Mahaba ya Diamond, Zuchu katika Henna Night
Muktasari:
- Mwanaspoti lilikuwepo katika tukio hilo wakati wageni walipoanza kuelekea eneo lililoandaliwa kwa ajili ya chakula. Diamond, badala ya kumuacha Zuchu aende mwenyewe, alimbeba na kwenda naye hadi sehemu hiyo.
MAPENZI ya Diamond Platnumz na Zuchu yaliendelea kuteka macho ya wengi kwenye Henna Night ya Zuchu, baada ya Diamond kumbeba mke wake huyo hadi eneo la chakula, huku wakiongeza dozi ya mahaba mbele ya wageni.
Mwanaspoti lilikuwepo katika tukio hilo wakati wageni walipoanza kuelekea eneo lililoandaliwa kwa ajili ya chakula. Diamond, badala ya kumuacha Zuchu aende mwenyewe, alimbeba na kwenda naye hadi sehemu hiyo.
Baada ya kufika, wawili hao walichukua chakula na kuendelea kuwa pamoja, huku Diamond na Zuchu wakionekana kufurahia muda wao bila kujali macho ya waliokuwa karibu nao.
Lakini kilichovuta zaidi ni pale wawili hao walipoonekana kula kwenye sahani moja, huku Zuchu akimlisha Diamond wakati wakiendelea na mlo wao.
Zuchu alionekana kufurahia kumlisha Diamond, huku mwanamuziki huyo naye akipokea huduma hiyo kwa bashasha. Tukio hilo liliongeza picha ya ukaribu wa kimapenzi iliyokuwa ikionekana kati yao usiku huo.
Hilo lilikuwa miongoni mwa matukio yaliyofanya Henna Night hiyo kuwa na ladha ya kipekee, kwani muda mwingi Diamond na Zuchu walionekana pamoja, wakicheza, kukumbatiana na kufurahia muziki uliokuwa ukipigwa.
Hayo yote yalijiri katika Henna Night, sherehe ambayo Zuchu amefanyiwa ikiwa ni ya kifamilia na kitamaduni kuelekea tukio la 40 ya mtoto wake aliyejifungua Agosti 2, 2026.
Hafla hiyo imefanyika nyumbani kwa Mama Dangote, Sanura Abdul, eneo la Madale jijini Dar es Salaam, huku 40 ya mtoto wa Zuchu na Diamond ikitarajiwa kufanyika kesho Jumamosi, Septemba 12, 2026.