Juventus, Barcelona zinapigana vikumbo kwa Bernardo Silva
Muktasari:
- Kwa mujibu wa tovuti ya Caught Offside, Bernardo ana mkataba na Man City hadi mwaka 2026 na anaonekana kuwa tayari kuondoka na kupata changamoto mpya sehemu nyingine.
BARCELONA na Juventus zimepanga kumsajili kiungo wa Manchester City, Bernardo Silva,31, ambaye pia anawindwa na timu za Saudi Arabia zikiwamo Al-Ahli, Al-Qadsiah na Al-Nassr.
Kwa mujibu wa tovuti ya Caught Offside, Bernardo ana mkataba na Man City hadi mwaka 2026 na anaonekana kuwa tayari kuondoka na kupata changamoto mpya sehemu nyingine.
Timu za Saudi Arabia zipo tayari kumpa mshahara wa zaidi ya Pauni 800,000 kwa wiki, karibia mara tatu zaidi ya ule anaoupata kwa sasa wa Pauni 300,000 kwa wiki.
Silva pia anatajwa pia kuwa na mpango wa kurudi Benfica lakini kwa sasa mpango huo unaonekana kuwa mgumu kutokana na ofa nono ambazo timu nyingine zinahitaji kumpa.
Silva amekuwa na mafanikio makubwa taajiunge na Man City mwaka 2017 na ameshinda mataji matano ya Ligi Kuu England, moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya na matatu ya Kombe la Carabao.
Tangu kuanza kwa msimu huu Silva amecheza mechi 12 za michuano yote, akafunga bao moja na kutoa asisti moja.
Adam Wharton
CRYSTAL Palace inapanga kumpa kiungo wao chipukizi Adam Wharton, 21, mkataba mpya ili kuzuia asiondoke dirisha lijalo la majira ya kiangazi na Liverpool, Chelsea na Manchester City zinahitaji huduma yake. Wharton, amekuwa mmoja wa viungo wanaochipukia kwa kasi EPL na ameonyesha kiwango bora tangu kuanza kwa msimu huu. Kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail, katika mkataba huo mpya, Palace inataka kumpa mshahara mara mbili ya ule anaoupokea kwa sasa.
Kobbie Mainoo
NAPOLI inadaiwa ndiyo inaongoza katika mbio za kumsajili kiungo wa Manchester United, Kobbie Mainoo, 20, dirisha lijalo la majira ya baridi. Kwa mujibu wa tovuti ya Sky Switzerland, Napoli imekuwa ikifuatilia maendeleo ya Mainoo tangu kuanza kwa msimu huu na wanaamini atakuwa suluhisho kwa tatizo lao la kukosekana kwa ubunifu katika eneo la kiungo. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
William Osula
Eintracht Frankfurt ya Ujerumani inataka kumsajili kwa mkopo mshambuliaji wa Newcastle United, William Osula, 22. Kwa mujibu wa Sky Sports, Frankfurt inataka kumchukua dirisha la Januari ili kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji baada ya kutetereka katika Bundesliga msimu huu. Osula, ambaye alilelewa katika akademi ya Sheffield United, anasifika kwa kasi na nguvu, lakini hajapata nafasi ya kutosha katika kikosi cha Newcastle.
Karim Adeyemi
BARCELONA inapanga kufanya usajili wa mshambuliaji wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Ujerumani, Karim Adeyemi,23. Staa huyu amekuwa akifuatiliwa na Barca tangu mwaka 2023 na sasa Hans Flick naye anatamani sana kuipata saini yake. Mkataba wa Adeyemi unatarajiwa kumalizika mwaka 2027 na Dortmund inadaiwa kuhitaji zaidi ya Euro 40 milioni ili kumuuza.
Rodri
MANCHESTER City imesisitiza haina nia ya kumuuza kiungo, Rodri, 29, dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Kwa mujibu wa tovuti ya Teamtalk, Madrid ilikuwa inamfikiria Rodri kama mrithi wa muda mrefu wa Toni Kroos, lakini Man City haitaki kumwachia. Rodri amekuwa mhimili wa kikosi cha Pep Guardiola kwa muda mrefu licha ya majeraha ya mara kwa mara ambayo amekuwa akikutana nayo hivi karibuni.
Arda Guler
REAL Madrid haina mpango wa kumruhusu kiungo wao wa kimataifa wa Uturuki, Arda Guler, 20, dirisha lijalo la majira ya baridi. Hivi karibuni kumekuwa na timu kibao ikiwemo Arsenal na Newcastle zinazohitaji kumsajili. Kwa mujibu wa Football Insider, Madrid inataka Guler aendelee kujengeka akiwa ndani ya kikosi na sio nje.
Yehor Yarmolyuk
MANCHESTER United imeanza mazungumzo na Brentford ili kuipata saini ya kiungo wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Ukraine, Yehor Yarmolyuk,21, dirisha la Januari. Staa huyu anaonekana kama mbadala wa muda mrefu wa Casemiro anayeweza kuondoka mwisho wa msimu huu. Alijiunga na Brentford mwaka 2022 kutoka Dnipro-1 ya Ukraine na msimu uliopita alicheza mechi 34 za michuano yote.