Kocha Simba aishi kifahari D’salaam

Friday January 12 2018

Kwenye picha ni mfano wa chumba cha hoteli

Kwenye picha ni mfano wa chumba cha hoteli ambacho kocha huyo anaishi jijini Dar es Salaam. Gharama ya kulala usiku mmoja ni mshahahra wa mtu. 

By MWANAHIBA RICHARD

SIMBA inajiweza kifedha kwa sasa asikwambie mtu. Katika kuthibitisha hilo imempa maisha ya kifahari kocha wake, Masudi Djuma, japo taarifa za chini chini zinadai kocha huyo wala hayafurahii hata kidogo.

Timu hiyo ya pili kwa kutwaa mataji mengi ya Ligi Kuu Bara imemkodia kocha huyo chumba katika moja ya hoteli za kisasa jijini Dar es Salaam (jina tunalo) ambapo gharama ya kulala usiku mmoja inakaribiana na mshahara wa waajiriwa wengi tu mjini.

Pamoja na kwamba kocha huyo amekuwa akiwasisitiza mabosi wake kuwa hafurahii maisha ya hotelini na kushinikiza wamtafutie nyumba, bado ameendelea kuishi hotelini hapo kwa siku 86 sasa.

Taarifa ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba awali mabosi wa Simba walimtafutia kocha huyo nyumba, lakini walichelewa kwenda kuilipia hivyo ikawahiwa na mteja mwingine.

Hata hivyo zipo taarifa pia kwamba kitendo cha Simba kuvurunda kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi nacho kimechelewesha mchakato wa kocha huyo kutafutiwa nyumba pamoja na gari ya kutembelea hivyo kuendelea kuishi hotelini hapo.

Kocha huyo ambaye alitua nchini Oktoba 19 mwaka jana kuchukua nafasi ya Mganda Jackson Mayanja, amekuwa akiishi hotelini hapo katika chumba ambacho kina kila kitu ndani ikiwemo sehemu ya kufanyia kazi na vikao vifupi.

Mwanaspoti ilizungumza na mmoja wa wahudumu wa hoteli hiyo ambaye aliomba hifadhi ya jina lake ambapo alisema kocha huyo bado yupo hotelini hapo tangu alipotua nchini na sasa ni siku ya 86 (hadi jana Alhamisi).

Mhudumu huyo alisema kuwa kwa siku Simba hulazimika kulipia Sh179,000 ingawa alidai kwa mtu ambaye ni mteja wao wa siku nyingi kunakuwepo na punguzo za asilimia kadhaa. 

Kwa hesabu za haraka, tangu kocha huyo Mrundi aanze kukaa hotelini hapo, Simba itakuwa imelipia kiasi cha Sh15.3 milioni (kabla ya punguzo), achilia mbali gharama nyingine.

“Ni kweli kocha wa Simba bado yupo hapa,  ni mteja wetu mzuri maana tunaingiza pesa, nafikiri kuna punguzo ambalo wamepata ila sijajua ni kwa asilimia ngapi maana mimi sio Mtendaji Mkuu wa hoteli hii japo baadhi ya mambo nayafahamu,” alisema mhudumu huyo.

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, alisema kwa sasa hawezi kuzungumza chochote ila atatoa taarifa rasmi baada ya siku tatu juu ya maisha halisi ya kocha huyo.

Naye Mratibu wa Simba, Abbas Ally, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwani hafahamu kama kocha huyo alikubaliana na uongozi atakaa hotelini hapo ama atatafutiwa nyumba.

Kwa upande wake Djuma, alikiri kuishi hotelini.

Mwanaspoti linafahamu kocha huyo bado hajapewa hata gari ya kutembelea kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake,   Joseph Omog. Taarifa ambazo tunazo ni kwamba Djuma anahitaji gari la kifahari jambo ambalo linachelewesha mchakato wake.