Aika afichua siri za Navy Kenzo
Muktasari:
- Ikumbukwe, Julai 2025 walitangaza kuachana na jina la Navy Kenzo na kutumia majina yao, Aika na Nahreel. Hata hivyo, historia ya kundi hilo bado ni sehemu muhimu ya safari yao ya kisanii.
Kwa miaka mingi, Aika na Nahreel walitengeneza jina kubwa katika muziki kutokana na kundi lao la Navy Kenzo, huku maisha yao ya uhusiano wa kimapenzi ukiendelea kuwavutia mashabiki. Siri ya kudumu kwao, namna wanavyokabiliana na changamoto na mtazamo wao kuhusu muziki ni baadhi ya mambo yaliyowafanya wawili hao kuendelea kuwa gumzo.
Ikumbukwe, Julai 2025 walitangaza kuachana na jina la Navy Kenzo na kutumia majina yao, Aika na Nahreel. Hata hivyo, historia ya kundi hilo bado ni sehemu muhimu ya safari yao ya kisanii.
Katika mahojiano ya Dakika 5 Na....Aika ameelezea namna wanavyolinda uhusiano wao na mchango wa muziki katika mafanikio yao.
Mwanaspoti: Siri ya kudumu kwa uhusiano wenu ni ipi?
Aika: (Kicheko) Hapa kwenye suala la mahusiano hili swali watu wengi hupenda kutuuliza sijui kwa nini, ‘anyway’ ni sisi kuwa wakweli kwa kila mmoja na kuzungumza tunapokutana na changamoto ni sehemu muhimu ya uhusiano wetu.
Mwanaspoti: Inapotokea kutokuelewana, mnafanyaje?
Aika: Huwa tunazungumza kuhusu mambo yanayotusumbua na kutafuta namna ya kuyatatua badala ya kuyaacha yaendelee kuwa tatizo na hatuyatoi nje mambo yetu.
Mwanaspoti: Kuna wakati uliwahi kumfumania Nahreel akiwa na mwanamke mwingine?
Aika: Hapana sijawahi kumfumania Nahreel na mwanamke hata siku moja.
Mwanaspoti: Mnalindaje maisha yenu binafsi yasivamiwe na umaarufu?
Aika: Sisi tunapendelea kuweka mambo yetu binafsi faragha, licha ya kuwa watu maarufu na kufuatiliwa na mashabiki.
Mwanaspoti: Ukiwa kwenye warsha ya Tamasha la 44 la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo 2026, umesisitiza wasanii kuwekeza nguvu katika kuboresha vipaji vyao kabla ya kutafuta umaarufu. Kwa nini?
Aika: Nimeeleza hivyo kuwa msanii anapaswa kwanza kujenga ubora wa kazi zake na kuhakikisha muziki anaoutoa unakuwa katika kiwango kizuri, sababu nimeona ubora wa kazi unapaswa kupewa kipaumbele kabla ya kujikita katika kujenga jina na umaarufu.
Mwanaspoti: Kwa hiyo, kati ya kujenga chapa ya msanii na kuboresha muziki, kipi kinapaswa kuanza?
Aika: Msanii aanze kwa kuimarisha kipaji na ubora wa kazi zake. Chapa na umaarufu vitakuja baada ya kuwa na kazi inayoweza kumtambulisha vizuri.