Carragher: Piga benchi Wirtz
Muktasari:
- Nyota huyo wa Ujerumani alijiunga na Liverpool kwa ada ya pauni 116 milioni, lakini amekuwa akipitia wakati mgumu tangu alipoanza maisha yake ndani ya Ligi Kuu England.
MANCHESTER, ENGLAND: MANENO makali yameelekezwa kwa kiungo mshambuliaji wa Liverpool, Florian Wirtz, baada ya gwiji wa klabu hiyo, Jamie Carragher, kutaka mchezaji huyo akae benchi kufuatia kiwango chake kisichoridhisha dhidi ya Manchester City.
Carragher, ambaye ni beki wa zamani wa Liverpool na mchambuzi wa soka wa Sky Sports, amesema Wirtz hajafanya vya kutosha kuendelea kupewa nafasi katika kikosi cha kwanza cha mabingwa hao wa England.
Nyota huyo wa Ujerumani alijiunga na Liverpool kwa ada ya pauni 116 milioni, lakini amekuwa akipitia wakati mgumu tangu alipoanza maisha yake ndani ya Ligi Kuu England.
Ingawa msimu wake wa kwanza alipewa nafasi ya kuwa kipindi cha kuzoea ligi hiyo, kiwango chake kimeendelea kuibua maswali, huku akishindwa kufunga bao na kutoa asisti moja pekee katika mechi sita za ligi zilizokuwa zimechezwa msimu huu.
Akizungumza kupitia Sky Sports, baada ya mchezo dhidi ya Manchester City Jumapili, Carragher amesema Liverpool inahitaji mchango mkubwa zaidi kutoka kwa Wirtz, hasa wakati timu inapokosa baadhi ya washambuliaji wake muhimu.
“Kwa sasa, Wirtz hafanyi vya kutosha kwa Liverpool. Amecheza mechi 55 hadi 60 akiwa na klabu hii, lakini bado hatuoni mchango tunaoutarajia,” amesema Carragher.
Ameongeza kuwa wachezaji vijana waliopata nafasi katika safu ya ushambuliaji walionyesha kiwango bora zaidi kuliko baadhi ya nyota walionunuliwa kwa fedha nyingi.
“Leo tulikuwa bila Isak na Gakpo, ambao ni miongoni mwa washambuliaji wetu bora msimu huu. Tulihitaji Wirtz apige hatua na kusaidia safu ya ushambuliaji, lakini Koumas na Munoz walikuwa bora kuliko hao wachezaji wawili wenye thamani ya zaidi ya pauni 100 milioni,” amesema.
GRAVENBERCH APEWA KIPAUMBELE
Carragher pia amemtaja kiungo Ryan Gravenberch kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wanapaswa kupewa nafasi zaidi, akisema hakuna sababu ya Wirtz kuendelea kuanza kikosi cha kwanza mbele ya Mholanzi huyo kwa kiwango cha sasa.
Gravenberch, ambaye kwa mujibu wa Carragher alianza mchezo vibaya kabla ya kuondolewa kikosini, alitajwa kuwa miongoni mwa wachezaji walioonyesha mwanga katika mchezo huo.
“Ninachokiona ni kwamba hakuna sababu Wirtz aanze mbele ya Gravenberch kwa sasa. Wirtz hapaswi kuwa katika kikosi cha kwanza cha Liverpool kwa kiwango anachoonyesha,” alisisitiza Carragher.
Hata hivyo, Wirtz tayari amecheza mechi 56 akiwa Liverpool, akifunga mabao saba na kutoa asisti 11 katika michezo hiyo, takwimu ambazo zinaonyesha amechangia mabao ya timu hiyo licha ya kukabiliwa na ukosoaji.
KLOPP ALITAJWA KAMA SULUHISHO
Katika maelezo yake, Carragher alikumbusha kuwa awali aliamini aliyekuwa kocha wa Liverpool, Jürgen Klopp, angeweza kumsaidia Wirtz kupata kiwango bora kupitia mazungumzo na kumjengea kujiamini.
Amesema Wirtz aliwahi kuonyesha kiwango kizuri alipokuwa chini ya Klopp katika mazingira ya timu ya taifa ya Ujerumani, lakini bado hajaweza kuonyesha ubora huo kwa uthabiti akiwa Liverpool.
Carragher alifafanua kuwa ukosoaji wake haujatokana na mechi chache pekee, bali idadi kubwa ya michezo ambayo Wirtz tayari ameichezea klabu hiyo.
“Hatuzungumzii baada ya mechi tano au 10. Tunazungumza baada ya mechi 50 hadi 60,” amesema.