Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

GRAMMY 2026 Afrika patamu

Muktasari:

  • Ni tuzo kubwa zaidi za wasanii duniani zinazotambua ubora wa kazi kutoka kwa wanamuziki, waandaaji, wachekeshaji na sanaa nyingine, na hii ni mara ya 68 tangu kuanzishwa kwake 1959 Marekani.

NI usiku wa tuzo za muziki duniani.Macho na masikio ya wapenzi wa burudani yako Crypto.com Arena, Los Angeles, Marekani kushuhudia usiku wa tuzo za Grammy zinazotolewa kila mwaka zikitambua mchango wa wasanii.

Ni tuzo kubwa zaidi za wasanii duniani zinazotambua ubora wa kazi kutoka kwa wanamuziki, waandaaji, wachekeshaji na sanaa nyingine, na hii ni mara ya 68 tangu kuanzishwa kwake 1959 Marekani.

Sherehe hizo zitanogeshwa na burudani kutoka kwa wasanoo kama Bruno Mars, Lady Gaga, Justin Bieber, Sabrina Carpenter, Rosé, Tyler, the Creator, Pharrell Williams na Clipse watakaolishambulia jukwaa hilo kwa pafomansi zao.

Hadi sasa Beyonce anashikilia rekodi ya msanii anayeongoza kuwania tuzo hizo mara 99, ndiye msanii anayeshikilia rekodi ya msanii aliyechukua tuzo za Grammy mara nyingi zaidi akibeba mara 35 ndani ya miaka tofauti.


AFRIKA PATAMU

Mwaka huu Grammy imeongeza ushindani kwa wasanii wa Afrika baada ya kuweka idadi kubwa, tofauti na mwaka jana ambapo kwenye kipengele kimoja kiliwaniwa na wasanii watano pekee.

Mwaka jana Tems alishinda tuzo hiyo kupitia wimbo wa Love Me JeJe, akiwashinda Yemi Alade (Tomorrow), Asake & Wizkid (MMS), Chris Brown ft Davido & Lojay (Sensational) na Burna Boy (Higher).

Kiujumla, mwaka huu Afrika imeweka rekodi ya kuingiza wasanii tisa kuwania tuzo hizo, na kwenye kipengele cha Best African Music Performance kinashindaniwa na wasanii sita: Burna Boy (Nigeria) akiingia kwenye vinyang’anyiro viwili: Best African Music Performance kwa Love na Best Global Music Album kwa No Sign of Weakness.

Burna Boy ni mmoja wa wasanii wa Afrika waliokuwa na waliowania Grammy nyingi zaidi, akishindania 11 lakini alishinda Grammy yake ya kwanza mwaka 2021 kupitia albamu Twice As Tall.

Wasanii wengine wanaowania kwenye kipengele hicho ni Davido kutoka Nigeria, akiingia kupitia wimbo wa With You aliomshirikisha Omah Lay. Hii ni mara ya tatu nyota huyo anaingia kwenye tuzo hizo; mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2023 ambapo Tyla (Afrika Kusini) aliiondoka na tuzo hiyo kupitia wimbo wa Water.

Mwaka uliofuata, tuzo hiyo ikaenda kwa mwanadada Tems (Love Me Jeje), na mwaka huu ameingia tena.

Ayra Starr anaingia na wimbo wa Gimme Dat, akimshirikisha Wizkid, na anawania mara ya pili kwenye tuzo hizo; mara ya kwanza ilikuwa 2023 aliposhindwa kupenya mbele ya Tyla.

Wengine ni Tyla (Afrika Kusini) anawania kupitia wimbo wa Push 2 Start. Tyla alishinda Grammy yake ya kwanza kabisa mwaka 2024 katika kipengele cha Best African Music Performance kupitia wimbo Water, akawa msanii wa Kiafrika wa kwanza kushinda kipengele hicho.

Youssou N’Dour (Senegal) kupitia wimbo wa Éclairer le Monde (Light the World), ni msanii mwenye historia ndefu ya Grammy, akiwania mara ya saba sasa. Alishinda Grammy moja kabla (2005) kupitia albamu Egypt, ni nguli wa muziki wa Afrika waliotambuliwa kimataifa.

Mwingine ni mwanamama Angélique Kidjo (Benin / France), ndiye Mwafrika wa kwanza kuwania tuzo nyingi zaidi, 16, kati ya hizo ameshinda tano. Mwaka huu anawania kipengele cha Best Global Music Performance kupitia wimbo wa Jerusalema.

KENDRICK ATAVUNJA REKODI?

Hadi sasa rapa wa Marekani, Kendrick Lamar ndiye anaongoza kwa kuingia kwenye vipengele vingi (tisa). Hii ina maana kuwa ana nafasi kubwa ya kushinda tuzo nyingi, zaidi kuliko wasanii wote walioingia kuwania mwaka huu.

Kendrick ni mmoja wa wasanii waliofanikiwa zaidi katika historia ya tuzo za Grammy, na anaongoza kama mtu mwenye idadi kubwa ya ushindi kati ya marapa wa kizazi chake.

Tangu Kendrick aanze tasnia ya muziki 2003, amewania tuzo za Grammy mara 66 na kushinda tuzo 22. Hii inamfanya awe mmoja wa wasanii wenye tuzo nyingi zaidi duniani, hasa katika muziki wa hip‑hop.

Hii si mara ya kwanza kwa mkali huyo kuondoka na tuzo tano ndani ya usiku mmoja; mwaka jana alifanya hivyo na kumfanya kuwa mmoja wa wasanii walioongoza katika tuzo hizo.

Alinyakua tuzo ya Best Rap Album kupitia albamu yake ya GNX, wimbo bora wa rap (Best Rap Song) kwa wimbo Luther aliyemshirikisha SZA, kipengele kingine ni Best Rap Performance kupitia wimbo huo huo Luther akiwa na SZA, Best Song Written for Visual Media kwa wimbo wa Power kutoka kwenye filamu ya Black Panther: Wakanda Forever, na Best Music Video kwa video ya wimbo Luther.

Mwaka huu kuna upinzani mkubwa kwani mbali na Lamar kuingia kwenye vipengele vingi wapo wasanii wengine walioingia kwenye vinyang’anyiro vingi pia kina Lady Gaga, Cirkut na Jack Antonoff wakiwania mara saba, na Bad Bunny, Leon Thomas, na Sabrina Carpenter kila mmoja akiingia mara sita. Hapo ndipo ulipo ushindani wenyewe, kwani wote wanaowania vipengele vingi wamekutana mara tatu kwenye kipengele kimoja cha tuzo.