Afande Sele: Nikiwa mbunge nitakuwa bwege sishuki jukwaani
Muktasari:
- Katika mahojiano na Mwanaspoti, Afande Sele anakiri uamuzi wa kujiunga na siasa umetoka ndani ya moyo wake, hakuna aliyemshauri kufanya hivyo.
WIMBI la wanamuziki kuingia katika siasa linashika kasi nchini baada ya hivi karibuni Seleman Msindi ‘Afande Sele’ kutangaza kuingia katika ulingo wa siasa, lengo likiwa kuisaidia jamii.
Katika mahojiano na Mwanaspoti, Afande Sele anakiri uamuzi wa kujiunga na siasa umetoka ndani ya moyo wake, hakuna aliyemshauri kufanya hivyo.
Anasema mara nyingi ndege wanaoimba nyimbo zinazofanana huruka katika kundi moja wanapokuwa katiak safari zao.
“Mara nyingi nimekuwa naimba nyimbo za kupiga vita mambo yasiyofaa katika jamii, kuanzia ufisadi, unyonyaji kwa wanyonge na hata kupigia kelele huduma duni za jamii,” anasema.
Anasema jamii ya Watanzania inahitaji wawakilishi vijana katika nyanja mbalimbali ili waweze kupata uwakilishi utakaofanya kazi nzuri katika vikao vikubwa vyenye maamuzi.
Slaa, Zitto wamvuta Chadema
Oktoba mwaka jana Afande Sele alikabidhiwa kadi ya uanachama wa Chadema na kutangazwa kuwa mmoja wa vijana wapya wa chama hicho watakaopambana kuhakikisha demokrasia inatawala nchini.
Afande Sele anasema tangu zamani alikuwa anampenda mwanasiasa kijana Zitto Kabwe ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema na Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilbroad Slaa.
“Hakuna mtu aliyenishauri kujiunga na siasa hata Chadema si wao, tangu zamani nilikuwa navutiwa na wanasiasa wa chama hicho; Dk Slaa na Zitto.
“Hawa ndiyo wanasiasa pekee wasioogopa kusimama hadharani na kutetea wananchi, navutiwa nao ndiyo maana nikaona nijiunge nao kuunganisha nguvu zetu kisiasa,” anasema.
Anasema alisoma alama za nyakati na kugundua Chadema ndiyo chama pekee ambacho kingeweza kumpokea kutokana na maisha yake yalivyo na kazi zake pia. “Unajua mimi ni rasta, CCM wangeniona muhuni tu kama ningesema najiunga nao ndiyo maana nikaona Chadema ni waungwana na naweza kujiunga nao, halafu aina yangu ya muziki isingekuwa rahisi kujiunga na CCM.
“Mimi napiga vita ufisadi, unyonyaji wa jamii na huduma mbovu za jamii zinazotolewa na serikali, ingekuwa ngumu mimi kujiunga na chama ambacho kipo madarakani,” anasema.
Sugu kamtosa
Wengi walidhani Afande Sele amejiunga na Chadema kutokana na ushawishi wa mwanamuziki Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu ambaye alijiunga na chama hicho mwaka 2010 na kugombea ubunge katika Jimbo la Mbeya Mjini na kupata.
“Hapana Sugu hakushiriki katika harakati zangu za kujiunga na Chadema, wala sijawahi kungumza naye baada ya yeye kupata ubunge, nilimpigia kampeni za ubunge wake Mbeya lakini hakuna alichonifanyia hadi sasa.
“Mimi ndiye niliyemshauri ajiunge na Chadema na kugombea ubunge lakini hana msaada kwetu wote tuliomsaidia, amejisahau baada ya kupata ubunge na sihitaji anisaidie lolote,” anasema.
Anasema vijana wengi wakipata ubunge wanasahau walipotoka kwa kisingizio cha kuwa na shughuli nyingi wakati wanatumia muda mdogo kukaa bungeni na kufanya kazi za ubunge.
“Mimi nitaendelea kuimba huku nashiriki siasa, mbona kuna wabunge wanafanya biashara zao huku wanafanya kazi ya kuhudumia wananchi? Wapo wanaojifanya wanashughuli nyingi ili mradi kukwepa kukutana na watu wao.
“Ujue ubunge si ubonge, bali ubunge ni ubwege, maana yake ubunge si mahala pa kutafuta fedha ili unenepe na upate kitambi, ubunge ni kazi ya wito ya kutumikia wananchi, unatakiwa kuwa kama bwege kwa watu waliokuchagua, unatakiwa kufanya wanachokutuma,” anasema Afande Sele.
