Mamitto: Haikuwa kazi rahisi kutoboa maisha

EUNICE Wanjiru ni mchekeshaji maarufu wa Stand Up Comedy aliyeibukia kupitia shoo ya Churchill Show.

Mamilioni ya mashabiki wake wanamfahamu vyema kama Mamitto. Akiwa na umri wa miaka 27, tu Mamitto ni kati ya wachekeshaji wachache nchini Kenya wanapata dili za mamilioni ya pesa kupitia vipaji vyao.

Kabla hajawa maarufu, Mamitto alikuwa ni binti wa kwaida katika mtaa wa kawaida tu wa Kibera, Nairobi.

Mwanaspoti lilipata nafasi ya kufanya mahojiano na mchekeshaji huyo na alizungumza mambo mbalimbali juu ya sanaa yake kama ifuatavyo;


Mwanaspoti: Maisha yalikubadilikiaje baada ya kuzuka kwa janga la Covid-19?

Mamitto: Nilikuwa nimezoea maisha ya kupiga shoo kwenye steji ya Churchill Show lakini tangu Corona iliyosababisha kumbi nyingi kufungwa, niligeukia mitandao. Mtandaoni kwa sasa ndio steji yangu, ndiyo maana kila muda utanikuta nikishuti kitu kwa ajili ya kuposti mtandaoni.


Mwanaspoti: Wewe ndiye mchekeshaji wa kike mwenye followers wengi barani Afrika ukiwa na zaidi ya wafuasi milioni moja. Hili unalizungumziaje?

Mammito: Kwanza, ni jambo kubwa sana kwangu. Inakuonyesha ni jinsi gani sanaa yangu inavyokubaliwa na wengi na ndiyo sababu kila siku utanikuta nashuti kitu kwa ajili ya kuwaridhisha mashabiki wangu.


Mwanaspoti: Hebu turudi nyuma kidogo, ulizaliwa wapi?

Mamitto: Nilizaliwa Ghetto kule Kibera. Mama yangu alinipata akiwa bado mdogo wa miaka 15 tu na maisha hayakuwa mepesi.


Mwanaspoti: Yalikuaje?

Mamitto: Hili ni swali ambalo nimeulizwa zaidi ya mara mia na wakati wote huwa sina jibu sahihi.

Kibera ni ghetto, maisha ni ya umaskini kila kona. Tuliishi kwenye chumba kidogo sana, kupata chakula ilikuwa tatizo na mara nyingi tulikula mahindi yaliyochemshwa na kushinda kutwa bila ya msosi mwingine.

Choo Kibera haikuwa rahisi, tulilipia Sh10 (ya Kenya), kwa ajili ya kuweza kuzitumia sababu kwenye ghetto choo huchangiwa, hata bafu tulilipia kuogea.


Mwanaspoti: Mama yako alijishughulisha na nini kupata riziki?

Mamitto: Alikuwa ni fundi wa nguo. Mara nyingi nilishuhudia akikesha hadi usiku wa manane akishona nguo kwa kutumia mwanga wa mshumaa. Jitihada zake hizo za kusaka riziki ndizo hunipa motisha ya kuhangaika kila siku. Mimi huwa sina siku ya kupumzika, napiga shughuli kila kukicha.


Mwanaspoti: Utotoni ulikuwa mtoto wa aina gani?

Mammito: Nilikuwa mkorofi sana. Nilikuwa sijui kutulia lazima ningefanya jambo. Mara nyingi mama alikuwa akitoka kazini na kunikuta nikiwa juu ya paa la nyumba au wakati mwingine nimeharibu kitu ndani ya nyumba. Nilizoea kupigwa na mama kwa sababu ya utukutu.


Mwanaspoti: Utukutu wako uliishia kwenye komedi, nini mtazamo wa mama?

Mamitto: Huwa ananitania kama angelijua ukorofi wote ule ungeishia kwenye kuwa mchekeshaji, basi angeniadhibu sana kama alivyofanya .


Mwanaspoti: Sanaa yako ilianzia wapi?

Mamito: Baada ya kumaliza masomo yangu ya kidato, bibi yangu alinisajili kwenye Chuo Kikuu cha Mt Kenya University kusomea Diploma ya Community Developmenmt and Social Work, nikiwa chuo, nikajiunga na kundi la drama. Nilipenda uigizaji ila nilivutiwa zaidi na kila mara nilipotoa utani na watu wakawa wanacheka sana, hapo ndipo nikaamua kujikita zaidi kwenye uchekeshaji sababu huwa nafarijika sana kuwachekesha watu.

Nilifanya uamuzi wa kujitosa kwenye komedi mwaka 2015 nikiwa mwaka wangu wa mwisho chuoni, familia yangu haikufurahia kabisa taarifa hizi sababu komedi haikuwa ikilipa nyakati hizo.


Mwanaspoti: Ulipataje fursa Churchill Show?

Mamitto: Haikuwa rahisi na ningependa watu waelewe ufanisi wangu sio wa siku moja mbili, ni jitihada ya miaka mingi iliyoishia kulipa sasa.

Churchill Show nilitambulishwa kule mwaka 2016 ila nilikuja kupewa fursa baada ya miezi 18. Katika kipindi hicho, nilikuwa nashiriki usahili kila Jumanne narudishwa nyumbani eti bado sijaiva. Sikuwahi kufa moyo niliendelea. Hatimaye nilipata fursa ya kupewa shoo ila hadhira ikawa haicheki.

Nikashushwa tena na kurudishwa kwenye zile harakati za usahili kwa miezi sita zaidi, nilipopewa fursa stejini safari hii, niliiacha hadhira hoi, ikawa ndio mwanzo wangu.


Mwanaspoti: Ni jambo lipi ulilojifunza na sanaa hii?

Mamitto: Sanaa ya uchekeshaji ni ya ajabu sana, ipo tofauti na sanaa nyingine kabisa, hii sio sanaa utakayotegemea eti kuwa mwanamke utasaidika, hapana. Kama huwezi kuwachekesha watu, basi tafuta kitu kingine cha kufanya, siri hapa ni kujitahidi sana kuboresha sanaa yako na kipaji kama unajua unacho.


Mwanaspoti: Ni kina nani waliokupa sapoti kubwa kwenye safari hii?

Mamitto: Nimejifunza mengi sana kutoka kwa mpenzi wangu mchekeshaji vile vile, Eddie Butita ambaye ni mbunifu kinoma, kuna YY, Sleepy David hawa wote tumejengana na kukuzana kisanii, kisha kuna Daniel Ndambuki ambaye ndiye kama baba ninayeweza kusema alinishika mkono na kunisaidia kuikuza sanaa yangu.


Mwanaspoti: Hofu yako kubwa ni nini?

Mamitto: Kupotea kwenye gemu na ndio sababu kila kukicha utanikuta nipo kwenye harakati hizi za kuandaa viklipu vya vichekesho au kutafuta mawazo mapya, huwa nafuatilia sana kinachoendelea na ndio maana hakuna kitakachotrendi bila mimi kujihusisha nacho.


Mwanaspoti: Ni kipi kinachokufariji na kukuridhisha kutokana na mafanikio yako?

Mamito: Kila nikiwaza kwa sasa ninaishi kwenye nyumba yenye choo, naiona ikiwa jambo kubwa sana.

Siwezi kuyatamani yale mtaisha niliyoishi utotoni, na kama hujawahi kupata matatizo kwa sababu ya kuwa na sehemu ya kujisaidia, basi hujaona shida bado.