Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wikiendi ya vipigo, maokoto England

EPL Pict

Muktasari:

  • Itakumbukwa kwamba wiki iliyopita timu tatu zinazochuana juu kwenye msimamo wa ligi hiyo zilipoteza pointi; Arsenal na Man City zilitoka sare dhidi ya Newcastle United na Fulham mtawalia wakati Brighton ilishtukizwa kwa kufungwa mabao mawili katika muda wa nyongeza na Hull City.

LONDON, ENGLAND: WIKI hii, wakubwa wa Ligi Kuu England wanapambana kuimarisha nafasi zao katika msimamo wa ligi hiyo kwa ushindani mkali.

Itakumbukwa kwamba wiki iliyopita timu tatu zinazochuana juu kwenye msimamo wa ligi hiyo zilipoteza pointi; Arsenal na Man City zilitoka sare dhidi ya Newcastle United na Fulham mtawalia wakati Brighton ilishtukizwa kwa kufungwa mabao mawili katika muda wa nyongeza na Hull City.

Hata hivyo, Liverpool ilitumia vizuri matokeo hayo kupunguza pengo la pointi baada ya kuichapa Manchester United mabao 4-0, ikiwa imecheza dhidi ya wapinzani waliokuwa na wachezaji 10 uwanjani. Kuanza vibaya kwa Mauricio Pochettino kuliifanya Manchester United kuendelea kubaki katika nafasi tatu za mwisho kwenye msimamo wa ligi. Wiki ya 12 ya michuano hiyo ina mechi zilizoanza jana Ijumaa, leo Jumamosi na kesho Jumapili.


LEO, JUMAMOSI


EP 01

LEEDS UNITED VS COVENTRY CITY

Ratiba ya Jumamosi itakuwa na michezo michache, ikianza saa 12:00 jioni, ambapo Leeds United itakuwa na lengo la kusogea karibu na nafasi nne za juu itakapokuwa mwenyeji wa Coventry City, ambapo Leeds inapewa nafasi ya asilimia 56.8 ya kushinda, ikiwa ndiyo timu yenye uwezekano mkubwa zaidi wa kupata ushindi katika wiki ya 12.

Hilo halishangazi kutokana na rekodi yake dhidi ya Coventry, kwani imepoteza mchezo mmoja pekee kati ya mechi zake 23 za mwisho za nyumbani dhidi ya timu hiyo katika ligi. Katika michezo hiyo, Leeds imeshinda mara 16 na kutoka sare sita. Kipigo chake pekee kilikuwa cha mabao 3-1, kilichotokea Desemba 1996.

Coventry ilipoteza mechi zote mbili za ligi dhidi ya Leeds bila kufunga bao walipokutana mara ya mwisho katika Championship msimu wa 2024/25. Ingawa mambo mengi yamebadilika tangu wakati huo, Opta inaipa Coventry nafasi ndogo ya asilimia 20.8 ya kupata ushindi katika mchezo huu.


EP 02

MAN UNITED VS BRENTFORD

Manchester United itakuwa na lengo la kusahau haraka mwanzo wake mbaya chini ya kocha Mauricio Pochettino itakapokutana na Brentford, ambayo imekuwa na kiwango kizuri. Pochettino anaingia katika mchezo wake wa kwanza wa nyumbani akiwa kocha wa United baada ya kichapo cha mabao 4-0 dhidi ya Liverpool na sare ya mabao 2-2 dhidi ya Sporting CP katika Ligi ya Mabingwa Ulaya mechi zote zilizopigwa ugenini.

Hata hivyo, United inapewa nafasi ya asilimia 44.1 ya kushinda, ikilinganishwa na 29.1 za Brentford.

United haijashinda mchezo wowote kati ya tisa iliyopita ya ligi, ikiwa imetoka sare tano na kupoteza minne. Huo ndiyo mfululizo wake mrefu zaidi wa kutopata ushindi katika historia ya michuano hiyo.


EP 03

ASTON VILLA VS IPSWICH TOWN

Mchezo wa mwisho wa leo Jumamosi utaikutanisha Aston Villa na Ipswich Town, huku Villa ikitaka kumaliza mfululizo wa kutoka sare katika mechi zake tatu zilizopita za ligi, ambapo haijawahi kutoka sare katika mechi nne mfululizo za Ligi Kuu England tangu Agosti na Septemba mwaka 2011. Mechi hiyo inapewa uwezekano wa asilimia 25.5 kumalizika kwa sare.

Kwa upande mwingine Villa haijapoteza katika mechi zote 22 za ligi dhidi ya timu zilizopanda daraja chini ya kocha Unai Emery ikishinda 15 na sare saba. Pia, mchezo huo utakuwa wa kihistoria kwa Aston Villa, kwani utakuwa wa 5,000 kwa klabu hiyo katika madaraja manne ya juu ya soka la England na katika mechi 4,999 zilizopita imeshinda 2,050, sare 1,199 na kupoteza 1,750.


