Alikiba anavyokula sahani moja na Gen Z
Muktasari:
- Lakini, ukiuliza ni nani anayeongoza kutoa nyimbo mara kwa mara, utaambiwa tena ni Diamond, huku Alikiba akiwa na tabia ya kutoa nyimbo chache, ingawa zinadumu muda mrefu kwenye masikio ya watu.
UKIAMBIWA utaje majina ya wasanii wakubwa wawili hapa Tanzania, utasema Diamond Platnumz na Alikiba, ambao kama ingekuwa soka, basi ni Simba na Yanga kwa upande wa ushindani.
Lakini, ukiuliza ni nani anayeongoza kutoa nyimbo mara kwa mara, utaambiwa tena ni Diamond, huku Alikiba akiwa na tabia ya kutoa nyimbo chache, ingawa zinadumu muda mrefu kwenye masikio ya watu.
Kuna wakati msanii anafika hatua ambayo jina lake pekee linatosha kumrudisha kwenye kumbukumbu za mashabiki, lakini kwa Alikiba inaonekana hataki kuishi kwa nguvu ya historia pekee. Katika miaka ya hivi karibuni, hasa mwaka 2026, amekuwa akionyesha upande mwingine wa muziki wake, akijaribu kusoma kasi ya kizazi kipya na kuingia kwenye mazingira ambayo Gen Z wamezoea.
SAUTI ILEILE, LADHA MPYA
Alikiba anayefahamika kwa sauti yake tulivu, melodi na nyimbo zilizobeba zaidi hisia za mapenzi, sasa anaonekana kuongeza vitu vipya kwenye muziki wake.
Sauti, midundo, namna ya kuwasilisha kazi na hata aina ya wasanii anaoshirikiana nao vinaonyesha hataki kubaki sehemu moja aliyozoeleka. Hii siyo kusema ameachana na Alikiba wa zamani, bali anaongeza sura nyingine kwa mashabiki wake na muziki wake kwa jumla.
KUENDANA NA GEN Z
Aliwahi kulizungumzia hilo katika mahojiano ya Mei 2026, akisema amekuwa akibadilisha midundo na kujibrandi mara kadhaa ili kuwafikia wasikilizaji wa kizazi kipya, akitaja wazi Gen Z kama sehemu ya hadhira anayolenga.
“Mazingira ya muziki yanabadilika na msanii anatakiwa kuelewa kile ambacho sekta inahitaji,” alisema Alikiba.
Kwa sasa, Alikiba si msanii anayesubiri wimbo utoke kisha kuwaachia mashabiki jukumu la kuusukuma, kwani katika kizazi hiki cha kidijitali, matumizi ya TikTok na YouTube yamekuwa sehemu muhimu ya kutangaza na kukuza muziki.
Kwa kizazi kinachokutana na muziki kupitia simu na mitandao, msanii lazima awepo pia kwenye mazingira hayo. Mwaka huu, hilo limeonekana pia kwenye uchaguzi wake wa washirika.
HAKUTAKA KUBAKI KWENYE HISTORIA
Mwaka huu, hilo lilionekana pia kwenye uchaguzi wake wa washirika. Alianza na Bhuju, akimshirikisha Mbosso, msanii ambaye yuko kwenye kizazi cha sasa cha Bongo Fleva. Wimbo huo ulitoka Mei 2026 na umefikisha zaidi ya watazamaji milioni 10 YouTube.
Kisha wimbo wa Finale, uliotoka mwezi Machi 2026, ushirikiano wake na Bien wa Kenya. Hapa Alikiba alitoka nje ya mipaka ya Tanzania na kuungana na msanii mwenye nguvu kwenye kizazi cha sasa cha muziki wa Afrika Mashariki na una watazamaji zaidi ya milioni 50.
Baada ya hapo alitoa wimbo wa Utanionea akiwa na Harmonize, ushirikiano uliowakutanisha wasanii wawili wenye mitindo tofauti, lakini wenye uwezo wa kufikisha muziki kwa hadhira kubwa. Wimbo huo ulitolewa Juni 5, 2026.
Kinachovutia zaidi ni kwamba Alikiba hakusubiri kushirikishwa pekee, kwani aliendelea kutoa kazi zake mwenyewe, ikiwa ni pamoja na Hater, iliyotoka Septemba 4. Ni mfano wa Alikiba akiendelea kusukuma muziki wake binafsi, huku akiweka ujumbe unaozungumzia chuki, wivu na watu wanaopinga mafanikio ya mwingine.
ANABADILIKA BILA KUMPOTEZA ALIKIBA WA ZAMANI
Kwa hiyo, kwa mwaka 2026 picha inayojitokeza ni ya Alikiba anayekwenda sambamba na kizazi kipya, huku akiendelea kubeba alama na utambulisho uliomjenga tangu mwanzo wa safari yake ya muziki.
Bado ana sauti yake, bado ana uwezo wa kuimba mapenzi, lakini sasa anaongeza midundo, collaborations na njia mpya za kuifikisha kazi yake kwa wasikilizaji kwa ukubwa zaidi.
Hapo ndipo swali la msingi linapokuja: je, Alikiba anabadilika kwa sababu muziki umebadilika au anajaribu kuhakikisha kizazi kipya kinamjua zaidi ya jina la Cinderella, Aje na Mapenzi Run Dunia? Ukweli ni kwamba hatua zake za sasa zinaonyesha hataki kuwa msanii anayeheshimiwa kwa historia tu.
Kwa msanii aliyedumu muda mrefu kama yeye, kuendelea kubadilika ni sehemu ya safari. Gen Z hawakumkuta Alikiba akianza, kwani walimkuta tayari akiwa jina kubwa.
Sasa, kazi yake ni kuhakikisha kizazi kipya kinamjua pia Alikiba wa leo. Kwa mwaka huu, kila dalili zinaonyesha kuwa anaendelea kufanya hivyo hatua kwa hatua.
KIMATAIFA KAUWASHA
Kolabo ya mwisho ya kimataifa aliyoifanya Alikiba, inaitwa 'Finale'.
Katika wimbo huu uliotoka katikati ya mwaka 2026, Alikiba ameshirikiana na msanii nguli wa muziki wa Afro-pop kutoka Kenya, Bien, aliyekuwa mwanachama wa kundi la Sauti Sol.
Wimbo huu umepata mafanikio makubwa sana ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na ulishika nafasi ya kwanza kwenye chati za Spotify (Spotify’s Global Impact List H1 2026) kama moja ya kolabo kubwa zilizovuka mipaka.