West Ham yamfungia kazi Endrik, Valencia, Sociedad zaingilia kati
Muktasari:
- Staa huyu,19, anahusishwa kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kutosha kikosi cha kwanza cha Madrid.
WEST Ham inataka kumsajili straika wa Real Madrid, Endrick kwa mkopo wa nusu msimu dirisha lijalo la majira ya baridi lakini inakumbana na ushindani kutoka kwa Valencia na Real Sociedad ambazo pia zinahitaji huduma yake.
Staa huyu,19, anahusishwa kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kutosha kikosi cha kwanza cha Madrid.
Mkataba wa sasa wa Endrick unatarajiwa kumalizika mwaka 2030 na tangu kuanza kwa msimu huu hajacheza hata mechi moja ingawa mara zote anaonekana kuwa benchi.
Inaelezwa kocha wa Xabi Alonso haoni kama staa huyu anaendana na mfumo wake, pia kuongezeka kwake uzito hivi karibuni kunachangia sana kwa kocha huyo kuona hamfai.
West Ham ambayo imekuwa na wakati mgumu tangu kuanza kwa msimu huu inataka kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha inaipata saini ya staa huyu ikiamini anaweza kwenda kuongeza kitu katika eneo lao la ushambuliaji linalopata tabu kwa sasa.
Marc Guehi
CHELSEA haina mpango wa kumsajili beki kisiki wa Crystal Palace na timu ya taifa ya England, Marc Guehi, 25, licha ya kuwa mkataba wake kutarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu. Mabosi wa Chelsea wameachana na mpango huo kutokana na ushindani mkali uliopo kwa timu nyingine ambazo pia zinamhitaji. Chelsea inaona itatakiwa kumlipa mshahara mkubwa ili kumshawishi ajiunge nao kwa sababu timu nyingine zinazomhitaji pia zimemweka mshahara mnono.
Antoine Semenyo
CHELSEA imeonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa Bournemouth na timu ya taifa ya Ghana, Antoine Semenyo, 25, dirisha lijalo la majira baridi au kiangazi na ipo tayari kulipa takribani Pauni 78 milioni kama ada yake ya uhamisho. Tangu kuanza kwa msimu huu, Semenyo amecheza mechi nane za michuano yote na kufunga mabao sita. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030 na kuna uwezekano akaondoka kusaka changamoto mpya.
Kenan Yildiz
JUVENTUS imeripotiwa kukataa ofa ya takribani Pauni 58 milioni kutoka kwa Chelsea inayohitaji saini ya staa wao wa kimataifa wa Uturuki, Kenan Yildiz dirisha lijalo. Chelsea imekuwa ikihitaji sana saini ya fundi huyu kutokana na kiwango chake na inaamini akitua katika timu yao ataenda kuboresha eneo lao la ushambuliaji. Staa huyu mwenye umri wa miaka 20, mkataba wake na Juventus unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.
Joshua Zirkzee
MSHAMBULIAJI wa Manchester United ambaye hapati nafasi ya kucheza katika kikosi hicho Joshua Zirkzee, 24, anafikiria kuendelea kusalia Ligi Kuu England ikiwa ataondoka OId Trafford mwisho wa msimu huu. Zirkzee ni miongoni mwa mastaa ambao Kocha Ruben Amorim haonekani kuwaamini katika mifumo yake na alitamani kuondoka dirisha lililopita hata kwa mkopo lakini ilishindikana. Mkataba wake unamalizika 2029.
Ronald Araujo
BEKI kisiki wa Barcelona, Ronald Araujo, 26, huenda akauzwa katika dirisha lijalo la majira ya baridi kwa Pauni 35 milioni. Staa huyu alikiwa akiwindwa na vigogo wengi tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi lakini aligoma kuondoka. Miongoni mwa timu zinazohitaji huduma yake ni pamoja na Chelsea, Liverpool, Tottenham na Juventus. Mkataba wa sasa wa Araujo unatarajiwa kumalizika mwaka 2031.
Bukayo Saka
ARSENAL ina matumaini makubwa ya kumalizana na staa wao Bukayo Saka kipindi hiki cha mapumziko ya wiki ya kimataifa. Mkataba wa sasa wa Saka unamalizika 2027 na inaelezwa Arsenal tayari imeshafikia naye makubaliano ya mkataba mpya lakini hadi sasa bado hajasaini. Msimu huu amecheza mechi saba za michuano yote na kufunga mabao matatu.
Ibrahima Konate
LIVERPOOL ipo katika mazungumzo na wakala wa beki wao kisiki, Ibrahima Konate, 26, ili kumsainisha mkataba mpya wakati ule wa sasa ukitarajiwa kumalizika mwaka 2027. Mabosi wa Liverpool wanataka kumsainisha beki huyu mkataba mpya baada ya kuona Real Madrid inainyemelea huduma yake. Tangu kuanza kwa msimu huu Konate amecheza mechi 10 za michuano yote.