Wakala wa Isak afunguka hatma ya Staa huyo Newcastle
Muktasari:
- Staa huyo kipenzi cha St James’ Park, amekuwa kwenye mipango ya Liverpool na timu ya Saudi Pro League, Al Hilal zikihitaji saini yake kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi na kumfanya akose mechi ya kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Celtic.
NEWCASTLE, ENGLAND: WAKALA wa straika, Alexander Isak amefichua kwamba staa huyo wa Newcastle United yupo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha hatima mpya ya maisha yake baada ya uvumi mwingi kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Staa huyo kipenzi cha St James’ Park, amekuwa kwenye mipango ya Liverpool na timu ya Saudi Pro League, Al Hilal zikihitaji saini yake kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi na kumfanya akose mechi ya kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Celtic.
Newcastle inataka Pauni 120 milioni kumuachia staa huyo, ambaye alifunga mabao 27 kwenye michuano yote aliyotumikia kikosi hicho cha Eddie Howe msimu uliopita.
Wiki iliyopita, Newcastle iliripotiwa kwamba haimuuzi Isak, hata kama mchezaji huyo alitaka kuzungumzia dili hilo ambalo litamfanya avunje rekodi ya uhamisho huko Uingereza. Na sasa, wakala wake anafichua kwamba kila kitu kinatazamwa vyema kwenye dirisha hili na kitakamilika muda wowote.
Wakala Gonzalo Gaitan aliliambia gazeti la Saudi Arabia, Arriyadiyah kuwa: “Tunapitia na kufanyia uchambuzi mambo yote na kila kitu kipo kwenye hatua za mwisho kukamilika. Tutaeleza kila kitu kama Isak ataondoka au atabaki Newcastle.”
Liverpool matumaini ya kunasa saini ya Isak yalikuwa makubwa baada ya staa huyo wa Sweden kushindwa kupewa ofa ya dili jipya kwenye klabu yake ya sasa.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu England wameifanyia umafia pia Newcastle kwa kuvamia kwenye mawindo yao ya straika Hugo Ekitike kutoka Frankfurt na muda wowote anaweza kutua kwenye kikosi cha miamba hiyo ya Anfield.
Kama Isak atatua Anfield, uhamisho wake unaweza kuvunja rekodi huko Uingereza, ambayo inashikiliwa na Florian Wirtz, aliyesajiliwa na Liverpool kwa ada ya Pauni 116 milioni kwenye dirisha hili.