2015 atagombea ubunge au udiwani
Afande Sele bado hana uamuzi kati ya kugombea ubunge au udiwani, bado anatazama upungufu ulipo katika Jimbo la Morogoro Mjini ambalo mbunge wake ni Abdulaziz Abood.
Anasema anafanya uchunguzi mdogo ili kubaini mahala kwenye matatizo yanayofanya wananchi kuwa na maisha magumu huku wakikosa huduma mbalimbali za jamii.
“Huwezi kukurupuka na kuwania ubunge tu kwa sababu upo katika chama chenye nguvu, hapana mimi natazama kama tatizo katika jimbo letu lipo wapi kati ya halmashauri au ofisi ya jimbo. Kama kikwazo ni halmashauri nitagombea udiwani lakini kama ni mbunge hakika nitapambana na mbunge wetu wa sasa ili nipate nafasi ya kuwawakilisha wananchi wa Morogoro Mjini,” anasema Afande Sele.
Afande Sele anasema Mbunge wa Morogoro Mjini, mara nyingi haitumikii jamii ya watu wa jimbo lake, amegeuka mfadhili kuliko kutatua matatizo.
“Watu wakipata matatizo kama misiba wanaenda kwake anawapa basi moja kwa ajili ya shughuli za mazishi hapo wananchi wanaona amewasaidia sana, kumbe hakuna lolote la maana.
“Kama ofisi yake ingefanya kazi vizuri na watu wa halmashauri kwa nini wasinunue basi ambalo linaweza kutumiwa na mtu yeyote? Vijana wengine wanaenda kwake kuomba fedha tu na wanapewa wakati mwingine Sh. 10,000 na wanaona vizuri tu, hawapewi jambo lolote la kujikwamua kiuchumi,” anasema Afande Sele.
“Kama mbunge anaweza kutoa basi katika maziko, anashindwa vipi kuhakikisha dawa za malaria zinakuwepo hospitali? Maana inawezekana marehemu alifariki baada ya kukosa dawa za malaria, wananchi wanapaswa kuelewa kuhusu hali hii.”
Mambo matano atakayoyasimamia
Amepanga kufanya mambo matano makubwa pindi atakapopata iwe udiwani au ubunge, mambo hayo ni;
1.Katika mshahara wa Sh. Milioni 10 atakaopewa kama mbunge, binafsi atachukua Sh. 1 milioni tu katika matumizi yake na zitakazobaki ataziingiza katika mfuko wa jimbo kwa matumizi mengine ya jimboni.
2.Kuhakikisha anafufua vyanzo vya maji ili Morogoro iwe na uhakika wa maji muda wote kama zamani, pia atashirikiana na mamlaka husika kupata umeme wa uhakika na huduma nyingine za mawasiliano.
3.Kuhakikisha vijana waendesha bodaboda wanathaminiwa katika huduma za jamii kwani ni watu hatari endapo wataendelea kudharauliwa na watoa huduma za jamii kama hospitalini na polisi. Pia atahakikisha vikundi vya vijana vinapatiwa mikopo na kuendeleza sekta isiyo rasmi.
4.Kuboresha afya ya uzazi kwa akina mama ambao mara nyingi wanapata tabu wakati wa kujifungua.
5.Kuboresha ushirikiano kati ya watu na Jeshi la Polisi ,
“Nadhani kwa kushirikiana na wasaidizi wakati huo, mambo yote haya yatafanyika kwa ukamilifu na kuirudisha Morogoro katika maisha mazuri ambayo sasa ni ndoto na historia kwa kizazi cha sasa,” anasema Afande Sele.
Albamu ya Kingdom ya Amani
Hadi sasa Afande Sele ana albamu nne lakini ya tano ipo jikoni na muda wowote itatoka. Albamu zake za zamani ni Mkuki Moyoni (2001), Darubini (2003), Nafsi ya Mtu (2005) na Karata Dume aliyotoa mwaka 2008.
Albamu mpya anayotarajia kuizindua Juni mwaka huu inaitwa Kingdom ya Amani na Upendo, ina nyimbo zaidi ya nne, zikiwamo; Kingdom, Simba Dume, Amani na Upendo, Soma Ule, Binadamu na Sukari na Chai.
Afande Sele ni baba wa watoto wawili, Tunda Jema (13) na Asante Sana mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu. “Tunda anasoma ingawa mama yao nimeachana naye baada ya kutokea matatizo fulani ya kifamilia,” anasema.
Jina: Seleman Msindi
Kuzaliwa: 24.05. 1976
Mahali: Morogoro, Tanzania
Kazi: Muziki/ Siasa