Finale ya King Kiba kuipiku Katam ya Mondi?
Muktasari:
- Ili kuivunja Katam, ni lazima kuwe na kampeni endelevu ya promosheni, ikiwemo matumizi ya TikTok, ushirikiano na watengeneza maudhui na mbinu za kuhakikisha wimbo unabaki kwenye trend.
NAMBA hazidanganyi. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya kuzuka mjadala kwenye mitandao ya kijamii kuhusu vita ya namba ya kazi mpya ya Bien wa kundi la Sautisol na mwanamuziki wa Tanzania, Ali Kiba, inayokwenda kwa jina la ‘Finale’ dhidi ya rekodi zilizowekwa na ‘Katam’, kolabo ya msanii huyo wa Kenya na Diamond Platnumz.
Kama unavyofahamu, Diamond na Alikiba wamekuwa wakifananishwa kwenye muziki wa Bongofleva kutokana na ubora wa kazi zao na namna walivyoupa heshima muziki huo hadi kimataifa.
Sasa vita ya kushindanishwa imehamia hadi kwenye kolabo walizofanya na mkali wa kundi la Sautisol, Bien, ambaye amejizolea umaarufu mkubwa Tanzania na hata Afrika.
Vita inayozungumzwa hapa ni ya namba, ushawishi na mikakati ya kidijitali iliyofanya kolabo hizo kuwa maarufu, kama ilivyo kwenye soka, ambapo takwimu huamua nani bingwa.
Mwanaspoti imekusogezea namba za kila kolabo. Kwanza, Finale, ndani ya muda mchache imefanya vizuri. Ndani ya siku mbili ilikuwa tayari imeingiza zaidi ya watazamaji milioni mbili kwenye mtandao wa YouTube.
Ukilinganisha na Katam, ndani ya siku mbili iliiingiza zaidi ya watazamaji milioni moja, hivyo kuna utofauti mdogo wa namba baina ya kolabo hizo mbili, lakini ni kama zinaendana.
Kasi ya Finale, ambayo hadi sasa ina zaidi ya watazamaji milioni tatu, ipo kwenye nafasi nzuri ya kufikia rekodi ya Katam ambayo, ndani ya miezi nane, ilifikisha watazamaji milioni 17.
Na hii ni kwa sababu Finale haijatangazwa kwa ukubwa kama ilivyo Katam, ambayo Diamond ndiye aliyemshirikisha Bien, hivyo ubora pekee wa nyimbo umefanya kuwa maarufu ndani ya muda mchache.
Kimahesabu, kama wimbo huu utaendelea kupata wastani wa watazamaji milioni moja kwa siku ama kwa wiki kadhaa, basi kufikia milioni 17 ndani ya mwezi mmoja inawezekana.
TOFAUTI ILIYOPO
Tofauti kati ya nyimbo hizo mbili ipo kwenye uimara wa muda mrefu. Katam haikuvuma siku mbili, bali ilikuwa na muendelezo wa kusikilizwa na kukusanya watazamaji milioni 17 ndani ya miezi nane.
Inaonyesha kuwa ngoma hiyo ilikuwa na kitu cha ziada kuanzia kwenye promosheni, ubora wa video na sauti.
Katika pambano la wawili, ni kama Bien anaonekana kuwa kiungo muhimu kama mchezaji wa kati anayesambaza mipira pande zote mbili.
Ana mashabiki wengi Kenya, Tanzania na hata nje ya Afrika Mashariki. Kupitia Katam alishirikiana na Diamond kutikisa soko la Tanzania, na sasa kupitia Finale anarudi tena, safari hii akiwa na Alikiba.
Lakini hii si mara ya kwanza King kufanya kazi na Bien. Awali walifanya kolabo ya 'Unconditionally Bae' na kundi la Sautisol na Mkenya huyo akiwemo ndani, ngoma ikafanya vizuri sana miaka 10 iliyopita.
Miaka minne iliyopita akafanya tena kolabo na kundi hilo, wakati huo Alikiba waliwashirikisha kupitia wimbo wa 'Let Me'.
Hivyo, rekodi ya kolabo zao kufanya vizuri miaka iliyopita inaifanya Finale kuwa na nguvu ya kuvuka mipaka, ikiunganisha mashabiki wa nchi mbili kwa wakati mmoja.
Hata hivyo, nguvu ya Diamond kwenye muziki wa Afrika ni kubwa.
Diamond sio msanii pekee bali ni taasisi ya muziki. Mkali huyo ana mtandao wake wa WCB Wasafi, ana uwezo mkubwa wa kusukuma kazi zake kimkakati.
'Katam' ilinufaika sana na promosheni kali, ushawishi wa mitandao ya kijamii na ushiriki wa watengeneza maudhui.
Kwa upande wa Alikiba, anajulikana zaidi kwa ubora wa muziki kuliko mbwembwe za promosheni. Ni kama mchezaji mwenye kipaji kikubwa lakini asiye na makelele mengi nje ya uwanja. Mashabiki wake wanaaminika kuwa waaminifu na wanaopenda kazi zenye ladha ya kudumu.
Hii inaweza kuipa Finale nguvu ya kukaa muda mrefu sokoni, hata kama haitavuma kila siku.
Jambo lingine muhimu ni ubunifu wa video. Zama za sasa, YouTube sio sehemu ya kusikiliza tu bali pia kutazama. Video yenye hadithi nzuri, ubora wa picha na mvuto wa kipekee inaweza kuongeza idadi ya watazamaji.
Baadhi ya maoni ya mashabiki wanasifia ubora wa sauti za wasanii hao lakini hawakuwekeza zaidi kwenye video.
Kwa ujumla, 'Finale' ina kila sababu ya kuwa tishio kwa rekodi ya Katam kwani ina mwanzo mzuri, ina muunganiko wa wasanii wenye nguvu na ina uwezo wa kuvuka mipaka ya soko.
Lakini, kama ilivyo kwenye michezo, ubingwa haupatikani kwa kuanza vizuri pekee bali unahitaji nidhamu, mkakati na uimara wa muda mrefu.
Ili kuivunja Katam, ni lazima kuwe na kampeni endelevu ya promosheni, ikiwemo matumizi ya TikTok, ushirikiano na watengeneza maudhui na mbinu za kuhakikisha wimbo unabaki kwenye trend.
Kwa Alikiba, hilo halionekani kwani hadi wimbo unafanya vizuri umejiuza wenyewe kwa ubora wa kazi, lakini hajafanya promosheni nyingi.
Tofauti na Diamond, ambaye amekuwa akitumia mbinu mbalimbali za kuusambaza muziki wake, ndiyo maana ndani ya muda mchache baada ya kuuachia huwa unafanya vizuri.
MSIKIE MWENYEWE
Baada ya kolabo hiyo, Bien anasema, "namshukuru Ali kwa kukubali kushirikiana na mimi kwenye kazi hiyo, mambo ya kushindanishwa ngoma hiyo na Katam ya Diamond sipendi hayo mambo."