Nyota Madola kusaka medali kwa unyonge
Muktasari:
- Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe, anatarajia kuwaaga wanamichezo wa timu hiyo Dar es Salaam kabla ya kesho kupaa kwenda Australia.
Dar es Salaam.Wakati timu ya Tanzania ya michezo ya Madola inaagwa leo, matumaini ya kutwaa medali katika mashindano hayo ni madogo.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe, anatarajia kuwaaga wanamichezo wa timu hiyo Dar es Salaam kabla ya kesho kupaa kwenda Australia.
Michezo ya Madola imepangwa kuanza Aprili 4 hadi 15 na Tanzania itawakilishwa na timu nne za ngumi, riadha, kuogelea na tenisi ya meza.
Michezo ya Madola inayofanyika kila baada ya miaka minne, imepangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Carrara mjini Gold Coast.
Hata hivyo, matumaini ya Watanzania kupata medali ni madogo kutokana na morali ya ‘nyota’ kupungua kutokana na sababu mbalimbali.
Sababu morali kupungua
Iko hivi. Morali ya wachezaji imepungua kutokana na maandalizi duni tangu mwanzo baada ya timu hiyo kuanza kambi.
Timu hiyo ilifanya mazoezi katika mazingira magumu na baadhi ya mabondia walidai hawakuwa na vifaa vya michezo.
Pia mabondia hao walidai kupata mlo mmoja kwa siku, kutokuwa na posho ya nauli ya kwenda na kurejea nyumbani.
Ukiondoa changamoto hiyo, kuondolewa kambini kwa wanariadha nyota kulipunguza morali ya wengine kujituma katika mazoezi.
Baadhi ya wanariadha walikuwa tegemeo la Tanzania katika michezo hiyo na kukosekana kwao ni pigo kwa Watanzania.
Jeshi liliwaondoa kambini wanariadha tisa wa timu ya Taifa waliokuwa katika hatua za mwisho kwa mashindano ya kimataifa na kupelekwa kwenye mafunzo maalumu ya kijeshi.
Matumaini ya kutwaa medali katika riadha ni ndoto kwa kuwa nyota tegemeo Alphonce Simbu na Emmanuel Giniki hawapo katika kikosi hicho. Pia Agustino Sulle alitimuliwa kambini kwa madai ya utovu wa nidhamu.
Wasikie Kinyogoli, Shahanga
Bondia nguli wa zamani Habibu Kinyogoli na bingwa mara mbili wa Madola kwenye marathoni, Gidamis Shahanga kwa nyakati tofauti wametoa kauli kuhusu matumaini ya timu hiyo.
“Kukosekana kwa Simbu (Alphonce) na Giniki (Emmanuel) kumeharibu mipango, timu imekosa morali tofauti na awali, lakini wasikate tamaa,” alisema Shahanga. Kinyogoli alisema maandalizi ya mabondia hayakuwa mazuri kwa kuwa mwezi mmoja walioingia kambini ulikuwa muda mfupi.
“Muda hautoshi walipaswa kufanya maandalizi mapema, lakini nafasi ya kufanya vizuri kwa juhudi binafsi za mchezaji ipo,” alisema Kinyogoli.
Bayi wa TOC afunguka
Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi aliyewahi kuvunja rekodi ya dunia ya mita 1,500 katika Michezo ya Madola alisema kukosekana Giniki na Simbu kumepunguza morali ya timu.
“Tegemeo kubwa la medali lilikuwa kwenye riadha, alipoondoka Simbu, tulitegemea Giniki ndiye ‘atubebe’ naye pia hayupo, japo Failuna (Abdi) anapewa nafasi lakini morali ya mwanzo imepungua kutokana na sekeseke la wanariadha,” alisema Bayi.
Makocha watoa kauli
Kocha wa ngumi Benjamin Oyombi alisema ana uhakika wa kuiletea nchi medali moja ya ndondi kwenye michezo hiyo.
“Falsafa yangu naamini mabondia 10 wa timu moja wanaweza kuleta medali tatu, tuko wanne, natamani wote walete medali lakini haiwezekani, uhakika wa medali moja upo,” alisema kocha huyo raia wa Kenya.
“Tumefanya mazoezi kwa kiwango bora, tulicheza mechi za kimataifa za kirafiki baada ya kambi yetu ya awali ya China, tuko vizuri, hatuna cha kuhofia,” alisema kocha wa tenisi ya meza Issa Mtalaso.
Timu ya riadha inaundwa na Said Makula, Failuna Abdi, Stephano Huche, Sarah Ramadhani, Ali Gullam na Anthony Mwanga.
Ngumi Kassim Mbutike, Selemani Kidunda, Ezra Paul na Haruna Swanga.
Waogeleaji, Hilal Hilal na Sonia Tumiotto. Wachezaji wa tenisi ya meza, Amoni Amani, Masoud Mtalaso, Neema Mwaisyula na Fathiya Pazi.
Makocha ni Zacharia Barie na Lwiza John (riadha), Benjamini Oyombi (ngumi), Ramadhani Othman (tenisi ya meza) na Khalid Lushaka (kuogelea).
Wachezaji wanena
Failuna alisema hana hofu na ushindani ingawa amekiri kukosekana kwa Giniki, Simbu na Magdalena kumewavunja nguvu.
Nahodha wa ngumi Kidunda alisema maandalizi waliyoyafanya chini ya kocha Oyombi yananatoa taswira ya wao kufanya vizuri.
Pia Hilal nahodha wa kuogelea alisema kuwa watakwenda kushindana.