Simba watua Zanzibar kifua mbele

Mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya

Muktasari:

Timu hiyo ambayo haikutaka kuweka wazi jina la hoteli,  imesafiri na wachezaji 24 pamoja  na viongozi 6,  ambao kama watafanya vizuri wataendelea kukaa kisiwani humo mpaka mashindano yatakapofikia kikomo Januari 13,  siku itakapochezwa mechi ya fainali.

KIKOSI cha Simba, kimewasili salama Kisiwani Zanzibar leo Jumatatu mchana na moja kwa moja wamekwenda katika hoteli ya nyota tano iliyo nje kidogo ya mji na wameahidi  kurudi na kombe Dar es Salaam.

Timu hiyo ambayo haikutaka kuweka wazi jina la hoteli,  imesafiri na wachezaji 24 pamoja  na viongozi 6,  ambao kama watafanya vizuri wataendelea kukaa kisiwani humo mpaka mashindano yatakapofikia kikomo Januari 13,  siku itakapochezwa mechi ya fainali.

Kocha wa Simba Masoud Djuma amesema, kikosi chao kimewasili salama na wanachofikilia wakati huu ni mechi yao ya kwanza kesho dhidi ya Mwenge itakayochezwa jioni kwenye Uwanja wa Amaan.

"Hatukuwa na muda wa kutosha kujiandaa, tumetoka kucheza mechi ya ligi Mtwara hatuja pumzika,  tumepitiliza kuja huku na kesho tunacheza, hata mazoezi mazuri ya maandalizi yetu hatujafanya," amesema Djuma.

Kocha huyo ambaye amerithi mikoba ya aliyekuwa mkuu, Mcameroon Joseph Omog amesema, pamoja na changamoto hizo,  watahakikisha wanafanya viziri kwenye mashindano haya.

Azam FC ndiyo mabingwa watetezi wa Kombe la Mapinduzi ambalo walilitwaa mikononi mwa Simba mechi ya fainali kwa ushindi wa bao 1-0,  lililofungwa na Himid Mao.