Faini ya Basata ilivyogeuka neema kwa Dudubaya
Muktasari:
- Siku chache zilizopita, BASATA ilitoa adhabu dhidi ya msanii huyo pamoja na Mratibu Mkuu wa Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Flava kutokana na matukio yaliyojitokeza Septemba 19, 2026 katika Viwanja vya General Tyre, jijini Arusha.
HATUA ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kumfungia msanii mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva, Godfrey Tumaini ‘Dudubaya’ (Oil Chafu), pamoja na kumtoza faini ya Sh3 milioni, imegeuka neema na fursa ya kipekee kwake baada ya wadau mbalimbali wa michezo na burudani kujitokeza na kumlipa fedha za adhabu hiyo.
Siku chache zilizopita, BASATA ilitoa adhabu dhidi ya msanii huyo pamoja na Mratibu Mkuu wa Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Flava kutokana na matukio yaliyojitokeza Septemba 19, 2026 katika Viwanja vya General Tyre, jijini Arusha.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya BASATA iliyotolewa Ijumaa ya Septemba 25, 2026, Dudubaya alikiuka masharti ya Kifungu cha 20(a) cha Kanuni za Baraza la Sanaa la Taifa (Tangazo la Serikali Na.137 la Mei 22, 2026). Kutokana na kosa hilo, Baraza lilimpa tahadhari msanii huyo, likamtaka kulipa faini ya Sh3 milioni ndani ya siku 14, na kumzuia kujihusisha na shughuli yoyote ya sanaa nchini hadi atakapotekeleza maagizo hayo.
Wakati huo huo, mratibu mkuu wa tamasha hilo naye alikumbana na adhabu ya faini ya Sh3 milioni pamoja na kuzuiliwa kufanya shughuli za sanaa kwa kosa la kumruhusu Dudubaya kutumbuiza jukwaani bila kuhakikisha kama ametimiza vigezo na sifa zinazohitajika kisheria.
KITANZI NA NEEMA
Hata hivyo, tofauti na matarajio ya wengi kuwa adhabu hiyo ingemweka msanii huyo kwenye wakati mgumu, mambo yamekuwa tofauti kabisa. Ni kama vile adhabu hiyo imefungua milango ya neema na mapenzi mapya kutoka kwa jamii na wadau wa michezo na muziki nchini.
Tangu kutangazwa kwa adhabu hiyo, wimbi kubwa la wadau wa soka na sanaa limejitokeza kumchangia mwanamuziki huyo ili kufikisha kiasi hicho cha fedha kabla ya muda wa siku 14 uliowekwa na BASATA haujamalizika.
Miongoni mwa walioonyesha upendo wao kwake ni Afisa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga, Ali Kamwe. Kamwe, ambaye anafahamika kwa ushawishi wake mkubwa kwenye mitandao ya kijamii na sekta ya michezo, amekuwa kinara wa kuhamasisha na kuchangia kiasi cha fedha ili kumwezesha Dudubaya kurejea jukwaani haraka iwezekanavyo.
Sio Kamwe pekee, bali pia uongozi wa waandaaji wa Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva wenyewe umeamua kuonyesha uungwana na mshikamano wa dhati na kumlipia staa huyo adhabu hiyo.
Pamoja na wao wenyewe kukabiliwa na faini ya Sh3 milioni kutoka kwa lebo hiyo ya mlezi wa sanaa nchini, waandaaji hao wamejitolea kumsaidia Dudubaya kwa kumchangia sehemu ya faini yake ili asiteseke peke yake.
WABUNGE NAO WAIBUKA
Mbali na wasanii kupaza sauti na wengine kutoa mchango wao, baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania nao wameshiriki kwenye michango hiyo huku wengine wakijitokeza hadharani kuonyesha kuwa wanamuunga mkono msaniii huyo ambaye kauli zake zimeshamfanya awe maarufu kwa kipindi kifupi pamoja na kwamba aliwahi kuwika huko nyuma.
Hali hii inaonyesha kuwa msanii huyo baada ya kushuka amepanda kwa kasi kubwa lakini pia adhabu yake imeonyesha kuwa alikuwa anafuatiliwa na watu wengi zaidi tofauti na hali ilivyokuwa kabla ya kupata adhabu hiyo.
MASHABIKI WAFURIKA NA MICHANGO
Mbali na watu hao maarufu, baadhi ya mashabiki wa Dudubaya na wapenzi wa muziki wa Bongo Fleva nao wamekuwa wakichangishana kuhakikisha kuwa msanii huyo sasa anapata chochote kitu.
Kupitia kampeni za hiari zinazoendelea kwenye mitandao ya kijamii, mashabiki wamekuwa wakituma fedha kidogo kidogo kupitia namba za simu zilizoainishwa, jambo linaloonekana wazi faini hiyo itamfanya msanii huyo abaki na kiasi cha fedha kwa ajili ya kuendesha maisha yake kwa kuwa tayari faini imeshalipwa.
Wadau wengi wanaona kuwa Dudubaya anapewa ushirikiano huu sio tu kwa sababu ya huruma, bali kutokana na mchango wake wa kihistoria katika ujenzi wa msingi wa muziki wa Bongo Fleva ambao leo hii unaajiri maelfu ya vijana nchini, lakini kauli yake ambayo amekuwa akiitumia mara kwa mara inaonekana kuwavutia wengi.
Ingawa neema hii imemwangukia Dudubaya, BASATA imesisitiza msimamo wake wa kusimamia sheria, kanuni na maadili ya sanaa nchini uko palepale. Baraza hilo limebainisha hatua zilizochukuliwa zinalenga kutoa fundisho kwa wasanii wote na waandaaji wa matamasha ili kuzuia matukio ya ukiukwaji wa sheria katika siku zijazo.
BASATA imewakumbusha waandaaji wote nchini kuhakikisha wanawatumia wasanii waliokidhi vigezo vya kisheria na waliosajiliwa rasmi na Baraza hilo kabla ya kuwapandisha kwenye majukwaa ya umma.
Hata hivyo, kwa upande wa Dudubaya, matokeo ya adhabu hii yamezua taswira mpya.
Licha ya watu kumchangia, lakini Dudubaya alizungumza kuwa pesa hizo za michango atazipeleka kwa watu wenye uhitaji na hivi karibuni alitoa kiasi cha Sh1 milioni kwa Zahir Zoro, baba mzazi wa mwanamuziki Banana Zoro ambaye anasumbuliwa na maradhi.