KESHO JUMAPILI


EP 04

EVERTON VS LIVERPOOL

Dabi ya Merseyside ndiyo itakayofungua ratiba ya kesho Jumapili, huku Everton ikiwa na dhamira ya kurejea baada ya kufungwa mabao 4-0 katika mchezo uliopita itakapokutana na wapinzani wake, Liverpool.

Katika mchezo kesho uwezekano wa kutokea kwa kadi nyingine nyekundu hauwezi kupuuzwa, kwani pambano hilo limekuwa na wachezaji wengi zaidi walioonyeshwa kadi nyekundu kuliko mchezo mwingine wowote katika historia ya Ligi Kuu England, likiwa na jumla ya kutolewa kwa wachezaji 25.

Rekodi ya Everton dhidi ya Liverpool si nzuri. Imeshinda mechi mbili pekee kati ya 31 zilizopita za ligi kuu dhidi ya wapinzani hao, huku ikitoka sare 14 na kupoteza 15. Pia, Everton imewahi kuruhusu mabao sita ya ushindi kufungwa dhidi yake katika dakika ya 90, yakiwamo yale ya mchezo huo msimu uliopita, wakati Virgil van Dijk alipofunga bao la ushindi.

Liverpool, ambayo iliifunga Club Brugge mabao 3-0 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano, imepoteza mchezo mmoja pekee kati ya mechi 15 za mwisho za Ligi Kuu England ilizocheza ugenini dhidi ya Everton. Hata hivyo, mechi 10 kati ya hizo zilimalizika kwa sare. Na leo, Liverpool ndiyo inayopewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda, ikiwa na asilimia 42.7 huku Everton ikipewa asilimia 32, ilhali sare ikiwa 25.3.


EP 05

BRIGHTON VS NEWCASTLE

Brighton, ambayo inapewa asilimia 56.3 kushinda, ilishindwa kufunga bao kwa mara ya pili pekee msimu huu katika mchezo wake uliopita. Sasa itakuwa inalenga kuimarisha nafasi yake ya pili kwenye msimamo wa ligi itakapokutana na Newcastle United, ambayo inapewa nafasi ya asilimia 21.1 ya kushinda.

Brighton haijapoteza katika mechi zote tisa za nyumbani za Ligi Kuu England dhidi ya Newcastle, ikiwa imeshinda nne na sare tano. Katika historia ya michuano hiyo, hakuna timu ambayo Brighton imekutana nayo mara nyingi zaidi nyumbani bila kupoteza, kama ilivyo Newcastle.

Newcastle iliyotoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Arsenal Jumamosi iliyopita, haijashinda katika mechi 39 za mwisho za Ligi Kuu England ilizocheza ugenini dhidi ya timu zilizokuwa zikianza siku zikiwa katika nafasi mbili za juu kwenye msimamo. Katika mechi hizo, imetoka sare tano na kupoteza 34. Kazi yake haitakuwa rahisi pia kutokana na rekodi ya Brighton ya kuruhusu mabao machache zaidi nyumbani msimu huu, ikiwa imefungwa moja pekee.


EP 06

PALACE VS HULL CITY

Ushindi wa Hull City dhidi ya Brighton katika mchezo uliopita ulihitimisha mfululizo wa mechi nane bila ushindi katika Ligi Kuu England na kwa upande mwingine, Crystal Palace imepoteza mechi zake tano zilizopita. Msimu huu ndiye kipa aliyeokoa mara nyingi zaidi, akiwa na sevu 48, huku pia akiwa na asilimia kubwa zaidi ya kuokoa mashuti, akiwa na asilimia 81.4. Hata hivyo, huenda akahitaji kuonyesha kiwango bora zaidi katika mchezo ujao.

Hull imeshinda mchezo mmoja pekee kati ya mechi zake 13 za mwisho ilizocheza ugenini dhidi ya Palace katika mashindano yote, huku ikitoka sare tano na kupoteza saba. Kwa mchezo huo, Hull inapewa asilimia 31 kushinda katika Uwanja wa Selhurst Park.

Palace inapitia kipindi kigumu zaidi cha kupoteza mechi mfululizo tangu Juni na Julai 2020, ilipofikisha vipigo saba mfululizo. Hata hivyo, inapewa asilimia 42.3 ya kupata ushindi dhidi ya Hull.


