Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nyika: Hivi ndo namna alijigeuza kinyozi kumnasa Fei Toto

Muktasari:

Nyika msimu uliopita tu wakati uongozi mpya ulipoingia ndio alikuwa anamaliza kipindi chake katika uongozi ndani ya klabu hiyo.

KIONGOZI wa zamani na mdau mkubwa wa Yanga, Hussein Nyika, ana stori nyingi utakazopenda kuzifahamu kutoka ndani ya klabu hiyo kuanzia uendeshaji hadi umafia unaofanyika katika kuwasajili nyota katika klabu hiyo ya Jangwani.

Alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na pia alifanya kazi katika Kamati ya Usajili iliyokuwa chini ya mwenyekiti na makamu wake Abdallah Bin Kleb na Seif ‘Magari’ Ahmeid na huko kote walifanya mambo makubwa tangu alipopata ridhaa hiyo baada ya kushinda kiti cha Mjumbe wa Kamati ya Utendaji katika uchaguzi wa klabu hiyo wa mwaka 2014.

Nyika msimu uliopita tu wakati uongozi mpya ulipoingia ndio alikuwa anamaliza kipindi chake katika uongozi ndani ya klabu hiyo.

Huyu hapa anasimulia mambo aliyopitia klabuni hapo:

Majukumu ya usajili

Anasema: “Kuhusu usajili mambo yalikuwa na ugumu wake na nirudie, nikifika katika eneo hili nawakumbuka sana walimu wangu Bin Kleb, Sief Magari na Mhandisi Isack Chanji ambao bila mafunzo yao kazi hii nisingeiweza. Walinifundisha jinsi ya kuwa jasiri na kutokukubali matokeo kirahisi kuanzia mazungumzo na mchezaji hadi unafanikisha.

“Kuna watu walikuwa hawaelewi kwanini tuliamua kuwa wazungumzaji sana. Kuna mambo yalikuwa hayako sawa, sasa huwezi kuwa kimya na mambo yanakwama. Ilikuwa lazima ukifanikisha jukumu moja unalazimika kuongea kidogo ili kuwatisha timu pinzani na nashukuru ilitusaidia, tulikuwa hatuna pesa makocha wanataka wachezaji, mashabiki wanahitaji kuona timu inasajili.”

Bajeti ya usajili finyu

Klabu yoyote inapofika wakati wa usajili hutenga fungu maalum kwa zoezi hilo na hapa Nyika anaeleza walichokuwa wanapata kutoka katika klabu.

“Wengi wanadhani kwamba tulikuwa tunapata fedha za kusajilia kama bajeti, lakini nakumbuka mara ya mwisho Kamati ya Usajili kupewa fedha ilikuwa ni wakati wa Mhandisi Clement Sanga anakaimu nafasi ya mwenyekiti alipotupa kiasi cha Sh 180 milioni kama bajeti. Tuliishiwa nguvu, lakini ukweli ni kwamba klabu haikuwa na pesa, nilimuelewa kwa kuwa nilikuwa ndani ya kamati ya utendaji.

“Kiasi kama hicho kilikuwa kinatosha kusajili kama sio mchezaji mmoja basi wawili tena kwa kujibana sana kulingana na soko la kibiashara. Sasa unaweza kujiuliza tulikuwa tunapata wapi pesa? Ilitulazimu kutanua wigo kwa kuwakaribisha wadau mbalimbali ili tusaidiane majukumu.

“Tulichokuwa tunafanya ni wakati tunataka kumsajili mchezaji fulani tunamuita mezani tunajadiliana naye na tutakachokubaliana tunaanza kuchangishana hapohapo mpaka tunakamilisha zoezi.”

Filamu la Fei Toto

“Ngoja nikwambie stori mmoja. Nakumbuka mambo yalikuwa magumu sana (anacheka) wakati tunamhitaji Feisal Salum ‘Fei Toto’. Alikuja hapa kwenye mashindano ya Sportpesa, alifanya vizuri sana lakini watu wengi hawakujua kama Yanga ilikuwa inamfuatilia kwa muda mrefu huko nyuma.

“Wakati tunamuona Feisal tukataka kumalizana naye, lakini kocha wetu wa wakati huo Lwandamina (George) alisema tusubiri kwanza amuangalie zaidi, akisema apewe mkataba wa awali, tukafanya hivyo. Lwandamina akatuambia tutangulie kumchukua Martin (Emmanuel) tukamsajili. Baada ya muda, Feisal alikuja tena hapa Dar es Salaam katika mashindano ya Sportpesa. Fei Toto alifanya vizuri sana kumbe kabla hajaja tayari Singida walishampa mkataba kamili wakati huo sisi tulimpa mkataba wa awali.

