Ya Manchester United, yamkuta Rashford Barca
Muktasari:
- Ikumbukwe, mshambuliaji huyo aliwahi kuwekwa benchini wakati akiwa Man United chini ya kocha Erik Ten Hag kwa makosa kama hayo na kwenye mechi hiyo ya La Liga dhidi ya Getafe ya ushindi wa mabao 3-0, kwa mujibu wa tovuti ya Mundo Deportivo ya Hispania, kocha wa Barca, Hansi Flick hakumwanzisha kwa sababu alichelewa kuhudhuria mkutano wa timu siku hiyo baada ya mazoezi.
BARCELONA, HISPANIA: NYOTA wa Barcelona, Marcus Rashford yamemkuta kama yaliyotokea akiwa na kikosi cha Manchester United kwa kupewa adhabu ndogo ya kukaa benchi na kucheza kipindi kimoja kwa kosa la kuchelewa kikao cha timu.
Ikumbukwe, mshambuliaji huyo aliwahi kuwekwa benchini wakati akiwa Man United chini ya kocha Erik Ten Hag kwa makosa kama hayo na kwenye mechi hiyo ya La Liga dhidi ya Getafe ya ushindi wa mabao 3-0, kwa mujibu wa tovuti ya Mundo Deportivo ya Hispania, kocha wa Barca, Hansi Flick hakumwanzisha kwa sababu alichelewa kuhudhuria mkutano wa timu siku hiyo baada ya mazoezi.
Rashford aliingizwa uwanjani kipindi cha pili wakati Barca ikiwa inaongoza kwa mabao mawili yaliyofungwa na Ferran Torres, aliyeanza badala ya mchezaji huyo wa timu ya taifa ya England.
Hata hivyo, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Newcastle United Alhamisi iliyopita, nyota huyo aliyejiunga na Barca kwa mkopo akitokea Man United, alifunga mabao mawili na kuipa timu yake pointi tatu muhimu katika ushindi wa mabao 2-1.
Akiwa na miamba hiyo ameanza mechi tatu na ameonyesha kiwango bora chini ya Flick, lakini Mjerumani huyo hana uvumilivu hata kidogo linapokuja suala la kuchelewa au utovu wa nidhamu.
Kocha huyo wa zamani wa Bayern Munich ana sera ya kutochagua wachezaji kuanza mchezo ikiwa watachelewa kufika mazoezini au katika mikutano ya timu.
Mwaka jana, wachezaji Inaki Pena, Jules Kounde na Raphinha pia walikumbwa na hali ya kuwekwa benchini baada ya kuchelewa.
Hali hiyo pia ilitokea kwa Raphinha wiki iliyopita lakini baadaye aliingizwa na akafunga mabao mawili katika ushindi wa 6-0 dhidi Valencia.
Mundo Deportivo inadai Rashford alichelewa dakika mbili tu kufika kwenye mkutano kwa sababu hakufika kwa wakati eneo la kusaini wachezaji kila wanapoingia.
Kabla ya uhamisho wake wa majira ya joto kwenda Barca, kocha wa sasa wa Old Trafford, Ruben Amorim alimtoa Rashford kwa mkopo kwenda Aston Villa kutokana na kutovutiwa na kiwango chake mazoezini.
Rashford aliifungia Villa mabao manne katika mechi 17, lakini haikutosha kurejesha nafasi yake Man United na hivyo kutolewa kwa mkopo kwenda Barca dirisha lililopita.