Zirkzee apanga kuikimbia Manchester United Januari
Muktasari:
Tangu msimu huu ulipoanza Zirkzee amekuwa akianzia benchini, ambapo ameanza katika mechi chache za mashindano Ulaya licha ya kwamba alihusika kwa kiasi kikubwa kwenye maandalizi ya msimu mpya wa mashindano, ikiwamo katika ziara ya mechi zilizopigwa Marekani.
MSHAMBULIAJI wa Manchester United na timu ya taifa ya Uholanzi, Joshua Zirkzee (24), huenda kaondoka katika dirisha dogo lijalo la Januari, 2026 ili kutafuta nafasi ya kucheza zaidi aweze kujumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa kitakachoshiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Amerika.
Tangu msimu huu ulipoanza Zirkzee amekuwa akianzia benchini, ambapo ameanza katika mechi chache za mashindano Ulaya licha ya kwamba alihusika kwa kiasi kikubwa kwenye maandalizi ya msimu mpya wa mashindano, ikiwamo katika ziara ya mechi zilizopigwa Marekani.
Mchezaji huyo amekuwa akisugua benchini kutokana na uamuzi wa kocha Ruben Amorim kumtumia Matheus Cunha na wakati mwingine Benjamin Sesko ambao wanapishana eneo la ushambuliaji, huku wakati mwingine akiingia na mfumo usiohitaji mshambuliaji kamili pale mbele.
Hata hivyo, Zirkzee anadaiwa kwamba kwa sasa anaangalia uwezekano wa kurejea Italia alikokuwa akikipiga katika timu ya Bologna kabla ya kutua Manchester United.
Kobbie Mainoo
KIUNGO wa Manchester United na England, Kobbie Mainoo, 20, amesisitiza kwamba anataka kuondoka ifikapo Januari, mwakani, huku Napoli ikatajwa kumhitaji akaungane na wakali wengine waliotokea Old Trafford, Rasmus Højlund aliyetua kwa mkopo dirisha kubwa lililopita na Scott McTominay. Hata hivyo, Man United imekuwa ikisisitiza kwamba mchezaji huyo hauzwi wala kutolewa kwa mkopo msimu huu, na pia haina mpango wa kusikiliza ofa yoyote. Mkataba wake unamalizika 2027.
Harry Maguire
BEKI wa kimataifa wa England na Manchester United, Harry Maguire, 32, ana mpango wa kuendelea kubaki katika timu hiyo kwa muda mrefu zaidi, lakini unaweza kumgharimu kwani atalazimika kukubali kupunguziwa mshahara iwapo atasalia hapo. Maguire aliyetua Old Trafford akitokea Leicester City 2019, mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu, lakini amekuwa kipenzi cha kocha Ruben Amorim ambaye amekuwa akimpa nafasi ya kuanza kikosini mara kwa mara.
Axel Disasi
KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca hana mpango wa kumrejesha kikosini beki wa kimataifa Ufaransa, Axel Disasi, 27, licha ya kwamba anakabiliana na janga la majeraha kwa sasa. Yuko kwa mkopo katika timu ya Aston Villa, ambako amekuwa kwenye ubora wa kiwango cha juu. Disasi aliyetua Darajani 2023 akitokea Monaco, alitolewa kwa mkopo Villa dirisha lililopita la usajili kutokana na kutokuwa sehemu ya mipango ya Maresca.
Harry Wilson
LEENDS United iko katika mawindo kuisaka saini ya winga wa kimataifa wa Wales anayekipiga Fulham, Harry Wilson, 28.
Timu hiyo imemuweka mchezaji huyo kwenye rada zake za wakali inaowataka katika dirisha la Januari baada ya kufeli kumsajili siku ya mwisho ya uhamisho wa dirisha kubwa lililopita. Wilson anatarajia kumaliza mkataba wake na Fulham ifikapo mwakani.
Raphinha
MACHESTER United inapanga kupiga hodi Barcelona kumtaka winga wa zamani wa Leeds United na Brazil, Raphinha, 28, baada ya mkali huyo kutesa akiwa Camp Nou tangu 2022. Hata hivyo, huenda Masheatni Wekundu wakajikuta wakitoboka mzigo mkubwa unaofikia Pauni 120 milioni. Raphinha ambaye kwa sasa ni majeruhi, nafasi yake inatishiwa na ujio wa Marcus Rashford ambaye ameng’ara.
Antoine Semenyo
BOURNEMOUTH inatarajia kupokea ofa kubwa kutoka kwa baadhi ya timu kubwa za England kutokana na kiwango anachoonyesha beki huyo katika msimu huu, Manchester United na Liverpool zikiwa kati ya zile zinazomfukuzia mchezaji huyo kwa sasa. Hata hivyo, kwa ubora wake, bei yake inaweza kuwa kubwa zaidi ikitajwa kuzidi Pauni 75 milioni.
Karim Adeyemi
BARCELONA huenda ikaongeza juhudi za kumsajili mshambuliaji wa Borussia Dortmund na Ujerumani, Karim Adeyemi, mwenye umri wa miaka 23, majira ya kiangazi mwakani licha ya mkataba wake na klabu hiyo ya Bundesliga kumalizika 2027. Mchezaji huyo amegeuka kuwa tegemeo katika kikosi cha Dortmund msimu huu ambako hadi sasa ameshatupia nyavuni mabao matano kwenye mechi nne.