“Mashindano yalipomalizika Simba wakaongezeka katika timu zinazomuhitaji na kuna timu nyingine kubwa tu nao walianza kumfuatilia, tukapewa taarifa

Timu yake wakati huo JKU ilikuwa imefikia Bondeni Hotel. Tukazungumza naye tukapeana muda kwamba kesho yake tuonane lakini usiku wake Simba wakaingia kazini wakafanikiwa kumtoa hadi nje ya hoteli na kwenda kufanya naye mazungumzo na pia wakakubaliana kila kitu kuwa, nao kesho yake wakamalizane kama ambavyo sisi tulipewa ahadi.

“Aliporudi saa nane usiku, Yanga tukapewa taarifa usiku huohuo kuwa kijana alitoka na kama tukichelewa tutalizwa. Kesho yake tukajipanga jinsi ya kuingia pale mchana. Ikatuwia ugumu. Nakumbuka nilikuwa na makamu wangu marehemu Mustapha Urungo.

“Tukajipanga. Ikabidi mimi nijifanye kinyozi kwamba Fei Toto ameniita anataka kunyoa, lakini pia makamu wangu akajifanya dereva wa teksi. Mimi kinyozi nikaruhusiwa kuingia ndani ya hoteli, dereva akaambiwa asubiri nje.

“Niliingia ndani na kukutana na Fei. Tukaongea na kumuomba tutoke ili tukaongee zaidi akaomba ruhusa akakubaliwa, baadaye makamu wangu ikabidi abadili gari akachukua gari nyingine na kurudi pale hotelini, lakini safari hii hakushuka katika gari yenye vioo vyeusi. Akawapigia simu viongozi wa JKU na kocha wao lakini sasa akijitambulisha kama kiongozi wa Yanga.

Wale viongozi walikubali na walipofika ndani ya gari akawaomba waende sehemu wakaongee. Tukaenda wote Temeke tukiwa na mchezaji na hao viongozi, lakini akili tuliyotumia Fei tulimuhamishia katika gari ya Bin Kleb ambaye tulimuita aje aongeze nguvu na hakujua kama katika gari nyingine kuna viongozi wake.

“Tukazungumza na viongozi wake tukakubaliana. Sasa wao wakatuambia ofa ambazo Fei anazo na mwisho tukakubaliana. Lakini wakasema zoezi haliwezi kukamilika hadi wakaongee na mchezaji. Sisi tukaawambia mambo ya mchezaji waachane nayo kwani tutamalizana naye tu, wakagoma. Mwisho ikabidi tuwaambie kuwa mchezaji yuko hapa eneo hilohilo. Wakakataa ikabidi tukafungue kioo upande wa pili waamini. Walipomuona walichoka kabisa.

Simba warudi kazini

“Wakati tukiwa katika maongezi hayo kule hotelini, Simba walirudi kufuatilia ahadi yao ya jana yake.Tukapewa taarifa, wakaambiwa lwamba si mchezaji wala viongozi wote hawapo. Wakaanza kupiga simu sana. Kumbe wakati tunatoka pale kuna watu kwenye gari walimuona Fei akiondoka hivyo gari hiyo ikawa inatufuatilia lakini bahati nzuri kuna sehemu tuliitoroka hawakujua tumeleekea wapi. Jamaa wakaanza kumsumbua mchezaji kwa simu.

“Wakati mazungumzo yanaendelea tulipoona simu za Simba zimezidi tukasema hapana pale tuhame, tukaondoka kundi lote bila ya kujua tunaenda wapi. Kitu kibaya zaidi wakati wote wa majadiliano maafikiano ya pesa yalikuwa bado.

“Tukakubaliana twende Posta katika ofisi moja ya mjumbe wetu Mashauri (Lucas). Baada ya kukubaliana na klabu yake mchezaji akasema pesa ambayo alipewa Singida United Sh 18 milioni ameshaila na hawezi kukubaliana hivihivi akasema anataka aongezwe fedha.

BinKleb avunja safari

“Nakumbuka tulianza saa tano mpaka tunafikia makubaliano ilikuwa saa nane mchana mwenzetu BinKleb akaamua kuvunja safari yake ya nje ya nchi ili zoezi likamilike akiwa tayari ameshakata tiketi ya ndege. Tukawasiliana na Singida nashukuru bosi mkuu wa Singida Mwigulu (Nchemba) tulimshirikisha na kumwambia ukweli akatupa ruhusa kwamba kama tumefikia hapo na yeye ni mwenzetu basi fedha alizompa Fei utakuwa ni mchango wake sasa tukaanza kutafuta fedha zaidi za kumalizana na mchezaji na klabu yake.

“Tulishikana pale kama viongozi mpaka mwisho tukafanikiwa kukamilisha mchakato. Nakumbuka BinKleb aliagiza fedha zije tena sio kwa gari bali kwa bodaboda mpaka tulipokuwa na nawashukuru viongozi wenzangu Mashauri na wajumbe wengine mpaka baadaye tukafanikiwa.”

Usikose sehemu ya pili kesho upate masimulizi zaidi.