Fally Ipupa avuta warembo Lugalo
Muktasari:
- Katika shoo hiyo iliyofurika mashabiki, wanawake walionekana kujitokeza kwa wingi huku wengi wao wakivutia kwa mavazi na mwonekano wao, hali iliyoongeza ladha ya mandhari ya tukio hilo.
SHOO ya mwanamuziki nyota kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Fally Ipupa, iliyofanyika usiku wa kuamkia leo Novemba 29, 2026, katika viwanja vya Lugalo Golf Course, Kawe, Dar es Salaam, haikuwa burudani ya muziki pekee, bali pia ilivutia idadi kubwa ya wanawake waliojitokeza kushuhudia makamuzi ya mwanamuziki huyo.
Katika shoo hiyo iliyofurika mashabiki, wanawake walionekana kujitokeza kwa wingi huku wengi wao wakivutia kwa mavazi na mwonekano wao, hali iliyoongeza ladha ya mandhari ya tukio hilo.
Mwanaspoti lilizungumza na baadhi ya wanawake waliohudhuria shoo hiyo, akiwamo Stella Peter, aliyesema alivutiwa na Fally kutokana na namna anavyocheza jukwaani, hasa umahiri wake wa kukata mauno.
Stella amesema hilo ndilo lililomshawishi kuhudhuria onyesho hilo na kwamba alilipa tiketi ya VIP ili kushuhudia burudani hiyo kwa ukaribu zaidi.
Mwanamke mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Marry Alphonce, ameliambia Mwanaspoti kuwa ameamua kufika Lugalo kwa sababu alikuwa hajawahi kumuona Fally akiimba moja kwa moja, hivyo alitaka kupata nafasi ya kumshuhudia.
Ameongeza kwamba, alikuwa na hamu ya kuusikiliza wimbo wa “May Day” ukiimbwa live, kwani anapenda namna Fally anavyoimba.
Fally alitumia takribani saa tatu jukwaani akiimba live, akiwapa mashabiki nafasi ya kufurahia nyimbo zake na kushuhudia uwezo wake wa kutawala jukwaa.