MVP NBA anunua chake Atletico
Muktasari:
- Mchezaji huyo aliyeshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa NBA (MVP) mara mbili anageuza mkataba wake mkubwa wa kucheza mpira wa kikapu kuwa uwekezaji katika michezo nje ya Marekani.
MADRID, HISPANIA: SUPASTAA wa Oklahoma City Thunder na Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), msimu uliopita Shai Gilgeous-Alexander maarufu kama SGA amechagua klabu ya soka ya kuwekeza na ni moja ya vigogo nchini Hispania; Atletico Madrid.
Mchezaji huyo aliyeshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa NBA (MVP) mara mbili anageuza mkataba wake mkubwa wa kucheza mpira wa kikapu kuwa uwekezaji katika michezo nje ya Marekani.
Hilo ni jambo la kawaida kwa wanamichezo wa kulipwa kuwa wamiliki wa hisa za sehemu katika timu za michezo baada ya kumaliza maisha yao ya kucheza. Hata hivyo, Shai hakuona sababu ya kusubiri, kwani tayari amechagua klabu ya soka atakayowekeza fedha zake. Mchezaji huyo ambaye aliwahi kushiriki katika mchezo wa NBA All-Star kwa misimu minne mfululizo, alisaini mkataba mpya wa kuongeza muda wa kuitumikia Oklahoma City Thunder wenye thamani ya Dola 285 milioni mwakajana.
Dili hilo lilikuwa baada ya kupata nyongeza ya mkataba wake wa awali wa kiwango cha mchezaji anayeanza kucheza NBA (rookie extension), wenye thamani ya Dola 172 milioni, miaka minne iliyotangulia. Pia amekuwa na mikataba ya udhamini na kampuni za Converse na sasa Nike.
Kwa sasa SGA anatarajiwa kutumia sehemu ya fedha alizopata kuwekeza Atletico Madrid, mojawapo ya klabu zinazotambulika katika soka la duniani, ikiwa na mashabiki kibao nchini Hispania.
Ingawa siyo maarufu kwa mashabiki wa kawaida kama Real Madrid au Barcelona, klabu hiyo inayofahamika kwa jina la utani la “Atleti” inachukuliwa kuwa ya tatu kwa ukubwa nchini humo. Hadi jana Atletico Madrid ilikuwa inashika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Hispania (LaLiga), mbele ya Real Betis na Real Madrid.
Akizungumzia suala la kuamua kuwekeza katika klabu hiyo, Shai alikaririwa akisema: “Nina furaha kujiunga rasmi na kundi la wamiliki wa Atletico Madrid. Hii ni klabu ambayo imekuwepo muda mrefu katika kilele cha soka la Ulaya, na ninashukuru kupata fursa ya kuwa sehemu ya mustakabali wake.”
Kwa upande wake, Atletico Madrid pia ilitoa taarifa ikisema: “Mshindi wa tuzo ya MVP wa NBA kwa misimu miwili mfululizo na bingwa wa NBA anajiunga na kundi la wamiliki wa klabu, akiendeleza mapenzi yake kwa Atletico Madrid ambayo tayari ameyaonyesha kwa kuvaa jezi za rangi nyekundu na nyeupe kabla ya tangazo hili rasmi.”