Angelique Kidjo pilato bato la Diamond, Ayra Starr
Muktasari:
- Mjadala huo uliibuka baada ya kusambaa kwa video katika mitandao ya kijamii ikimuonyesha Ayra Starr akimtazama Diamond kwa mshangao wakati akitumbuiza nchini Zambia hivi karibuni.
MWANAMUZIKI kutoka Benin mwenye makazi yake Paris nchini Ufaransa, Angelique Kidjo, ni kama amekuja kutoa jibu la mjadala uliokuwa ukiendelea ukimuhusisha staa wa Bongofleva, Diamond Platnumz na Ayra Starr wa Nigeria.
Mjadala huo uliibuka baada ya kusambaa kwa video katika mitandao ya kijamii ikimuonyesha Ayra Starr akimtazama Diamond kwa mshangao wakati akitumbuiza nchini Zambia hivi karibuni.
Wapo waliosema alipagawa na show ya Diamond, huku wengine wakisema Ayra Starr ni mkubwa kimuziki kuliko Diamond, hivyo si kwamba alikoshwa na show bali alikuwa akimshangaa kwanini anatumia nguvu kubwa kucheza jukwaani badala ya kujikita kuimba.
Ghafla mjadala ukabadilika na kuanza kuwapambanisha Diamond na Ayra, ikawa nani ni mkubwa kimuziki kuliko mwenzake?, na nani anafanya vizuri kimataifa kwa sasa? Hata hivyo, kile alichofanya Angelique Kidjo kuelekea tuzo za 68 za Grammy 2027, kinaweza kutupa picha ya maswali hayo kwa upande mmoja.
Aprili 2026, Angelique Kidjo aliachia albamu yake inayokwenda kwa jina la Hope!! ikiwa na nyimbo 16, kati ya wanamuziki walioshirikishwa katika albamu hiyo ni pamoja na Diamond na Ayra Starr. Diamond alisikika katika wimbo uitwao Kakua, na Ayra Starr katika wimbo, Aye Kan (Are You Coming Back).
Kutokana na mafanikio ya Angelique Kidjo kimataifa akishinda tuzo tano za Grammy, wengi walitegemea ataweza kumbeba au kumpa Diamond fursa ya kuwania tuzo hizo kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, hilo halijatokea kwa sababu kuelekea Grammy 2027, hajaupendekeza wimbo wake na Diamond kwenda katika mchakato wa kupata nafasi ya kuwania tuzo hizo.
Baada yake, Angelique Kidjo amependeza kolabo yake na Ayra Starr ndio iwanie kile kipengele maalumu kwa ajili ya muziki wa Afrika cha Best African Music Performance ambacho kilianzishwa mwaka 2023. Pia kolabo yake na Quavo na Pharrell Williams 'Bando' ameipendekeza katika vipengele vingine.
Kwa matokeo hayo, ni wazi kuwa Angelique Kidjo ameona kolabo na Ayra Starr inaweza kupata nafasi ya kuwania na hata kushinda kuliko ile na Diamond, au amejiridhisha kuwa Ayra Starr anafanya vizuri kimataifa kuliko Diamond, hivyo ikampa sababu ya kumchagua.
Ikumbukwe Ayra Starr ana rekodi ya kuwania tuzo za Grammy ila Diamond hana!, hata kama wewe ndio ungekuwa Angelique Kidjo angechagua kwenda na nani kati ya wawili hao?. Ayra Starr aliwania Grammy 2024 kupitia wimbo wake 'Rush', akarejea tena 2026 kupitia wimbo 'Gimme Dat' akiwa na Wizkid.
Kwa kifupi, Diamond anaweza kuwa mwanamuziki mkubwa Afrika kuliko Ayra Starr kwa data za ujumla, lakini ukweli kwa wakati huu Ayra Starr anafanya vizuri kimataifa kuliko Diamond.
Ayra Starr amethibitisha hilo hivi majuzi baada ya kuweka rekodi kama mwanamuziki wa kwanza kutokea Afrika kutumbuiza katika kipindi cha mapumzikoni (halftime show) katika mchezo wa NFL International Games, ambapo Philadelphia Eagles na Jacksonville Jaguars zilikuwa uwanjani.
NFL International Game ni mchezo wa Ligi ya Soka Marekani (NFL) ambao huchezwa nje ya taifa hilo kwa lengo kukuza mchezo huo kimataifa. Sasa Ayra Starr alitumbuiza katika tukio hilo lilofanyika Uingereza katika Tottenham Hotspur.
Ayra Starr aliimba nyimbo zake kadhaa zikiwemo 'Rush' na 'Heaven Baby' unaofanya vizuri kwa sasa ukitokea katika albamu yake ya tatu, Starrgirl (2026).
Mafanikio hayo yamekuja miezi michache tangu ashiriki katika albamu maalum ya Kombe la Dunia 2026, ambapo alisikika katika wimbo 'Show Me' akishirikiana na rapa wa Marekani, Latto.
Ayra Starr anapepea kwa kasi kimataifa baada ya mwaka uliopita kusaini makuliano na kampuni ya Jay Z, Roc Nation. Makubaliano hayo ya usimamizi wa kazi zake, yanalenga kumtafutia masoko mpya na makubwa Ulaya na Marekani ambapo anaishi kwa sasa.
Roc Nation inatumia mtandao wake kuiuza chapa (brand) ya Ayra Starr, kumtafutia show, mikataba ya kibiashara, na fursa nyingine zitakazoongeza thamani ya muziki wake. Hata hivyo, bado msanii huyo anaendelea kufanya kazi na lebo iliyomtoa, Mavin Records.
Kwa muktadha huo, ni wazi kuwa kwa wakati huu Ayra Starr ni bidhaa yenye mvuto zaidi katika soko la kimataifa kuliko Diamond ambaye mara yake kwanza kuvuma kimataifa ilikuwa mwaka 2013/14.
Ikumbukwe Ayra Starr alipata umaarufu zaidi barani Afrika kupitia wimbo wake, Rush (2022) ambao uliwania tuzo za Grammy. Video ya wimbo huu imeshatazamwa (views) YouTube mara milioni 613 ikiwa ndio video yake iliyofanya vizuri zaidi katika mtandao huo kwa muda wote.
Kwa upande wake Diamond, wimbo wake uliofanya vizuri zaidi YouTube kwa muda wote, ni Yope Remix (2019) akishirikiana na Innoss'B kutokea DR Congo. Huu video ina views milioni 284.
Na katika mtandao wa Spotify, Ayra Starr ana wastani wa kupata wasikilizaji (monthly listeners) milioni 19 kila mwezi, wakati Diamond ana milioni 1. Kwa hiyo Angelique Kidjo hakumchagua Ayra Starr kwa bahati mbaya, vitu vinajieleza. Mambo kwa ushahidi kabisa!.