Mama Dangote, Zuchu gumzo wakicheza taarabu za mafumbo
Muktasari:
- Mwanaspoti lilikuwepo kushuhudia sherehe hiyo iliyofanyika nyumbani kwa Mama Dangote, Madale jijini Dar es Salaam, ambapo Zuchu alikuwa akifurahia usiku wake akiwa amezungukwa na ndugu, marafiki na watu mbalimbali waliokuja kusherehekea naye.
KATIKA tukio la Henna Night lililoandaliwa maalum kwa ajili ya Zuchu, kulinoga baada ya Mama Dangote, Sanura Abdul, kuonekana akiwa karibu na Zuchu, huku nyimbo za taarabu zenye mafumbo zikitawala burudani na kuwafanya wageni kuingia kwenye dansi.
Mwanaspoti lilikuwepo kushuhudia sherehe hiyo iliyofanyika nyumbani kwa Mama Dangote, Madale jijini Dar es Salaam, ambapo Zuchu alikuwa akifurahia usiku wake akiwa amezungukwa na ndugu, marafiki na watu mbalimbali waliokuja kusherehekea naye.
Zuchu amefanyiwa sherehe hiyo ambayo ni ya kifamilia na kitamaduni kuelekea tukio la 40 ya mtoto wake aliyejifungua Agosti 2, 2026. Sherehe ya 40 ya mtoto aliyezaa na Diamond, inatarajiwa kufanyika kesho Jumamosi, Septemba 12, 2026.
Muziki ulipoanza kushika kasi, Mama Dangote na Zuchu walionekana kucheza pamoja huku nyimbo za taarabu zikiendelea kupigwa. Wakati mwingine walikumbatiana na kuendelea kufurahia muziki, jambo lililovuta macho ya waliokuwa kwenye hafla hiyo.
Tukio lingine lililovuta macho ya Mwanaspoti ni pale Zuchu alipokwenda alipokuwa amekaa Mama Dangote na kuanza kumtunza hela, huku wimbo wa Sabaha Salum Muchacho uitwao ‘Donge la Nini’, ukiendelea kupigwa. Zuchu alionekana kufurahia muda huo, huku Mama Dangote akiwa sehemu ya burudani hiyo iliyokuwa ikiendelea mbele ya wageni.
Kilichoongeza ladha kwenye tukio hilo ni kwamba baadhi ya nyimbo zilizokuwa zikipigwa zilikuwa na mafumbo ya mapenzi. Badala ya kukaa pembeni, Mama Dangote na Zuchu waliendelea kucheza na kufuatisha muziki huo, huku sherehe ikiendelea kwa shamrashamra.
Picha hiyo ilikuja wakati ambapo kumekuwa na mazungumzo kutoka kwa baadhi ya watu kuhusu uhusiano wa Mama Dangote na Zuchu, wengine wakidai kuwa wawili hao hawaelewani. Lakini katika usiku huo, Mwanaspoti lilishuhudia hali tofauti, huku Mama Dangote na Zuchu wakionekana kuwa karibu, wakicheza na kufurahia pamoja wakiacha gumzo kwa waliokuwa wakiwatazama.
Zuchu ambaye alikuwa mwenye furaha muda wote wa sherehe, alionekana kufurahia uwepo wa Mama Dangote, huku wote wakiendelea kushirikiana na wageni na kuingia kwenye burudani. Kwa kifupi, kama taarabu zile zilikuwa na mafumbo yake, basi usiku huo Mama Dangote na Zuchu walijibu kwa dansi, tabasamu na ukaribu wao.