Kiki za wasanii zinavyowachefua mashabiki
Muktasari:
- Kiki za wasanii zimekuwa zikichukua sura mbalimbali, kuanzia mapenzi, ndoa, kuvishana pete, kuachana, ugomvi, kuugua hadi taarifa za vifo, huku lengo likiwa ni kuwavuta mashabiki wafuatilie jambo fulani ambalo baadaye hugeuka kuwa promo ya wimbo, filamu, tamthilia au shoo.
KIKI zimekuwa sehemu ya promosheni za wasanii, lakini pale mashabiki wanapoamini jambo ni la kweli na baadaye kugundua limepangwa kwa ajili ya kutangaza kazi, wengi hugeuka na kuwaponda wahusika.
Kiki za wasanii zimekuwa zikichukua sura mbalimbali, kuanzia mapenzi, ndoa, kuvishana pete, kuachana, ugomvi, kuugua hadi taarifa za vifo, huku lengo likiwa ni kuwavuta mashabiki wafuatilie jambo fulani ambalo baadaye hugeuka kuwa promo ya wimbo, filamu, tamthilia au shoo.
Baadhi ya wasanii wamekuwa wakipanga matukio hayo kwa siku kadhaa au wiki, wakijenga simulizi mitandaoni, huku mashabiki wakifuatilia kila kinachoendelea, wengine wakitoa pongezi, pole, ushauri na hata kuingia kwenye mabishano, kabla ya kufahamu kumbe ni sehemu ya kutangaza kazi.
Hata hivyo, mbinu hiyo imeanza kuonekana kuwachosha baadhi ya mashabiki, ambao baada ya kugundua wameamini tukio lisilo la kweli, hujikuta wakimwaga lawama, kejeli na maneno makali kwenye kurasa za wasanii husika.
DULLVANI
Wiki iliyopita, mchekeshaji Abdallah Sultan ‘Dullvani’, aliibua gumzo kwa tukio lililowafanya baadhi ya mashabiki kuamini alikuwa akifunga ndoa, lakini baadaye ikafahamika lilikuwa sehemu ya promo ya tamthilia yake mpya ya Ukweni.
Dullvani ambaye amejijengea jina kupitia uchekeshaji, alitumia simulizi iliyohusisha ndoa kuvuta hisia za watu kabla ya kufahamika nyuma yake kulikuwa na kazi mpya ya filamu.
ASMA NA SAID SAID
Wachekeshaji Asma na Said Said hivi karibuni walitumia simulizi ya kuoana kuibua gumzo, lakini kumbe walikuwa wakitangaza kuanzishwa kwa shoo yao ya komedi.
Kilichovutia zaidi ni namna mashabiki walivyoitikia baada ya kufahamu ukweli, huku baadhi wakionyesha kutofurahishwa na mbinu hiyo, wakihisi walikuwa wameingizwa mkenge.
HARMONIZE NA SARAH
Septemba 2019, Harmonize na aliyekuwa mchumba wake, Sarah Michelotti walizua gumzo baada ya picha kusambaa zikionyesha kana kwamba wamefunga ndoa.
Watu wengi waliamini wawili hao wamefunga ndoa ya siri, lakini baadaye meneja wa Harmonize, Beauty Mmari ‘Mjerumani’, alifafanua tukio hilo lilikuwa ni utengenezaji wa video ya wimbo Marry Me.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa wakati huo, Harmonize alikuwa akitengeneza video iliyohusisha mavazi na mazingira ya harusi, huku mashabiki wakitafsiri picha zilizokuwa zimesambaa ni ndoa halisi.
Mbinu hiyo iliwafanya wengi kufuatilia kilichokuwa kinaendelea, lakini baada ya ukweli kufichuka, mjadala ukahamia kwenye promo ya wimbo huo.
DIAMOND NA ZARI
Mwanamuziki Diamond Platnumz amewahi kutumia picha za harusi na mahusiano kuvuta hisia za mashabiki katika kutangaza kazi zake.
Wakati uhusiano wake na Zari Hassan ukiwa umevuta hisia za wengi, video ya wimbo Iyena iliyomshirikisha Zari kama bibi harusi na Diamond akiwa bwana harusi ilizua gumzo kubwa.
