‘Selemani’ ya Mbosso yawakumbusha Yanga
Muktasari:
- Mbosso alipokuwa akitumbuiza mbele ya mashabiki wa tamasha hilo, aliimba wimbo wake ‘Selemani’. Hata hivyo, kabla hajaendelea sana na wimbo huo, mashabiki walilipuka kwa shangwe huku baadhi yao wakilitaja jina la Yanga.
Jina la mshambuliaji Selemani Mwalimu limeendelea kutawala mitandao ya kijamii tangu alipohama Simba na kujiunga na Yanga, lakini safari hii limeibuka katika upande wa burudani baada ya mwanamuziki Mbosso kulitaja jukwaani wakati wa Tamasha la Imbeju Sauti Moja.
Mbosso alipokuwa akitumbuiza mbele ya mashabiki wa tamasha hilo, aliimba wimbo wake ‘Selemani’. Hata hivyo, kabla hajaendelea sana na wimbo huo, mashabiki walilipuka kwa shangwe huku baadhi yao wakilitaja jina la Yanga.
Mwitikio huo ulimfanya Mbosso naye kuingia kwenye mzuka wa jukwaani na kusema: “Ila Sele, daah!”
Kauli hiyo ilizidisha shangwe, huku mashabiki wakiendelea kuimba na kupaza sauti. Tukio hilo likawa miongoni mwa matukio yaliyoacha gumzo kwenye tamasha hilo.
Si vigumu kuelewa sababu ya mwitikio huo. Kwa sasa, jina la Selemani Mwalimu ni miongoni mwa yanayotajwa zaidi katika mitandao ya kijamii kutokana na namna alivyohama Simba na kutua Yanga ndani ya muda mfupi.
Mwalimu alikuwa ametangazwa na Simba kuwa sehemu ya kikosi cha msimu wa 2026/27 na tayari alikuwa ameshiriki maandalizi ya timu hiyo. Hata hivyo, mambo yalibadilika ghafla baada ya Yanga kufanikiwa kumnasa mshambuliaji huyo kwa mkopo kutoka Wydad Casablanca ya Morocco.
Usajili huo uliwashangaza mashabiki wengi wa Simba ambao tayari walikuwa wameamini kuwa Mwalimu angeendelea kuvaa jezi nyekundu msimu mwingine.
Kilichoongeza uzito wa sakata hilo ni kwamba mchezaji huyo alikuwa ametangazwa na Simba baada ya klabu hiyo kueleza kuwa imeongeza muda wa mkopo wake kutoka Wydad Casablanca.
Hata hivyo, muda mfupi baadaye Yanga ikaingia kwenye hesabu na hatimaye kumtambulisha Mwalimu kama mchezaji wake mpya.
Mabadiliko hayo ndiyo yaliyofanya jina la Selemani kuwa gumzo, na Mbosso alipolileta jukwaani kupitia wimbo wake, mashabiki wakapata fursa ya kulihusisha moja kwa moja na sakata hilo la soka.
MBOSSO AENDELEA KUTIKISA
Baada ya ‘Selemani’, Mbosso hakusimama hapo. Msanii huyo aliendelea kuwaburudisha mashabiki kwa nyimbo zake zilizowahi kufanya vizuri, zikiwemo ‘Pawa’, ‘Nadekezwa’, ‘Amepotea Hodari’ na ‘Robo Saa’, ambazo ziliendelea kuinua shangwe ndani ya ukumbi.
Pia aliingiza kwenye burudani yake wimbo mpya wa DJ, uliowafanya mashabiki kuendelea kucheza na kuimba pamoja naye.
Mbosso, ambaye amejijengea jina kupitia nyimbo zenye mchanganyiko wa mapenzi, hisia na ladha ya kipekee ya Bongo Fleva, alionyesha tena uwezo wake wa kuunganisha muziki wake na matukio yanayozungumziwa na mashabiki kwa wakati huo.
‘MIMI NI NANI’ NAYO YAPATA NAFASI
Mbali na nyimbo zake za Bongo Fleva, Mbosso pia amegusa muziki wa Injili kupitia wimbo ‘Mimi Ni Nani’, alioutoa akiwa ameshirikishwa na kundi maarufu la muziki wa Injili kutoka Burundi, Rachats Classic.
Wimbo huo unapatikana kama Rachats Classic ft Mbosso – ‘Mimi Ni Nani’, na ushirikiano huo umemwonyesha Mbosso katika upande mwingine wa muziki wake.
Hivyo, katika usiku wa Imbeju Sauti Moja, Mbosso alitoa burudani yenye ladha mbalimbali. Hata hivyo, miongoni mwa nyimbo zilizozua hisia za kipekee ni ‘Selemani’, hasa kutokana na jina hilo kuwa tayari limetawala mjadala wa soka nchini.
Kwa mashabiki waliokuwa ukumbini, ilikuwa burudani ya muziki; lakini kwa upande mwingine, ilikuwa kama kumbukumbu ya sakata jipya la usajili lililomtoa Selemani Mwalimu Msimbazi na kumpeleka Jangwani.
Na kwa sasa, kila jina la “Selemani” linapotajwa, ni vigumu kwa mashabiki wa soka kutokumbuka stori hiyo.