Kutoka Pah One Navy Kenzo hadi Aika & Nahreel
Muktasari:
- Tangu kipindi cha Pah One hadi kuja kuzaliwa kwa Navy Kenzo, na sasa zama mpya za Aika & Nahreel, hii ni simulizi nyingine iliyojiandika kwa upekee wake!.
Kwa miaka takribani 18, harakati za kimuziki za wasanii wa Bongo Fleva, Aika & Nahreel zimebeba sura mbalimbali baada ya kupitia vipindi vingi vya kimageuzi ambavyo vililenga kuwafanya kuwa bora zaidi ya hapo awali.
Tangu kipindi cha Pah One hadi kuja kuzaliwa kwa Navy Kenzo, na sasa zama mpya za Aika & Nahreel, hii ni simulizi nyingine iliyojiandika kwa upekee wake!.
Wakiwa Pah One na Navy Kenzo, walitambulika kama kundi ila sasa wanakuja kama wasanii wawili wanaofanya kazi pamoja (duo) na si kundi tena. Ni Aika & Nahreel, wala si Navy Kenzo tena, ukurasa huo ulishafungwa.
Kwa sasa wawili hao wanatamba na albamu yao mpya, Steppa (2026) ambayo imetoka hivi karibuni ikiwa na nyimbo 10 na baadhi Nahreel amehusika moja kwa moja katika utayarishaji wake kupitia studio yake, The Industry.
Steppa ni albamu inayozungumzia safari ya maisha, ukuaji, kujitambua na kuendelea kusonga mbele katika kila hatua ya maisha, huku ikiwapa mashabiki ladha mpya ya muziki ambao ni ubunifu mpya kutoka kwa wasanii hao.
Hii ni albamu yao ya kwanza tangu wamefanya mabadiliko ya jina au utambulisho wao katika muziki huu ambao umewapa heshima kubwa.
Mnamo Julai 2025, Nahreel na Aika ambao walikuwa akitambulika kama kundi la Navy Kenzo walitangaza kufika ukomo wa matumizi ya jina hilo la kundi na kueleza watatumia majina yao.
Katika taarifa yao kwa umma walieleza tangu mwanzo wa safari yao ya muziki, mashabiki wamekuwa pamoja nao wakiwapa moyo, nguvu na kuwaonyesha upendo usio na mwisho lakini wakati wa mabadiliko umefika.
“Tunatangaza rasmi jina letu la kisanii ‘Navy Kenzo’ linafika mwisho wake na tunaanza ukurasa mpya tukiitwa: Aika & Nahreel. Hatubadili kiini cha muziki wetu, bali tunaufanya uwe wa karibu zaidi, halisi zaidi na wa kweli kwetu kama wasanii na watu binafsi.
“Kwa wote mlioamini katika sisi, mkashika mikono yetu na kutembea nasi, tunaw ashu kuru kwa dhati. Upendo wenu ndio umetufikisha hapa. Na upendo wenu huo huo ndiyo unatusukuma katika sura hii mpya. Yours Truly. Aika & Nahreel,” taarifa yao ilieleza.
Hivyo sasa ni mwaka mmoja tangu wameanza kutambulika kama Aika & Nahreel, na ndipo wamekuja na albamu hiyo ikiwa ni ya nne kutoka kwao kwa jumla.
Ikumbukwe wakiwa kama Navy Kenzo waliweza kuachia albamu tatu, ambazo ni AIM (Above Inna Minute) (2016), Story Of The African Mob (2020) na Most People Want This (2023).
Kundi la Navy Kenzo lilianzishwa mwaka 2013 baada ya wawili hao kujiondoa katika kundi la Pah One, moja ya sababu zinazotajwa nyuma ya uamuzi huo ni pamoja na uhusiano wao wa kimapenzi.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Nahreel akiongea na kipindi cha Mkasi, waliachana na Pah One baada ya wao kuwekwa kando katika shoo ambayo walipaswa kutumbuiza pamoja kama kundi, hivyo kuanzia hapo na wao wakajiweka pembeni.
Mbali na Aika na Nahreel, wanamuziki wengine waliounda kundi la Pah One ni pamoja na Ola na Igwee ambao kwa sasa hawasikiki kwa sana. Nyimbo zao za mwanzoni ni kama I Wanna Get Paid, Ghetto n.k.
Hivyo Nahreel na Aika ambao walifahamiana tangu mwaka 2008 wakiwa wanasoma India, wakaanzisha Navy Kenzo ambapo walipata mafanikio makubwa. Wimbo wa kwanza kuwatambulisha unaitwa Chelewa (Bokodo) (2014).
Baadaye walifunika zaidi kupitia nyimbo zao kama Game (2015) wakimshirikisha Vanessa Mdee, Kamatia (2016), Feel Good (2016), Fella (2018), Manzese (2018) na Katika (2018) wakishirikiana na Diamond Platnumz.
Jambo nzuri ni kwamba nyimbo zote hizo Nahreel ndiye amezitengeneza kwa mikono yake mwenyewe kama mtayarishaji, huku director kutokea nchini Afrika Kusini, Justin Campos akiongoza video karibia zote hizo.
Huyu Justin Campos pia amesimama video za nyimbo zao mpya, Weird (2026) na Blood, Sweat & Tears (2026), yeye ndiye amehusika ila awamu amechang anya na teknolojia ya Akili Unde, yaani Artificial Intelligence (AI) ambayo sasa matumizi yake yameshika kasi duniani.
Ikumbukwe mbali na muziki wao, Aika & Nahreel ni wapenzi wakiwa tayari wana watoto wawili ambao walionekana katika utambulisho (trailer) wa albamu yao ya pili, Story Of The African Mob (2020) ambayo ilitoka ikiwa na nyimbo 12.