Diamond: kimataifa? fanya hivi utatoka
Muktasari:
- Kwa mtazamo wake, jukwaa la kimataifa linaanzia kwenye muziki wenye uwezo wa kuvuka mipaka. Na kwake mwenyewe, safari kutoka Tanzania hadi zaidi ya nchi 30 za Afrika ndiyo mfano anaoutumia.
UKITAKA kujua kwa nini Diamond Platnumz amekuwa akionekana mara kwa mara kwenye majukwaa makubwa nje ya Tanzania, safari yake ya muziki inatoa jibu moja, amejenga kazi inayoweza kuvuka mipaka.
Akizungumzia wasanii wanaotamani kufanya shoo nje ya nchi, Diamond amewataka wenzake wa Bongo Fleva kuanzia kwenye msingi wa muziki wao, akisisitiza umuhimu wa kutoa nyimbo zenye uwezo wa kufanya vizuri kimataifa.
Kauli hiyo ameitoa baada ya kutumbuiza Lusaka, Zambia, ambako alipata mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki. Shoo hiyo imekuwa sehemu ya mwendelezo wa safari yake ya kutumbuiza katika nchi mbalimbali za Afrika.
Kwa sasa Diamond ni miongoni mwa wasanii wa Tanzania wenye ratiba kubwa ya maonyesho ya kimataifa. Hivi karibuni pia alitumbuiza Kigali, Rwanda, akiendeleza safari yake ya muziki katika soko la Afrika.
Safari yake imefika katika zaidi ya nchi 30 Afrika, jambo linaloonyesha ukubwa wa soko alilolijenga nje ya Tanzania. Kutoka Afrika Mashariki hadi maeneo mengine ya bara, Diamond amekuwa akitumia shoo, muziki na ushirikiano na wasanii wa mataifa mbalimbali kuendelea kuipanua Bongo Fleva.
Moja ya mambo yaliyomsaidia ni kutengeneza muziki wenye ladha inayoweza kufika kwa wasikilizaji wa mataifa tofauti. Pia amefanya kolabo na mastaa mbalimbali wa Afrika na nje ya bara, akiwemo Davido, Omarion, Ne-Yo na Alicia Keys, hatua iliyoongeza jina lake kwenye ramani ya muziki wa kimataifa.
Kwa mtazamo wake, jukwaa la kimataifa linaanzia kwenye muziki wenye uwezo wa kuvuka mipaka. Na kwake mwenyewe, safari kutoka Tanzania hadi zaidi ya nchi 30 za Afrika ndiyo mfano anaoutumia.