Ferooz hana fedha, ila uzoefu

UNAFAHAMU kwamba staa wa wimbo bora zaidi wa Ukimwi wa Starehe, Feruzi Mrisho ‘Ferooz’ ana kundi la muziki lenye wasanii zaidi ya watano? Habari ndiyo hiyo.

Kundi analoliongoza Ferooz linaitwa Wabeshi na limejaa mchanganyiko wa wasanii wa kuimba na kurap likiwa na maskani Kinondoni, Dar es Salaam.

Sasa ishu ni kwamba Ferooz mwenyewe nafasi yake kwenye muziki imeshuka kwa kiasi kikubwa na inadaiwa hata kwenye suala la kifedha mshikaji hayupo vizuri.

Mwandishi wa Mwanaspoti alifanya naye mahojiano na kumuuliza anawezaje kusaidia wengine ikiwa mwenyewe hali yake sio nzuri? Kwanza Ferooz amekiri kweli hali yake kiuchumi si nzuri kama zamani, lakini pia amesema wasanii wake wanahitaji uzoefu wake zaidi ya pesa.

“Nimefanya muziki kwa muda mrefu kwa mafanikio. Nina uzoefu mkubwa ambao kwao unaweza kuwa darasa. Nadhani hilo ni muhimu kuliko hata pesa ninazoweza kuwapa,” alisema.

Ferooz alitamba miaka ya 2000 na wimbo wa Starehe ambao ulikuwa mkali mpaka akazawadiwa gari na Rais wa Tanzania kipidni hicho, Benjamin Mkapa.