Grammy 2027 ni vita ya Tyla, Tems
Muktasari:
- Macho ya mashabiki wa muziki Afrika yataelekezwa kwenye kipengele hicho kutokana na uwepo wa wasanii waliotengeneza majina yao kimataifa, wakiwemo Tyla, Tems, Burna Boy, Davido, Asake na Wizkid.
Kipengele cha Best African Music Performance (Mtumbuizaji Bora wa Afrika), kinatarajiwa kuwa moja ya vizutio katika kinyang’anyiro cha Tuzo za Grammy za mwaka 2027.
Macho ya mashabiki wa muziki Afrika yataelekezwa kwenye kipengele hicho kutokana na uwepo wa wasanii waliotengeneza majina yao kimataifa, wakiwemo Tyla, Tems, Burna Boy, Davido, Asake na Wizkid.
Orodha ya majina ya wasanii watakaowania tuzo hizo, yanatarajiwa kuwekwa wazi leo, Novemba 16, ikiwa ni baada ya kazi mbalimbali kuwasilishwa kwa ajili ya kuzingatiwa na waandaaji wa tuzo hizo.
Tofauti na misimu ambayo baadhi ya wasanii walionekana kuwa na nafasi kubwa zaidi kutokana na umaarufu au mafanikio ya kazi zao, safari hii ushindani unatarajiwa kuwa mgumu zaidi.
Tyla ni miongoni mwa majina yanayovuta hisia, hasa baada ya mafanikio aliyoyapata kimataifa kutokana na muziki wake.
Mwanadada huyo si mgeni katika tuzo hizo, kwani tayari ameshinda tuzo hiyo mara mbili kwa kipengele cha Best African Music Performance.
Tuzo yake ya kwanza alishinda mwaka 2024 kupitia wimbo wa ‘Water’, kabla ya kutetea mafanikio hayo mwaka 2026 kupitia ‘Push 2 Start’, akiwashinda kina Burna Boy, Davido, Omah Lay, Ayra Starr na Wizkid.
Rekodi hiyo inamfanya aingie kwenye mjadala wa msimu huu akiwa na historia kubwa.
Kinachofanya kipengele hicho kiwe na ushindani ni uwepo wa jina la Tems kutoka Nigeria ambaye tayari ameshinda tuzo mbili za Grammy, mwaka 2023 kupitia ‘Wait For U’, aliomshirikisha Future na Drake, kabla ya kuchukua tena mwaka 2025 kupitia ‘Love Me JeJe’.
Mbali na ushindi huo, amepata uteuzi mara nane, jambo linaloonyesha mwendelezo wa uwepo wake katika ushindani wa tuzo hizo.
Upekee wa sauti yake, ubunifu na uwezo wa kuunganisha ladha za muziki wa Afrika na soko la dunia vinamfanya kuwa miongoni mwa majina yenye uzito katika kinyang’anyiro cha msimu huu.
Burna Boy naye anaingia kwenye mjadala huo akiwa na uzoefu mkubwa wa Grammy, akiwa ameteuliwa mara 13 na kushinda tuzo moja mwaka 2021 kupitia albamu ya Twice As Tall katika kipengele cha Best Global Music Album, mafanikio yaliyomuweka miongoni mwa wasanii wa Afrika walioandika historia kwenye tuzo hizo.