Simba yafuta uteja ikiitandika Yanga 2-1
Muktasari:
- Timu hizo zimekutana tena tangu mara ya mwisho zilipokutana katika mechi ya Ngao ya Jamii, iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani, Zanzibar, Agosti 12, 2026 na Yanga kushinda kwa bao 1-0, la Albert Kangwanda dakika ya 31.
KISASI NI HAKI! ndivyo unavyoweza kusema baada ya Simba kuvunja uteja wa muda mrefu wa Yanga kwa kuifunga leo mabao 2-1, katika mechi ya Kariakoo Derby, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini, Dar es Salaam.
Timu hizo zimekutana tena tangu mara ya mwisho zilipokutana katika mechi ya Ngao ya Jamii, iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani, Zanzibar, Agosti 12, 2026 na Yanga kushinda kwa bao 1-0, la Albert Kangwanda dakika ya 31.
Katika mechi ya leo ya raundi ya saba kwa timu hizo katika Ligi Kuu Bara, msimu huu wa 2026-2027, ilianza kwa Yanga kupata bao la mapema dakika ya tano tu, lililofungwa na mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, raia wa Namibia, Peter Shalulile.
Shalulile alifunga bao hilo baada ya kazi nzuri iliyofanywa na kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Maxi Mpia Nzengeli na mfungaji huyo kutumia vyema makosa ya safu ya kujilinda yaliyofanywa na mabeki wa Simba.
Mechi hiyo ilianza kwa timu zote kucheza kwa tahadhari ya hali ya juu, ingawa Yanga ilionekana bora zaidi hasa dakika 10, zilizosababisha upatikanaji wa bao la mapema, ambalo liliiamsha Simba na kuanza kutengeneza mashambulizi ya haraka ya kutafuta kusawazisha, japo yaliipa faida mabingwa watetezi kwenda hadi mapumziko ikiwa tayari inaongoza.
DUKE ATIBUA HESABU
Kuumia kwa kiungo mkabaji wa Yanga, Mkenya Duke Abuya dakika ya 24, kulitibua hesabu za kikosi hicho, kwani kutoka kwake iliipa faida Simba ya kumiliki mpira na kutengeneza mashambulizi ya mara kwa mara.
Mabadiliko hayo ya kuumia kwa Duke na nafasi yake kuchukuliwa na Fred Ngoma, yalionyesha upungufu kwa Yanga katika eneo la kiungo na kuipa Simba wigo mpana wa kushambulia zaidi kuanzia katikati ya uwanjani.
SIMBA YAJIBU MAPIGO
Kipindi cha pili Simba ilirejea kwa kasi ya kutafuta nafasi ya kusawazisha bao hilo na dakika 68, kupitia kwa kiungo mshambuliaji wa kikosi hicho, Neo Maema na kurejesha matumaini ya timu hiyo na mashabiki kiujumla.
Bao hilo lilitokana na mashambulizi ya mara kwa mara yaliyokuwa yakielekezwa katika lango la Yanga, ambayo kipindi cha pili ilicheza zaidi kuzuia na kushambulia kwa kushtukiza.
Mashambulizi hayo ya Simba, yalikuwa mwiba kwa Yanga, kwa sababu dakika ya 72, Elie Mpanzu aliiandikia timu hiyo bao la pili na la ushindi lililozidi kuamsha morali ya kikosi hicho, iliyokuwa ikicheza kwa lengo la kuvunja uteja wa muda mrefu.
Mabadiliko yaliyofanywa na Kocha Mkuu wa Simba, Stever Barker ya kumtoa Clatous Chama na kumuingiza Keletso Makgalwa dakika ya 65, ndiyo yaliyochangia zaidi kutengeneza mashambulizi, jambo lililoonyesha wazi Yanga kuzidiwa kwa kiwango kikubwa.
SIMBA YAVUNJA UTEJA
Ushindi wa Simba umeifanya kuvunja uteja wa muda mrefu kwa Yanga, kwani kabla ya hapo mara ya mwisho kushinda katika Ligi Kuu Bara ilikuwa, Aprili 16, 2023, ambao ni miaka mitatu iliyopita.
Kuanzia, Aprili 16, 2023, Simba ilipoifunga Yanga mabao 2-0, katika mechi ya 110, kwa timu hizo kukutana kwenye Ligi Kuu Bara tangu, mwaka 1965, yaliyofungwa na Henock Inonga dakika ya 2 na Kibu Denis dakika ya 32, ilikuwa haijashinda tena hadi jana.
Tangu, Aprili 16, 2023, Simba ilipoifunga Yanga katika mechi ya Ligi Kuu hadi jana Oktoba 10, 2026, imefikisha jumla ya siku 1,273, sawa na miaka mitatu, miezi mitano na siku 24, jambo ambalo imevunja uteja huo.
KIPIGO CHA KWANZA YANGA
Kipigo cha Yanga kinakuwa ni cha kwanza kwa timu hiyo msimu huu katika Ligi Kuu Bara, baada ya kushinda mechi sita za mwanzoni ilizocheza na kukusanya pointi 18, huku ikiwaacha wapinzani wao Simba kushinda mechi ya saba mfululizo na kuongoza kwa kukusanya pointi 21.
SIMBA YAENDELEZA REKODIUshindi wa Simba umeifanya timu hiyo kuendeleza rekodi nzuri ya kutopoteza mechi yoyote ya Ligi Kuu, tangu mara ya mwisho ilipochapwa mabao 2-0, dhidi ya Azam FC, Desemba 7, 2025, ambao ni ya msimu wa 2025-2026.
Tangu ilipochapwa mabao hayo ya Jephte Kitambala dakika ya 81 na Idd Seleman 'Nado' dakika ya 88, Simba imecheza jumla ya mechi 32, za Ligi Kuu bila kupoteza, baada ya kushinda 25 na kutoka sare saba, huku ikifunga mabao 56 na kuruhusu 11.
VIKOSI VILIVYOANZA
SIMBA:
Djibrilla Kassali, Nathaniel Chilambo, Anthony Mligo, Ismael Olivier Toure, Rushine De Reuck, Yusuph Kagoma, Neo Maema, Libasse Gueye, Elie Mpanzu, Clatous Chama, Alain Anicet Oura.
YANGA:
Djigui Diarra, Yao Kouassi Attohoula, Chadrack Boka, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Hamad 'Bacca', Maxi Mpia Nzengeli, Mudathir Yahya, Duke Abuya, Albert Kangwanda, Housseine Zakouani, Peter Shalulile.