Diamond: Mapacha kibao kama Michael Jackson
Muktasari:
- Kupitia mitandao ya kijamii, tumeshuhudia vijana wengi wanaofanana na Diamond wakijaribu kufanya mambo mbalimbali kama yeye, yakiwamo kufanya maonyesho, kuvaa mavazi yanayofanana na yake au kutumbuiza kwa mtindo wake. Jambo hilo limekuwa likiwafurahisha mashabiki wengi.
TANGU mwaka 2009, jina la Diamond Platnumz limeendelea kuwa maarufu katika tasnia ya muziki. Umaarufu wake sasa umegeuka kuwa fursa kwa vijana wenye muonekano unaofanana naye, jambo ambalo limewahi pia kuonekana kwa mwanamuziki Michael Jackson.
Kupitia mitandao ya kijamii, tumeshuhudia vijana wengi wanaofanana na Diamond wakijaribu kufanya mambo mbalimbali kama yeye, yakiwamo kufanya maonyesho, kuvaa mavazi yanayofanana na yake au kutumbuiza kwa mtindo wake. Jambo hilo limekuwa likiwafurahisha mashabiki wengi.
Kwa sasa, anavuma kijana mmoja kutoka Katoro, Geita, anayetambulika kama ‘Diamond Mwitu’. Amekuwa akitumbuiza nyimbo za msanii huyo katika maeneo ya wazi na kuvutia watazamaji wengi. Kwa kumtazama kwa haraka, unaweza kudhani ndiye Diamond mwenyewe, lakini si yeye.
Kijana huyo anaungana na mwingine anayefahamika kama ‘Pacha wa Mondi’, ambaye ni maarufu sana Instagram. Hapo awali pia alikuwepo Mondi mwingine wa mchongo aliyejitokeza katika video ya wimbo wa Harmonize, ‘Ushamba’ (2020), ambao baadhi ya mistari yake ilikuwa na vijembe kwa Diamond.
Vijana hao wamekuwa wakifanya mahojiano na baadhi ya vyombo vya habari, hasa vya mtandaoni, huku wengine wakipata dili za matangazo madogomadogo na kujipatia kipato.
Kadiri matumizi ya mitandao ya kijamii yanavyozidi kushika kasi, vijana wanaofanana na Mondi wanajikuta katika ulimwengu mwingine wa uzalishaji wa maudhui (content creation), kazi ambayo imekuwa chanzo cha ajira kwa vijana wengi wenye vipaji.
Anko Nzala, mtengeneza maudhui (content creator) maarufu nchini Tanzania mwenye wafuasi (followers) zaidi ya milioni 10.8 kwenye TikTok, ni miongoni mwa waliomshirikisha ‘Diamond Mwitu’, ambaye amefika Dar es Salaam kwa ziara maalumu akitokea Katoro.
Wawili hao wametengeneza video iliyowavutia watu kwenye Instagram na Facebook, ambapo wamefanya changamoto ya kucheza wimbo mpya wa Zuchu na Diamond Platnumz, ‘Mvua ya Baraka’ (2026). Wimbo huo unafanya vizuri kwa sasa na ni kolabo ya sita kwa wanamuziki hao wa WCB Wasafi.
KWANINI DIAMOND?
Wanamuziki kama Harmonize, Marioo, Jux na Mbosso wamewahi kuwa na watu wanaofanana nao, ambao nao wamejitokeza mtandaoni na baadhi yao hata kutoa nyimbo zao. Lakini kwa nini wanaofanana na Diamond ndio wan aopata umaarufu zaidi?
Vijana wanaofanana na Diamond wanapata umaarufu kwa sababu msanii huyo ana mashabiki wengi, hasa kwenye mitandao ya kijamii. Hivyo, vijana hao hupata uungwaji mkono kutoka kwa watu wengi, jambo linalochangia kuibuka kwa wengine wapya mara kwa mara.
Diamond, mwanzilishi wa WCB Wasafi, ndiye msanii mwenye wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii kuliko msanii mwingine yeyote nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Diamond anaongoza Instagram akiwa na wafuasi milioni 19, Facebook akiwa na milioni 8.2 na YouTube akiwa na milioni 12. Hata hivyo, anashika nafasi ya pili kwenye X, zamani Twitter, akiwa na wafuasi milioni 1.3, na TikTok akiwa na milioni 11.5, akitanguliwa na mtengeneza maudhui Zero Brainer.
KUNA MICHAEL JACKSON
Hata baada ya kifo cha mwanamuziki wa Marekani, Michael Jackson, aliyekuwa akifanya muziki wa miondoko ya Pop, R&B na Soul, watu wengi duniani wanaofanana naye wameibuka na kupata umaarufu kupitia jina lake.
Michael Jackson, aliyefariki dunia mwaka 2009, ameacha alama kubwa katika muziki, dansi na filamu. Watu wanaofanana naye na kuiga mitindo yake ya uchezaji na mavazi hufanya hivyo kwa lengo la kuenzi urithi wake katika tasnia ya burudani.
Mmoja wa watu hao ni Sergio Cortes kutoka Hispania. Mwanamume huyo anafanana kwa kiasi kikubwa na Michael Jackson, jambo linalowavutia watu wengi .