Everton inasikilizia kwa Gabriel Jesus
Muktasari:
- Inaelezwa Arsenal inataka kumuuza fundi huyu kwa sababu Kocha Mikel Arteta haoni kama yupo katika mipango yake kutokana na majeraha ya mara kwa mara yanayomwandama.
ARSENAL inadaiwa ipo tayari kukubali ofa ya takribani Pauni 30 milioni kwa ajili ya kumuuza mshambuliaji wao wa kimataifa wa Brazil, Gabriel Jesus,28, dirisha lijalo la majira ya baridi.
Inaelezwa Arsenal inataka kumuuza fundi huyu kwa sababu Kocha Mikel Arteta haoni kama yupo katika mipango yake kutokana na majeraha ya mara kwa mara yanayomwandama.
Everton ni miongoni mwa timu zinazoitamani sana saini yake lakini haitaki kutoa kiasi hicho cha pesa kwani inaona ni kingi na badala yake inataka kumchukua kwa mkopo wa nusu msimu ambao utakuwa na kipengele cha kumnunua mazima ikiwa kwa masharti maalumu ikiwemo kufunga idadi fulani ya mabao.
Jesus mwenyewe ambaye alijiunga na Arsenal kutoka Manchester City mwaka 2022 kwa ada ya takribani Pauni 45 milioni anataka kuondoka kujaribu changamoto mpya sehemu nyingine baada ya kupona majeraha yake kwani nafasi yake pia ni finyu katika kikosi kutokana na usajili ambao umefanyika hadi sasa.
Mkataba wa staa huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2027 na anatarajiwa kupona majeraha yake Januari mwakani.
Bruno Fernandes
MANCHESTER United imepanga kujadili ofa kutoka Saudi Arabia kwa ajili ya kumuuza kapteni wao Bruno Fernandes, mwenye umri wa miaka 31. Mabosi wa Man United wataanza kwanza kwa kumsikiliza Bruno mwenyewe kabla ya kuanza kusikiliza ofa za timu zinazomhitaji. Fernandes ambaye alijiunga na Man United mwaka 2020, hadi sasa amecheza mechi 270 za michuano yote akiwa na timu hiyo na amekuwa akionyesha nia ya kutaka kuendelea kusalia Old Trafford .
Kobbie Mainoo
NAPOLI inadaiwa kuongoza vita ya kuiwania saini ya kiungo wa Manchester United, Kobbie Mainoo, mwenye umri wa miaka 20, dirisha lijalo la Januari. Mainoo ni miongoni mwa mastaa ambao kocha Ruben Amorim anaona haendani na mifumo yake ba amekuwa hampi nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza. Licha ya kutokuwa katika mipango ya Amorim, Man United iligoma kumwachia staa huyu dirisha lililopita ingawa kulikuwa na timu zilizohitaji huduma yake.
Dayot Upamecano
BARCELONA imepanga kuingia kwenye ushindani na Liverpool kwa ajili ya kumsajili beki wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ufaransa, Dayot Upamecano, 26, pindi mkataba wake utakapomalizika mwisho wa msimu huu. Upamecano ni miongoni mwa mastaa tegemeo wa Bayern na licha ya timu hiyo kumpa ofa ya mkataba mpya, amekataa kusaini hadi sasa ikielezwa anataka changamoto mpya sehemu nyingine.
Elliot Anderson
LICHA ya kumuuza miezi 16 iliyopita, Newcastle United inafikiria kuingia katika mazungumzo na Nottingham Forest ili kuipata huduma ya kiungo wao wa zamani, Elliot Anderson, mwenye umri wa miaka 22. Anderson ambaye alilelewa katika akademi ya Newcastle, aliuzwa kwa dau la takribani Pauni 35 milioni kwenda Forest mwaka jana na ameonyesha kiwango bora tangu atue timu hiyo kiasi cha kuivutia tena Newcastle kutaka kumrudisha.
Nahuel Molina
KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola amewasilisha jina la beki wa kulia wa Atletico Madrid, Nahuel Molina kwa mabosi wa timu hiyo akihitaji asajiliwe dirisha lijalo. Beki huyo, 27. Molina, amekuwa nguzo muhimu ya safu ya ulinzi katika kikosi cha Diego Simeone na timu ya taifa ya Argentina na Atletico huenda ikamuuza ikiwa itapewa Pauni 50 milioni, jambo ambalo Pep anasisitiza aletwe fasta.
Federico Chiesa
LICHA ya kuhitajika na timu mbalimbali za Italia, Mshambuliaji wa Liverpool, Federico Chiesa, 27, amesisitiza bado anatamani kuendelea kusalia na majogoo hao. Chiesa alisajiliwa kutoka Juventus dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana kwa Pauni 55 milioni lakini amekuwa hapati nafasi ya kutosha kikosi cha kwanza jambo lililoziaminisha AC Milan na Inter Milan zitampata.
Jurrien Timber
BAYERN Munich ni moja ya klabu zinazoiwania saini ya beki wa Arsenal, Jurrien Timber, 24, ambaye hivi karibuni ameanza mazungumzo ya mkataba mpya na washika mitutu hao. Timber alisajiliwa kutoka Ajax kwa takribani Pauni 38 milioni mwaka 2023, lakini hakucheza sehemu kubwa ya msimu wa kwanza kutokana na majeraha na baada ya kurejea ameonyesha kiwango bora kilichozivuti timu nyingi.