake licha ya kutofautiana na wazazi wake.
Katika mahojiano na mwandishi wa habari za muziki Joey Akan, CKay alieleza alitamani kujikita kwenye muziki, wakati familia yake ilikuwa na matarajio tofauti kuhusu maisha yake.
Aliondoka Kaduna na kuelekea Lagos kutafuta nafasi ya kujijenga katika tasnia ya muziki. Uamuzi huo ulimhitaji kuwa na ujasiri kwa sababu hakuwa na uhakika wa mafanikio.
Baadaye, wimbo wake Love Nwantiti, uliotolewa mwaka 2019, ulipata umaarufu mkubwa kimataifa na kumtambulisha kwa mashabiki wengi nje ya Nigeria.
BLACK WA USWAZI-FEDHA ZA SHULE ZIKAENDA STUDIO
Tanzania, Black wa Uswazi 'Black Mkwaju', amewahi kusimulia changamoto alizokutana nazo nyumbani alipokuwa akifuatilia muziki.
Katika mahojiano yaliyochapishwa na JamiiForums mwaka 2024, alieleza wazazi wake walitaka atangulize masomo. Hata hivyo, yeye alikuwa na hamu kubwa ya kufanya muziki.
Alisimulia aliwahi kutumia fedha za akiba za mama yake bila ruhusa ili kulipia gharama za kurekodi nyimbo studio. Uamuzi huo ulizua mgogoro nyumbani kwa sababu fedha hizo zilihitajika pia kwa matumizi ya shule.
Kwa mujibu wa simulizi lake, baadaye alimwomba mama yake msamaha na kumshawishi asikilize kazi alizokuwa amerekodi. Tukio hilo linaonyesha namna alivyokutana na mvutano wa kifamilia kabla ya kuendelea na safari yake ya muziki.