Hamisa Mobetto apewa nafasi UNESCO, afunguka mapambano ya mtandaoni
Muktasari:
- Hamisa ametambulishwa katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika leo Agosti 28, 2026 jijini Dar es Salaam, huku akieleza kuwa nafasi hiyo imegusa maisha yake kutokana na changamoto alizowahi kupitia kwenye mitandao.
Msanii na mfanyabiashara, Hamisa Mobetto, ametambulishwa kuwa UNESCO Global Champion, nafasi itakayompa jukumu la kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia na mitandao ya kijamii, hasa kwa wanawake na wasichana.
Hamisa ametambulishwa katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika leo Agosti 28, 2026 jijini Dar es Salaam, huku akieleza kuwa nafasi hiyo imegusa maisha yake kutokana na changamoto alizowahi kupitia kwenye mitandao.
Akizungumza katika mkutano huo, Hamisa amesema amewahi kukutana na unyanyasaji wa mtandaoni, uzushi na mashambulizi ya kidijitali.
“Nimepitia mwenyewe upande mwingine wa mitandao ya kijamii. Najua jinsi maneno, uzushi na mashambulizi ya mtandaoni yanavyoweza kumuathiri mwanamke,” amesema.
Hamisa amesema sasa anataka kutumia uzoefu huo kuwasaidia wanawake na wasichana wengine kutokuwa waathirika wa mazingira yasiyo salama mtandaoni.
“Sitaki kuzungumza kwa ajili yangu tu. Nataka kuzungumza kwa ajili ya msichana ambaye bado hajapata ujasiri wa kutumia sauti yake,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Communication and Information wa UNESCO Tanzania, Nancy Angulo, amesema uelewa wa vyombo vya habari na taarifa ni muhimu katika kuwasaidia vijana kuchambua taarifa, kutambua taarifa potofu na kutumia teknolojia kwa uwajibikaji.
Angulo amesema usalama wa wanawake mtandaoni unapaswa kupewa kipaumbele ili waweze kushiriki na kutoa maoni bila vitisho au udhalilishaji.
Naye Meneja wa Hamisa, Noel Mangoma, amesema nafasi hiyo inalenga kutumia ushawishi wa Hamisa katika jambo lenye manufaa kwa jamii.
“Hamisa amekuwa na jukwaa kubwa kwa muda mrefu, lakini tunachoangalia sasa ni namna ya kutumia jukwaa hilo kwa jambo lenye maana zaidi,” amesema.
Kupitia nafasi hiyo, Hamisa anatarajiwa kushirikiana na UNESCO katika kuelimisha vijana kuhusu matumizi sahihi ya mitandao na kuepuka kutoa taarifa za uongo, kufanya unyanyasaji wa mtandaoni na usalama wa kidijitali.