Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Haya ndo maisha ya G Nako nje ya muziki

DAKIKA Pict

Muktasari:

  • Ni mume, baba na ametamba na kazi mbalimbali za kwake binafsi na zile alizoimba na kundi huku pia akimshirikisha mwanamama Isha Mashauzi katika moja ya kazi zake ‘Mbele Yao’ inayofanya vizuri.

G Nako. Jina kubwa katika muziki wa Bongo Fleva. Ametamba katika Hip Hop akiwa ni mmoja wa waasisi wa kundi la Weusi, baada ya kutamba pia na kundi la Nako 2 Nako maskani yao ikiwa Arusha.

Ni mume, baba na ametamba na kazi mbalimbali za kwake binafsi na zile alizoimba na kundi huku pia akimshirikisha mwanamama Isha Mashauzi katika moja ya kazi zake ‘Mbele Yao’ inayofanya vizuri.

Dakika 5 Na... iliyoweka kambi katika Miaka 20 ya Isha Mashauzi, lilimtafuta G Nako ambaye amefunguka machache kuhusu maisha yake nje ya muziki, kirefu cha G katika jina lake la kisanii na kwa nini aliamua kumshirikisha Isha katika wimbo huo. Pia mezungumzia ndoa yake na mkewe pamoja na uhusiano wake na wasanii wenzake wa Weusi.

DAKI 01


Mwanaspoti: Ulitoa ngoma ya Mbele Yao ukamshirikisha mkongwe wa Taarab, Isha Mashauzi. Wazo la kukutanisha Bongo Flava na Taarab ya Pwani lilianzia wapi?

G Nako: Unajua muziki ni bahari isiyo na ukuta. Nilikuwa natafuta kitu kitakachovuka mipaka ya kawaida ya studio na kugusa hisia za vizazi vingi kwa wakati mmoja. Nilipokuwa naandaa wimbo huu, nilihitaji sauti yenye ladha halisi ya Kitanzania na utambulisho wa kipekee. Isha Mashauzi ana sauti yenye mamlaka na utambulisho thabiti. Tulipokaa na kusikilizana, nikaona hakuna mtu sahihi wa kufanya naye mradi huu zaidi yake.


DAKI 03

Mwanaspoti: Mashabiki wengi walishangaa kusikia sauti ya Isha Mashauzi kwenye mdundo wa Hip Hop. Mliwezaje kuunganisha mitindo hiyo bila kugongana?

G Nako: Ilikuwa zaidi ya kazi, ilikuwa darasa la ufundi wa sauti. Isha ana nidhamu kubwa kwenye uimbaji. Mimi nilileta nishati ya mtaani na mtindo wa uandishi wa kisasa, yeye akaja na ufundi wa Pwani na ladha ya Taarab. Kila mmoja alimpa nafasi mwenzake na matokeo yake ndiyo hayo mashabiki wanayasikia. Wimbo unatiririka vizuri bila mitindo yetu kugongana.


DAKI 06

Mwanaspoti: Mke wako Yasinta aliwahi kuonekana kwenye video ya Mama Yeyoo kabla hamjafunga ndoa. Je, ni rahisi kufanya kazi na mwenza wako kwenye sanaa bila kuchanganya mapenzi na kazi?

G Nako: Lilikuwa wazo zuri kwa wakati ule kwa sababu Mama Yeyoo ulikuwa wimbo wenye hisia halisi. Lakini mtazamo wangu wa sasa ni kwamba si lazima kila siku mke wangu awe kwenye meza ya habari au kwenye video zangu. Yeye ana maisha yake na mimi nina muziki wangu. Kwenye video ile ilitokea kwa sababu ya uzito wa wimbo wenyewe, lakini napendelea kulinda utulivu wa familia yangu mbali na kelele za mitandao na maisha ya ustaa.


Mwanaspoti: Tukiiacha studio na jukwaa, G Nako akiwa nyumbani na familia yake ni mtu wa aina gani?

G Nako: Mimi ni baba na mume wa kawaida kabisa. Nikitoka studio na kuvua viatu vya G Nako Warawara, nabaki kuwa George. Napenda kukaa na familia yangu, kupumzika na kuishi maisha ya kawaida bila ustaa. Nje ya muziki pia ninajihusisha na biashara na nina mapenzi makubwa na mazingira. Kabla muziki haujawa ajira yangu kamili, nilikuwa mtaalamu wa kuwaongoza watalii, yaani ‘tour guide’. Kwa hiyo bado ninapenda asili na maisha ya kawaida ya Kitanzania.


DAKI 02

Mwanaspoti: Unamshauri nini kijana anayetafuta mafanikio kwenye muziki au kazi nyingine yenye ushindani huku akitamani kujenga familia?

G Nako: Ushauri wangu ni kuchagua mwenza anayeelewa kazi yako na asiyeishi kwa ajili ya mwangaza wa watu wengine. Ukipata mtu anayekuvumilia wakati huna kitu, huyo ndiye wa kumthamini unapopata mafanikio. Kikubwa zaidi, tenga mipaka. Muziki ufanye mtaani na studio, lakini ukiingia mlangoni kwako acha ustaa nje.


Mwanaspoti: Umekuwa ukitoa ngoma zako binafsi na kushirikishwa kwenye kolabo mbalimbali. Je, hilo halileti ufa au mgongano wa kimasilahi ndani ya Weusi?

G Nako: Hapana kabisa, hakuna mgongano wowote. Sisi Weusi ni zaidi ya kundi la muziki; sisi ni familia na chapa kubwa. Mfumo wetu tangu mwanzo ulikuwa wazi. Kila msanii ndani ya Weusi ana uhuru wa kufanya miradi yake binafsi, na pia tuna muda wa kukaa pamoja kama kundi na kufanya kazi za Weusi. Kila mmoja kufanya kazi peke yake au kutoa ngoma yake binafsi haimaanishi kundi limevunjika. Badala yake, tunaongeza nguvu na kuendelea kuwapa mashabiki muziki mzuri.


DAKI 05

Mwanaspoti: Inapotokea umetoa wimbo wako binafsi ukawa mkubwa sana mtaani, wenzako wanachukuliaje? Hakuna wivu wa kisanaa?


G Nako: Hakuna wivu wowote. Badala yake, kunakuwa na furaha na sapoti kubwa. Kila mafanikio ya mwanachama mmoja wa Weusi ni mafanikio ya kundi zima. Joh Makini akitoa ngoma ikawa kubwa au Nikki wa Pili, au mimi mwenyewe, sote tunapongezana. Hiyo ndiyo nguzo inayotufanya tudumu kwa miaka mingi bila kugombana. Kila mmoja anafahamu mchango wa mwenzake na tunapeana nafasi ya kukua kisanaa.


DAKI 03

Mwanaspoti: Kwa hiyo, licha ya kila mmoja kuwa na safari yake binafsi, umoja wa Weusi bado ni muhimu?

G Nako: Ndiyo. Kila mmoja wetu ana nafasi ya kufanya mambo yake, lakini hilo haliondoi umoja wetu. Tunaheshimiana, tunaelewana na tunafurahia mafanikio ya kila mmoja. Kwetu sisi, kuona mwenzetu akifanya vizuri si sababu ya wivu, bali ni jambo la kujivunia kama familia ya muziki.