Balotelli afura kutemwa Italia

Muktasari:

Wakala wa mchezaji huyo Mino Raiola alisema mteja wake amekasirishwa kuachwa na kocha Luigi Di Biagio kujiandaa na mechi mbili dhidi ya Argentina na England.

 Rome, Italia. Mshambuliaji mtukutu wa timu ya Nice, Mario Balotelli amechukizwa na kitendo cha kutemwa katika kikosi cha Italia.

Wakala wa mchezaji huyo Mino Raiola alisema mteja wake amekasirishwa kuachwa na kocha Luigi Di Biagio kujiandaa na mechi mbili dhidi ya Argentina na England.

Raiola mmoja wa mawakala maarufu Ulaya, alisema Di Biagio hakuwa na sababu ya kumtosa Balotelli kwa kuwa anafanya vyema katika Ligi Kuu Ufaransa.

Mshambuliaji huyo amefunga mabao 22 katika michezo 31 aliyocheza msimu huu akiwa na kikosi cha Nice.

“Hatukufurahishwa na uamuzi wa kumuacha    Balotelli, pia hatukupendezwa na taarifa zilizotolewa hadharani,”alidai Raiola.

Alisema ameshangazwa na uamuzi wa kocha kumtema Balotelli akiwa kwenye kiwango bora msimu huu ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2014.

“Di Biagio angesema idadi ya washambuliaji wa timu ya Taifa kwa mchezaji kama yeye imetosha. Nadhani tatizo sio kocha, ni mfumo mzima wa soka Italia,”alisema Raiola.

Wakala huyo alisema vigogo wa Shirikisho la Soka Italia wanafanya kazi bila malengo, mtazamo wa mbali na timu ya Taifa inatakiwa kuundwa na wachezaji bora.