Video hiyo ilitoka baada ya wawili hao kutengana, hali iliyowafanya mashabiki kujiuliza kama ilikuwa ni ishara ya kurejeana au ni sehemu ya kazi ya muziki.
Diamond na Zari walikuwa tayari ni mastaa waliokuwa wakifuatiliwa kwa karibu, hivyo picha zao zikiwa katika mazingira ya harusi zilikuwa na uwezo wa kuvuta hisia za mashabiki na kuongeza mjadala kuhusu maisha yao.
DOGO JANJA, IRENE UWOYA
Mwaka 2017, Dogo Janja na Irene Uwoya waliwahi kuhusishwa na kufunga ndoa, huku taarifa zilizochapishwa wakati huo zikihusisha tukio hilo na promo ya filamu.
Tukio hilo lilizungumzwa kwa muda mrefu, huku baadhi ya watu wakiamini wawili hao walikuwa wameoana, kabla mjadala kuhusishwa na kazi ya filamu iliyokuwa ikitengenezwa.
MEJA KUNTA
Miongoni mwa kiki zilizowahi kukosolewa vikali ni ile ya msanii wa singeli Meja Kunta mwaka 2020.
Taarifa za ajali zilizosambaa zilieleza msanii huyo amepata ajali na baadaye taarifa za kifo chake zikaibuka, jambo lililowashtua mashabiki na watu mbalimbali.
Baadaye ilifahamika tukio hilo lilikuwa limeandaliwa kama kiki na msanii pamoja na uongozi wake waliomba radhi kwa Watanzania.
Meja Kunta mwenyewe baadaye alizungumzia namna alivyopokelewa na mashabiki baada ya tukio hilo na waliendelea kumuunga mkono na kumkubali tena.
DULLA MAKABILA
Mwaka 2020, msanii wa Singeli, Dulla Makabila alizua utata baada ya kuweka picha akiwa amejipodoa kama mwanamke, akivaa wigi na kufanya make-up.
Picha hizo ziliwafanya baadhi ya mashabiki kumshambulia na kumtolea maneno makali, lakini baadaye alifahamisha kuwa ilikuwa ni sehemu ya promo ya wimbo Ningekuwa Demu Ingekuwaje.
Hata baada ya kufafanua ilikuwa ni kazi ya muziki, baadhi ya mashabiki waliendelea kumponda, hali iliyoonyesha kiki inaweza kuleta mijadala.
Dogo Janja naye aliwahi kutumia muonekano wa aina hiyo katika wimbo Wayu Wayu, akijipodoa na kuvaa wigi, jambo lililozua mijadala na maneno kutoka kwa mashabiki.
KIKI ZA UGONJWA NA TAHARUKI
Kiki zinazohusisha afya nazo zimekuwa zikiibua mjadala katika tasnia ya burudani, hasa pale taarifa za ugonjwa zinapotumiwa kuvuta hisia za watu.
Mwaka 2020, msanii TID aliwahi kuonya dhidi ya kutumia janga la Corona kama njia ya kutafuta kiki, akisema ugonjwa huo ulikuwa tatizo kubwa linaloathiri watu wengi na haupaswi kutumiwa kwa ajili ya kujitangaza.
Hata hivyo, si kila taarifa ya ugonjwa wa msanii ni kiki. Baadhi ya mastaa wamekuwa wakipitia changamoto za afya za kweli na kuomba msaada, hivyo ni muhimu kutofautisha taarifa zilizothibitishwa na simulizi zinazotengenezwa kwa ajili ya promo.
MASHABIKI WAMECHOKA AU BADO WANAZIKUBALI?
Pamoja na kiki kuongeza umaarufu na kufanya kazi ya msanii izungumzwe, namna mashabiki wanavyoitikia baada ya ukweli kufichuka imekuwa sehemu ya mjadala.
Baadhi wanahisi wamechezewa akili, hasa wanapokuwa wamewekeza hisia zao kwenye tukio, wakitoa pole, pongezi au kuwatetea wasanii, halafu baadaye wanaambiwa ilikuwa ni promo.
Wengine wanaona kiki ni sehemu ya ubunifu wa kutangaza kazi, lakini wanasisitiza kuwa zinapaswa kuwa na mipaka, hasa pale zinapohusisha taarifa nyeti za vifo, magonjwa au migogoro ya kifamilia.