EP 09

FULHAM VS BOURNEMOUTH

Mfululizo wa ushindi wa mechi tano wa Bournemouth katika Ligi Kuu England umeifanya kusogea karibu na nafasi nne za juu. Hata hivyo, Fulham nayo imekuwa katika kiwango kizuri, ikiwa haijapoteza katika mechi tano zilizopita. Pamoja na hali hiyo, Bournemouth ndiyo inayotabiriwa kuongeza mfululizo wake wa ushindi. Kiwango kizuri cha timu hiyo kimeenda sambamba na kiwango bora cha mshambuliaji wake, Evanilson, ambapo amehusika katika mabao mengi zaidi kuliko mchezaji mwingine yeyote katika Ligi Kuu England msimu huu akifunga sita na asisti nne. Pia amefunga katika mechi sita mfululizo. Bournemouth inapewa asilimia 41 ya kushinda mchezo huo.

Kwa mchezo huo, Fulham inapewa asilimia 33.4 ya ushindi wake wa kwanza wa aina hiyo tangu Februari 2024.


EP 07

SUNDERLAND VS SPURS

Tottenham Hotspur imefurahia kupanda katika msimamo wa ligi baada ya kushinda mechi nne kati ya tano zilizopita za Ligi Kuu England, huku ikipoteza mchezo mmoja. Idadi hiyo ya ushindi ni kubwa kuliko ile ilioupata katika mechi 26 za kwanza za mwaka 2026 kwa pamoja, ambapo ilishinda tatu, sare 10 na kupoteza 13.

Na sasa kocha Roberto De Zerbi atarejea katika uwanja ambao alicheza mchezo wake wa kwanza akiwa kocha wa Tottenham, timu yake itakapokutana na Sunderland ambayo imeondoka katika nafasi za mwisho za msimamo wa ligi baada ya kuepuka vipigo katika mechi mbili zilizopita.

Ushindi wa Sunderland wa bao 1-0 katika mchezo huu Aprili 12 ulihitimisha mfululizo wa mechi 15 bila ushindi dhidi ya Tottenham katika ligi, ikiwa imetoka sare tano na kupoteza 10. Hata hivyo, tangu mchezo huo, ni timu sita pekee zilizokusanya pointi nyingi zaidi katika ligi kuliko Spurs ambayo imefikisha pointi 26 inayopewa pia nafasi kubwa zaidi ya kushinda mchezo huo kwa asilimia 39.3, huku Sunderland ikiwa na 34.8.


EP 08

ARSENAL VS MAN CITY

Macho yote yataelekezwa katika Uwanja wa Emirates, ambako vinara wa ligi hiyo, Arsenal, watakabiliana na Manchester City, ambayo imekuwa na kiwango kisichoridhisha hivi karibuni. Hiyo itakuwa mara ya pili kwa timu hizo kukutana msimu huu, ambapo Arsenal ilishinda kwa mabao 3-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamii mwezi Agosti. Hata hivyo, mengi yamebadilika tangu wakati huo.

Arsenal inaongoza Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi sita, wakati Manchester City haijashinda katika mechi nne zilizopita za ligi, ikiwa imetoka sare moja na kupoteza tatu. Timu zote mbili zilitoka sare katika michezo yao ya katikati ya wiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Arsenal ililazimika kuridhika na sare ya bao 1-1 dhidi ya Borussia Dortmund, huku kushindwa kutumia vizuri nafasi za kufunga kukiigharimu. Kwa upande mwingine, Manchester City ililazimika kusawazisha mara mbili kabla ya kutoka sare dhidi ya Napoli.

Arsenal haijapoteza katika mechi zake tatu za mwisho za nyumbani dhidi ya City, ikiwa imeshinda mbili na kutoka sare moja. Kutokana na rekodi hiyo inapewa nafasi kubwa ya kushinda, ikiwa na asilimia 54.5, huku Manchester City ikipewa asilimia 22.1.

Rekodi zinaonyesha City imeshinda mchezo mmoja kati ya sita iliyopita ya Ligi Kuu England dhidi ya Arsenal, huku ikitoka sare tatu na kupoteza miwili. Ushindi huo mmoja ulipatikana katika mchezo wa mwisho Aprili, ilipoifunga Arsenal mabao 2-1 katika Uwanja wa Etihad.

Hata hivyo, City imekuwa na rekodi nzuri dhidi ya timu zinazotetea ubingwa wa Ligi Kuu England ikiwa imeshinda mechi 12 kati ya 14 za mwisho dhidi ya mabingwa watetezi huku ikitoka sare moja na kupoteza moja.

Lakini, tangu wiki ya nane ya msimu huu, ni Crystal Palace pekee ambayo imekusanya pointi chache kuliko Manchester City ambayo imepata pointi moja. Kwa upande mwingine, Arsenal ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza pointi yoyote katika mechi za nyumbani za ligi hiyo msimu huu, ikiwa imeshinda michezo yote mitano iliyocheza katika Uwanja wa Emirates.