Balama Mapinduzi: Zahera alitupa programu ya mazoezi ya kesho

Muktasari:

Benchi la ufundi la Yanga sasa litasimamiwa na kocha Charles Boniface Mkwasa kwa muda

Dar es Salaam. Wakati Mwinyi Zahera akitupiwa virago Yanga, mchezaji wa timu hiyo, Balama Mapinduzi amesema imekuwa kama sapraizi kwao.

Yanga imetangaza kuachana na kocha huyo Mkongo ikiwa ni siku chache tangu walipoondoshwa katika mashindano ya kimataifa.

"Ni kama sapraizi kwetu, tulikuwa naye mazoezi ya leo asubuhi wala hakuonyesha kama kuna taarifa yoyote juu ya kuondoka.

"Amesimamia mazoezi leo Jumanne mwanzo mwisho, akatupa na programu ya kesho, hii taarifa ya kwamba ametimuliwa ni sapraizi kwangu," alisema mchezaji huyo.

Balama ameungana na Feisal Salim (Fei Toto) ambaye pia amesema kuondoka kwa Zahera ni jambo geni kwake.

"Mbona tulikuwa naye mazoezi na hakuonyesha dalili yoyote wala kutuaga kwamba anaondoka, sitaki kuamini kama ni kweli japo hiyo ni kawaida kwa makocha," alisema Fei Toto.