Mkwasa apewa mikoba ya Zahera Yanga

Muktasari:

Msola alisema pia wameamua kuvunja benchi zima la ufundi na kuanza upya huku kama kukiwa na yeyote ambaye atarejeshwa basi itafahamishwa.

Dar es Salaam.Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla ametangaza Charles Boniface Mkwasa atakuwa kocha wa muda wa Yanga kuchukua jukumu la Mwinyi Zahera kwa muda wa wiki mbili.

Msola alisema wameamua kufikia hatua ya kumvunjia mkataba Zahera baada ya kukaa na kuzungumza na pia kuona Mkwasa anafaa kuishika timu hiyo kwa muda baada ya kuachana na kocha wao.

"Mkwasa ndio atakayekuwa na timu hii kwa muda wa takribani wiki mbili wakati huo tukiangalia kocha wa kudumu, pia Mkwasa hatoweza kukaa peke yake kwahiyo tutakaa naye na kujua atakuwa na nani," alisema.

Mkwassa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Yanga alijiondoa katika nafasi hiyo kutokana na kusumbuliwa na maradhi.

Akizungumzia suala la afya ya Mkwasa, Msola alisema "Mpaka tumefikia hatua hii maana yake Afya yake ni nzuri, lakini sio jambo sahihi kulizungumzia hapa."

Msola alisema pia wameamua kuvunja benchi zima la ufundi na kuanza upya huku kama kukiwa na yeyote ambaye atarejeshwa basi itafahamishwa.

"Hii tunasafisha wote na tunakuwa wapya kwahiyo kama yùpo atakayerejea basi itatangazwa pia," alisema.

Mkwassa anachukua jukumu hilo kuanzia leo akiwa na kibarua kizito cha kuivaa Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara Alhamisi hii.

Januari 31, 2017, Yanga ilimtangaza Mkwassa kuwa katibu mkuu wake mpya, pia kiungo huo wa zamani alikuwa kocha msaidizi wa Yanga chini ya Hans Pluijm na baadaye kocha mkuu.