Hamisa Mobetto afunguka ya Aziz KI, siri ya ndoa yao na mahari ya ng'ombe
Muktasari:
- Hamisa amesema haya baada ya kutambulishwa kuwa UNESCO Global Champion, nafasi inayolenga kuhamasisha matumizi salama na yenye tija ya mitandao ya kijamii kwa wanawake na wasichana.
HAMISA Mobetto ambaye ni mwanamitindo na mfanyabiashara, amefunguka kuhusu maisha yake na mumewe, Stephane Aziz KI, huku akieleza pia namna anavyotazama mafanikio yake, ikiwamo mikataba mbalimbali ya ubalozi ambayo amekuwa akiipata.
Hamisa amesema haya baada ya kutambulishwa kuwa UNESCO Global Champion, nafasi inayolenga kuhamasisha matumizi salama na yenye tija ya mitandao ya kijamii kwa wanawake na wasichana.
Akizungumzia maisha yake ya ndoa na Aziz KI ambaye ni kiungo mshambuliaji wa Yanga na timu ya taifa ya Burkina Faso, Hamisa amesema hawakufanya uamuzi wa ndoa kwa haraka, akieleza kuwa walitumia muda kujenga uhusiano wao kabla ya kufikia hatua ya kufunga ndoa.
Kwa mujibu wa Hamisa, yeye na Aziz KI walikuwa kwenye mahusiano kwa takribani miaka mitatu kabla ya kuamua kuingia kwenye ndoa, huku wakichagua kutoweka kila hatua ya uhusiano wao hadharani.
Amesema kufanya hivyo kuliwasaidia kulinda maisha yao binafsi na kusubiri wakati sahihi wa kuweka mambo yao wazi.
“Tulikuwa kwenye mahusiano kwa muda, takribani miaka mitatu, kabla ya kuamua kuingia kwenye ndoa. Hatukuharakisha kuweka kila kitu wazi kwenye mitandao, tulisubiri wakati mwafaka,” amesema Hamisa.
SIRI YA MIKATABA YAKE
Hamisa pia amefunguka kuhusu namna anavyoendelea kupata mikataba ya ubalozi, akisema mafanikio hayo hayaji kwa bahati, bali yanahitaji nidhamu na kujituma.
Amesema anamshukuru Mwenyezi Mungu, huku akitaja kufanya kazi kwa bidii, kuheshimu mikataba na kuwa mwaminifu kwa kampuni anazofanya nazo kazi kuwa miongoni mwa sababu zinazomsaidia kuendelea kuaminiwa.
“Siri kubwa ya mafanikio yangu ni kumtanguliza Mwenyezi Mungu na kufanya kazi kwa bidii sana. Ninaheshimu kila fursa ninayopata na kufanya kazi kwa uaminifu na makampuni yanayonipa ubalozi,” amesema.
NG’OMBE WA HAMISA WAMEFIKIA WAPI?
Katika mazungumzo hayo, Mwanaspoti limemuuliza Hamisa kuhusu ng’ombe 30 wa mahari aliopewa wakati wa harakati za kufunga ndoa na Aziz KI, huku swali likiwa ni maendeleo yao yamefikia wapi, kama wameendelea kuzaana na kama kuna hatua nyingine iliyochukuliwa tangu alipopewa.
Hamisa amesema suala hilo kwa sasa linafahamika zaidi na mama yake, ambaye ndiye anayefuatilia maendeleo ya ng’ombe hao na kwakuwa ndio zinamuhusu yeye.
Kwa utani, Hamisa alifafanua kuwa yeye mwenyewe hakuchukua hata ng’ombe mmoja, hivyo hawezi kutoa maelezo ya moja kwa moja kuhusu idadi yao au maendeleo yaliyofikiwa.
“Hilo mama yangu ndiye analijua, kwa sababu mimi sikuchukua hata ng’ombe mmoja,” amesema Hamisa.
MITANDAO ILIVYOMJENGA
Hamisa amesema mbali na changamoto zake, mitandao ya kijamii imekuwa sehemu muhimu ya safari yake ya mafanikio, kwani imemsaidia kujenga jina, kupata mikataba na kukutana na fursa mbalimbali.
Amesema hata katika shughuli zake binafsi na kifamilia, matumizi mazuri ya mitandao yamekuwa na mchango, ikiwamo kuunganisha shughuli zao na makampuni yaliyokuwa tayari kushirikiana nao.
Kwa sasa, kupitia nafasi yake mpya ya UNESCO, Hamisa anasema anataka kutumia jukwaa alilonalo kuwafikia vijana, hasa mabinti, na kuwahamasisha kutumia teknolojia na mitandao kwa njia itakayowasaidia kujenga maisha yao badala ya kuwa chanzo cha madhara.