Diamond azungumzia kwa mara ya kwanza ishu ya baba yake

Habari kubwa wiki iliyopita kwa mashabiki wanaofuatilia maisha yasiyoishiwa visa na mikasa ya msanii wa muziki kutoka Tanzania, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ ilikuwa ni taarifa kwamba mtu anayefahamika kuwa ni baba mzazi wa Diamond, mzee Abdul Isaack sio baba yake mzazi.

Taarifa hiyo ilitolewa na mama mzazi wa Diamond, Sanura Kasimu ‘Mama Dangote’ kupitia mahojiano kwa njia ya simu yaliyofanywa katika kipindi cha Wasafi FM cha Mashamsham kinachoongozwa na mtangazaji Dida Shaibu.

Mama Dangote alipasua kwamba baba mzazi wa Diamond si mzee Abdul kama ilivyokuwa inafahamika na wengi na badala yake alisema baba wa damu wa msanii huyo anaitwa Salum Nyange ambaye kwa sasa ni marehemu.

Hata hivyo, Diamond amekuwa kimya kwa kipindi chote cha sekeseke hilo lakini leo amelizungumzia kwa mara ya kwanza.

Akijibu moja ya maswali katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo, Januari 19 kwenye ofisi za Wasafi TV na Redio kwa ajili ya kuongelea tamasha la Tumewasha Diamond amesema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa badala yake atatafuta muda wa kujibu.

“Samahani sana mwandishi, siwezi kuongelea mambo ya kitandani hapa. Naomba kaa na swali lako, nitakuja kujibu yote siku sio nyingi,” amesema Diamond.

Vuta n’kuvute ya nani baba wa damu wa msanii huyo imeendelea kuwa na joto kali huku upande wa pili, yaani kwa mzee Abdul akidai kuwa Diamond ni mwanaye.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya Simu alisema; “Ninachokifahamu Diamond ni mwanangu. Nilimpokea tangu siku ya kwanza anatoka hospital amana. Na nikamlea. Lakini kwa sababu mama yake kasema mimi sio baba yake, sawa, nimekubali, nachukulia kama huyo mtoto hakuwa riziki yangu.” alisema.