Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Basata yamshushia rungu Dudu Baya, mratibu wa Bongo Flava 30

Muktasari:

  • Hatua hiyo inahusiana na matukio yaliyotokea Septemba 19, 2026 katika Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Flava lililofanyika katika Viwanja vya General Tyre, jijini Arusha.

Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limemtoza msanii Godfrey Tumaini ‘Dudubaya’ na Mratibu Mkuu wa Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Flava faini ya Sh3 milioni kila mmoja baada ya kubainika kukiuka masharti ya sheria zinazosimamia shughuli za sanaa nchini.

Hatua hiyo inahusiana na matukio yaliyotokea Septemba 19, 2026 katika Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Flava lililofanyika katika Viwanja vya General Tyre, jijini Arusha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Basata leo Ijumaa Septemba 25, 2026, Dudu Baya alikiuka masharti ya Kifungu cha 20(a) cha Kanuni za Baraza la Sanaa la Taifa, Tangazo la Serikali Na.137 la Mei 22, 2026.

Kutokana na ukiukwaji huo, Basata imempa msanii huyo tahadhari na kumtaka kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo ya Baraza hilo katika uendeshaji wa shughuli zake za sanaa.

Mbali na tahadhari hiyo, Basata imemtaka Dudu Baya kulipa faini ya Sh3 milioni ndani ya siku 14 kuanzia tarehe aliyopewa uamuzi huo pamoja na kumzuia kufanya shughuli za sanaa kwa namna yoyote hadi atakapotekeleza maagizo yaliyotolewa na Baraza hilo.

Kwa upande wa Mratibu Mkuu wa Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Flava, Basata imesema alikiuka masharti kwa kumtumia Dudu Baya kutumbuiza jukwaani bila kuhakikisha kuwa msanii huyo alikuwa ametimiza sifa zinazohitajika kisheria.

Basata imesema kitendo hicho kilikiuka masharti ya Kanuni ya 20(a), pamoja na wajibu wa waandaaji wa matamasha kuhakikisha wasanii wanaopanda jukwaani wanakidhi matakwa ya sheria.

Kutokana na kosa hilo, mratibu huyo naye ametakiwa kulipa faini ya Sh3 milioni ndani ya siku 14 na kujiepusha na shughuli za sanaa hadi atakapotekeleza maagizo hayo.

Basata imesema hatua hizo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wasanii, waandaaji wa matamasha na wadau wengine wa sanaa wanazingatia sheria, kanuni, miongozo na maadili yanayosimamia sekta hiyo nchini.