Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watatoka? Man City, Liverpool kama zamani tu!

Muktasari:

  • Achana na mechi mbili za kwanza, mchezo kati ya Liverpool na Manchester City unatarajiwa kuwa mkali na kuibua kumbukumbu fulani za nyuma za wababe hao waounda Top Four ya ligi hiyo kwa miaka mingi.

LIVERPOOL, ENGLAND: LIGI Kuu England inaendelea leo kwa michezo mitatu; Crystal Palace ikiikaribisha Nottingham Forest katika mchezo wa mapema saa 10:00 jioni, huku Hull City ikiwa mwenyeji wa Everton muda huohuo ilhali Liverpool itakuwa nyumbani ikiwaalika Manchester City saa 12:30 jioni.

Achana na mechi mbili za kwanza, mchezo kati ya Liverpool na Manchester City unatarajiwa kuwa mkali na kuibua kumbukumbu fulani za nyuma za wababe hao waounda Top Four ya ligi hiyo kwa miaka mingi.

Siku zote Man City inapokwenda katika Dimba la Anfielf huwa inapokewa kwa hisia kali na mashabiki wa Liverpool lakini wikendi hii mashabiki wa Liverpool huenda wakawa na hisia zaidi kuliko kawaida. Kutokana na yote yaliyotokea katika wiki chache zilizopita juu ya mustakabali wa kikosi hicho, wachezaji wa Man City wanaweza kutamani kurejea uwanjani bila kuvuta hisia za watu wengi.

Hata hivyo, badala ya kurejea moja kwa moja katika utulivu uwanjani Etihad, wanakabiliwa na mechi inayoweza kuwa ya kutisha zaidi, kwenda Anfield, uwanja wenye mazingira magumu kwa timu pinzani.


ILE KASHFA NA MAMBO UWANJANI

Wachezaji hao pamoja na kocha wao mpya, Enzo Maresca, wamejikuta katikati ya moja ya kashfa kubwa zaidi kuwahi kutokea katika michezo England, baada ya tume huru kuikuta City na hatia ya mashtaka yote yanayohusiana na ukiukaji wa kanuni za kifedha za ligi hiyo kati ya misimu ya 2009/10 na 2017/18, pamoja na mashtaka mengi yanayohusu kushindwa kushirikiana na uongozi wa ligi katika uchunguzi wake. City imekanusha tuhuma zote na imekata rufaa dhidi ya mashtaka hayo.

Hata hivyo, baada ya uamuzi huo, City inatarajiwa kukabiliwa na ukosoaji mkubwa ambao hautaweza kuepukika. Klabu nyingine nyingi na mashabiki wake wanaamini kuwa walikosa mataji, zawadi za fedha, nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, fursa za kusajili wachezaji na mafanikio mengine kwa faida ya klabu iliyopatikana na hatia ya kufanya mambo kinyume na kanuni ambazo wao walizifuata na zilizowawekea vikwazo.

Liverpool inaamini kuwa ni miongoni mwa klabu zenye sababu kubwa zaidi za kuhisi zilionewa baada ya kuukosa ubingwa mbele ya City msimu wa 2013/14 na Kombe la Ligi 2015/16. Katika kipindi cha 2009 hadi 2018 ambacho City inakabiliwa na mashtaka, ingawa hakuna tuhuma za udanganyifu zilizotajwa, Liverpool pia ilimaliza nyuma ya City 2018/19 na 2021/22, ikiwa na pointi nyingi sana, 97 na 92 mtawalia.

Kwa miaka mingi, mashabiki wa Liverpool wamekosa furaha ya mafanikio kutokana na City, hivyo huenda wakawa na kinyongo dhidi yao.


ANFIELD PAGUMU

Uwanja wa Anfield umekuwa ukijulikana kwa muda mrefu kuwa mgumu kwa timu ngeni, na sehemu ya ugumu huo inatokana na mazingira yanayotengenezwa na mashabiki. Mara nyingi mashabiki wa Liverpool hutajwa kuwa miongoni mwa wenye sauti kubwa zaidi duniani, huku mazingira ya uwanja huo yakihesabiwa kuwa miongoni mwa bora zaidi.

Akizungumza na BBC Sport 2021, beki wa zamani wa Manchester City, Micah Richards, alisema: “Unapokuwa unacheza, unajiamini, lakini unapokwenda Anfield unahisi kana kwamba miguu yako imegeuzwa nyuma. Huwezi kupiga hata pasi rahisi. Ni kama ngome. Sina kumbukumbu nzuri kuhusu Liverpool. Walikuwa wazuri sana.”

Mwaka 2020, jarida la France Football liliuweka Anfield katika nafasi ya pili duniani, nyuma ya uwanja wa Bombonera wa Boca Juniors, katika orodha ya viwanja vyenye mazingira bora zaidi ya mashabiki katika soka.

Msimu wa Ligi Kuu England  wa 2020/21 ulioathiriwa na janga la corona ulionyesha jinsi mashabiki nyumbani wanavyoweza kuleta tofauti, jambo lililoonekana pia katika matokeo ya Liverpool.


