Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Cardi B amlipua mshauri wa Trump

Muktasari:

  • Sakata hilo lilianza baada ya mwandishi wa Politico, Jason Beeferman, kuchapisha ripoti ya kampuni ya utafiti wa taarifa potofu ya Cyabra, ikidai kuwa takribani asilimia 33 ya akaunti zilizokuwa zikichangia mijadala kwenye mitandao ya kijamii kuhusu machapisho ya kisiasa ya Nicki Minaj zilikuwa akaunti bandia.

RAPA maarufu wa Marekani, Cardi B, amemjibu mshauri wa zamani wa Rais wa Marekani, Donald Trump, Alex Bruesewitz baada ya kumhusisha kwenye mjadala unaoendelea mtandaoni kuhusu mabadiliko ya kisiasa na mpinzani wake wa muda mrefu, rapa Nicki Minaj.

Sakata hilo lilianza baada ya mwandishi wa Politico, Jason Beeferman, kuchapisha ripoti ya kampuni ya utafiti wa taarifa potofu ya Cyabra, ikidai kuwa takribani asilimia 33 ya akaunti zilizokuwa zikichangia mijadala kwenye mitandao ya kijamii kuhusu machapisho ya kisiasa ya Nicki Minaj zilikuwa akaunti bandia.

Ripoti hiyo ilihitimisha kuwa huenda kulikuwa na juhudi za makusudi za kufanya hivyo ili kuongeza wafuatiliaji kwa njia isiyo halali na ushawishi wa ujumbe wake wa kisiasa mtandaoni.

Hata hivyo mshauri huyo alipinga uhalali wa ripoti hiyo kupitia mtandao wa X, akidai kuwa mwandishi alishindwa kuweka wazi kwamba kampuni ya Cyabra ina uhusiano na wakala wa Cardi B.

Bruesewitz alidai kuwa sio vizuri kwa mwandishi kutoandika vitu vyote hususani suala la kutokutaja uhusiano huo, akihusisha jina la Cardi B moja kwa moja.

Cardi B hakukaa kimya, Kupitia ukurasa wake wa X akikanusha kuwa hahusiki na wala hana uhusiano wowote na jambo hilo linalodaiwa kuteka hisia za mashabiki wengi wa burudani.

“Umenihusisha na kunisumbua bila sababu. Hakuna mwanaume mzungu atakayekaa hapa kunidanganya au kunigeuza kama nina matatizo wakati ulipaswa kuniacha, kwa nini hutaki kujibu ukweli kwamba hiyo ni data halisi?

“Kwa nini hutaji wawekezaji wengine au wateja wengine wa kampuni hiyo ambao wanaweza kuwa upande wako? Hii siyo 2018 tena. Niko kwenye ziara iliyojaa mashabiki na sijali mambo yenu Marekani ina matatizo mengi,  biashara zinafungwa, wenye nyumba wanashusha bei, riba ziko juu halafu mshauri wa Trump anabishana na rapa mwanamke.”

Hata hivyo kupitia mahojiano na Billboard, Bruesewitz alisisitiza kuwa hakuwahi kusema Cardi alihusika moja kwa moja na ripoti hiyo, bali aliona ni muhimu kuweka wazi uhusiano wa wakala wake na Cyabra kutokana na historia ya mzozo wa wazi kati ya Cardi na Nicki.

Hivi karibuni, Nicki Minaj amekuwa akichapisha picha na video mbalimbali za kisiasa na kuonesha wazi kumuunga mkono Trump. Marapa hao wamekuwa wakifananishwa kutokana na ushindani wao wa muda mrefu na aina ya muziki wanaofanya.

Ushindani wa wawili hao ulianza mwaka 2019 kwenye usiku wa tuzo za Billboard Music Awards (BBMAs) ambapo wote wawili walikuwa wanawania tuzo hiyo, lakini alishinda Cardi B kupitia wimbo wake wa ‘Girls like You’ aliowashirikisha kundi la ‘Maroon 5’.

Wengine walidai kuwa Nick alistahili kushinda na baadhi waliona ushindi huo ni halali kwa Cardi B ambaye alikuwa anaanza kuchipukia kwa kasi kwenye tasnia ya Hiphop.

Tangu hapo hadi leo kumekuwa na mijadala mingi kuwahusu kinadada hao wawili wanaofanya vizuri kwenye muziki wa Hiphop ambao kwa muda mrefu umekuwa ukifanywa na wanaume.