Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DARASSA: Rapa anayetesa mitandaoni, redioni

DARASA Pict

Muktasari:

  • Kutoka kwenye makundi kama Kwanza Unit, Hard Blasters likiwa na wanachama mbalimbali akiwemo Profesa Jay, X Plastaz hadi kwa msanii mmoja mmoja kama Joh Makini, Stamina, Roma Mkatoliki, Darassa na wengineo tasnia imeendelea kuchukua nafasi kubwa katika jamii.

MUZIKI wa hip hop Tanzania umepitia hatua nyingi tangu kuanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Kutoka kwenye makundi kama Kwanza Unit, Hard Blasters likiwa na wanachama mbalimbali akiwemo Profesa Jay, X Plastaz hadi kwa msanii mmoja mmoja kama Joh Makini, Stamina, Roma Mkatoliki, Darassa na wengineo tasnia imeendelea kuchukua nafasi kubwa katika jamii.

Miongoni mwa majina yanayotikisa kizazi cha muziki wa hip hop ni Sharif Thabit Ramadhan maarufu kama Darassa aliyeanza muziki 2014 akiachia ngoma kama Sikati Tamaa.

Msanii huyo amejipatia heshima kubwa kupitia mashairi yake yenye uzito, ujumbe kwa jamii na mtindo wa kipekee unaobeba mchanganyiko wa rap na ladha ya R&B.

Tangu hapo ametoa ngoma mbalimbali kama Too Much, Hasara Roho, Proud of You na nyingine ambazo zimeendelea kumuweka kwenye ramani ya muziki.

Licha ya kufanya vizuri Bongo akichana mistari yenye kugusa jamii kutokana na ujumbe uliomo ndani, bado muziki wake haujapenya kimataifa zaidi ya Afrika Mashariki na Kati.

Kila ngoma anayotoa imekuwa pendwa mitaani na zikipigwa redioni, sehemu za starehe lakini pia zimekuwa zikifanya vizuri kwenye majukwaa mbalimbali ya kuuza muziki. Nyota huyo anashikilia rekodi ya kuwa rapa wa kwanza ambaye video ya wimbo wake wa Muziki uliotoka mwaka 2016 akimshirikisha mkali wa R&B, Ben Pol, kufanya vizuri zaidi YouTube ikiwa imetazamwa zaidi ya milioni 30.

Ben Pol ndiye msanii aliyechangia kwa kiasi kikubwa muziki wa Darassa kuanzia kolabo ya kwanza ya Sikati Tamaa iliyotoka mwaka 2012 ambayo ilimtoa na kumjulisha kimuziki. Miaka minne baadaye wakatengeneza ngoma nyingine Muziki. Wimbo huo ulifanya vizuri na kuuza zaidi kwenye majukwaa mbalimbali ya kidijitali.

Ikumbukwe pia albamu yake ya kwanza aliyoitoa mwaka 2020, Slave Becomes a King, ilisikilizwa zaidi ya milioni 20 kwenye mtandao wa Boomplay na hakuna albamu ya rapa iliyofikia rekodi hizo.

Kwa mwaka huo, ndiyo albamu iliyotoka na nyimbo nyingi zaidi ikiwa nazo 21, ikifuatiwa na Afro East ya Harmonize yenye nyimbo 18 na Story of the African Mob ya Navy Kenzo iliyokuwa na nyimbo 12. Pamoja na kuwa na kipaji kikubwa na kuaminika na mashabiki mbalimbali, ‘Mr Burudani’ huyo ambaye anafanya kazi chini ya lebo ya Classic Music Group (CMG), bado hajafanikiwa kutoboa kimataifa.

DARA 01

TUZO

Licha ya kufanya vizuri redioni na mitandaoni kwa zaidi ya miaka 10 kwenye tasnia hiyo, rapa huyo amenyakua tuzo moja tu tangu aanze maisha ya muziki. Tuzo ya kwanza kwa Darassa kushinda ilikuwa TMA kupitia wimbo wa Loyalty mwaka 2021.

Wimbo huo ulikuwa kwenye albamu yake ya kwanza, Slave Becomes a King ya mwaka 2020 akiwashirikisha Nandy na Marioo na ukashinda tuzo ya Wimbo Bora.

Loyalty ulizishinda ngoma kama Ndombolo ya Alikiba, Shikilia (Professor Jay), Unaua Vibe (Rapcha) na Lala ya Jux.

Tangu hapo, hakuna tuzo nyingine aliyoshinda rapa huyo anayetesa na kibao cha Looking for Love alichomshirikisha Mbosso.

DARA 02

SHOO

Mara ya mwisho Darassa kufanya shoo ilikuwa mwaka jana kwenye Wasafi Festival, tangu hapo amekuwa kimya muda mrefu kiasi cha mashabiki kuwa na hamu ya kusikia akichana mistari yake ‘live’.

Na hii si mara ya kwanza kwa msanii huyo kuwa kimya muda mrefu jukwaani, awali aliwahi kukaa karibu mwaka mzima bila kutoa ngoma.

Kwenye moja ya mahojiano aliwahi kusema, “niliamua kukaa kimya sababu nilikuwa na mambo ya kifamilia, nilimhamisha mama yangu kutoka kwake na kuja kwangu lakini pia nilikuwa kwenye kipindi cha kulea mtoto wangu Shantel.”

DARA 03

KOLABO KIMATAIFA

Mr. Burudani ameshafanya kolabo na wasanii mbalimbali akiwemo Nandy, Marioo, Zuchu, Alikiba, Harmonize na wasanii wengine hapa Bongo.

Kimataifa, Darassa amefanya kolabo na wasanii mbalimbali akiwemo Bien wa kundi la Sauti Sol, Nazizi, Jovial kutoka Kenya na Afrika Kusini alishirikiana na Sho Madjozi kwenye ngoma ya I Like It.

Bien ndiye msanii aliyemshirikisha mara nyingi, wakifanya hivyo mara mbili; kolabo ya kwanza walifanya mwaka 2023, ngoma inaitwa Nobody iliyofanya vizuri hasa kwenye mtandao wa YouTube. Audio pekee ilipata watazamaji zaidi ya milioni 10 huku video ikiwa na milioni 4. Wimbo mwingine ni Down for You uliokuwa kwenye albamu yake ya pili Take Away the Pain.

DARA 04

Hata hivyo, Darassa ndiye msanii wa kwanza wa Hip Hop kumleta Bongo Sho Madjozi na kufanya naye kolabo kipindi ambacho mwanadada huyo anawika na ngoma ya John Cena ambayo ilifanya vizuri si tu Tanzania bali hadi duniani. Kwenye kolabo hizo ambazo zilifanya vizuri hasa Tanzania na Afrika Mashariki na Kati, licha ya kuchanganya lugha ya Kiingereza na Kiswahili, hazikuenda mbali zaidi.

Ni ukweli kwamba Hip Hop ya Kiswahili bado haijawa bidhaa kubwa kimataifa. Wakati Afrobeat, Amapiano na Bongo Fleva zenye miondoko ya dansi zinavuma duniani, rap ya Kiswahili bado inapokelewa kwa wigo mdogo. Lugha ya Kiswahili, ingawa ni kubwa Afrika Mashariki, bado haina nguvu kubwa ya kibiashara kimataifa kama Kiingereza. Lakini kama Darassa atapata kolabo na wasanii wakubwa, inaweza kumfungulia njia kimataifa.