NAMBA ZINAONGEA

Ingawa Liverpool imekuwa timu nzuri kwa miaka mingi, haijawa bora kuliko timu zote katika sehemu kubwa ya historia ya ligi hiyo. Hata hivyo, timu ngeni zina asilimia 12.5 pekee ya ushindi katika Uwanja wa Anfield, kiwango cha chini zaidi kuwahi kurekodiwa katika uwanja wowote kwenye ligi hiyo. Liverpool imepoteza mechi 82 tu kati ya 654 ilizocheza hapo katika mashindano hayo, huku timu ngeni zikipata wastani wa pointi 0.62 kwa kila mchezo.

Timu nyingi zimekuwa zikiteseka Anfield. Newcastle United imeshinda mchezo mmoja tu na kupoteza 25 kati ya mechi 31 za Ligi Kuu England ilizocheza hapo, ikiwa na kiwango cha vipigo cha asilimia 80.6. West Ham United imeshinda mchezo mmoja tu kati ya 30, huku Tottenham Hotspur ikishinda mara mbili pekee kati ya mechi 34. Timu sita zimepoteza kila mchezo wa ugenini dhidi ya Liverpool katika ligi hiyo.

Mchezo wa leo, Jumapili, utakuwa mgumu kwa City hata bila matukio ya hivi karibuni. Ratiba ya msimu ilipotangazwa wakati wa kiangazi, Maresca aliutazama kama mchezo muhimu dhidi ya mpinzani anayeweza kuwa mshindani wa ubingwa au, angalau, mtihani mkubwa kwa City  kutwaa taji. Hii ni kwa sababu City, kama timu nyingine nyingi ina rekodi mbaya Anfield. Ingawa siyo mbaya kama timu zilizotajwa hapo juu, bado siyo nzuri na haitoi matumaini makubwa kabla ya mchezo huo.

Katika viwanja ambavyo City imecheza zaidi ya mara moja, wastani wake wa pointi kwa kila mchezo ni mbaya zaidi Highbury, kwa pointi 0.22, kuliko Anfield ambako ina wastani wa pointi 0.59. Hata hivyo, City imecheza Anfield mara 29, zaidi ya mara tatu ya mechi tisa ilizocheza katika uwanja wa zamani wa Arsenal, Highbury. Pia, City ilicheza Highbury wakati haikuwa timu yenye kiwango kizuri, tofauti na mechi zake za Anfield ambazo zimehusisha kipindi chote cha umiliki wa Sheikh Mansour.

Kwa ujumla, City imeshinda mechi tatu tu kati ya 29 za ligi hiyo ilizocheza Anfield, kiwango cha ushindi cha asilimia 10.3, ambacho ni miongoni mwa viwango vyake vibaya zaidi katika viwanja vyote. Pia imepoteza mechi 18 hapo, ikiwa na kiwango cha vipigo cha asilimia 62.1.

Hata hivyo, City ilishinda Anfield msimu uliopita, ikifunga mabao mawili ya dakika za mwisho na kupata ushindi wa 2-1 baada ya kuwa nyuma. Lakini, ushindi huo ulipatikana wakati Liverpool ikiwa katika kipindi kigumu, ikiwa imeshinda mchezo mmoja tu kati ya saba na kampeni yake ya kutetea ubingwa ilikuwa imepoteza mwelekeo.

City pia ilishinda Anfield Februari 2021, katika msimu wa corona ambao mechi zilichezwa bila mashabiki uwanjani. Ulikuwa ushindi wake wa kwanza hapo katika safari 18. Ni wazi kuwa City, kama timu nyingine nyingi hupata shida kucheza Anfield, hasa mashabiki wanapokuwepo.

Na sasa wikendi hii unaongezea hali hiyo na ukweli kwamba huu utakuwa mchezo wa kwanza wa City tangu kutangazwa kwa uamuzi wa tume huru kuikuta na hatia. Hilo linaifanya mechi kuwa changamoto kubwa kwa wachezaji na benchi la ufundi la klabu hiyo.

Hakuna tuhuma za makosa dhidi ya wachezaji wanaoweza kucheza Jumapili, ambao wengi wao hawakuwa klabuni kati ya 2009 na 2018. Hali kadhalika, Maresca, aliyefanya kazi katika timu za vijana za City kuanzia 2020 hadi 2021 na kuwa msaidizi wa Pep Guardiola katika msimu wa 2022/23 ambao City ilishinda mataji matatu, hakuwa klabuni katika kipindi kinachohusika.

Hata hivyo, wao ndio watakaokabiliana moja kwa moja na mashabiki wa Liverpool. Watalazimika kuvumilia kutoridhika kwa wale wanaoamini kuwa City haikufuata kanuni. Pia watalazimika kucheza katika uwanja wenye mojawapo ya mazingira bora zaidi duniani, ambako City ina rekodi mbaya, huku wakikabiliana na mashabiki ambao tayari watakuwa miongoni mwa wenye uhasama mkubwa zaidi watakaokutana nao msimu huu, hata kama matukio hayo yasingetokea. Changamoto ambayo tayari ilikuwa kubwa sasa itakuwa ngumu zaidi wikendi hii. Mwanzo mzuri wa City wa kushinda mechi zote uko katika mtego mkubwa.