Maresca wala hana hofu Manchester City
Muktasari:
- Kauli hiyo ya Maresca imekuja baada ya City kuichapa Liverpool mabao 3-0 katika mchezo uliowafanya kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England, wakiwa na tofauti ya pointi tatu dhidi ya timu inayowafuatia.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Manchester City, Enzo Maresca, amesema hajali muda ambao utachukuliwa na mchakato wa rufaa ya kesi inayohusisha klabu hiyo dhidi ya tuhuma 115 za ukiukwaji wa kanuni za Ligi Kuu England, akisisitiza kuwa jambo muhimu kwa sasa ni timu yake kuendelea kushinda mechi.
Kauli hiyo ya Maresca imekuja baada ya City kuichapa Liverpool mabao 3-0 katika mchezo uliowafanya kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England, wakiwa na tofauti ya pointi tatu dhidi ya timu inayowafuatia.
Maresca, ambaye alionekana kuwa na furaha baada ya ushindi huo, alieleza kuwa kelele na mijadala inayozunguka kesi ya klabu hiyo ni jambo ambalo wachezaji wanapaswa kujifunza kukabiliana nalo huku wakielekeza nguvu zao katika matokeo ya uwanjani.
“Tunajua kelele hizi zitaendelea kuwepo, hivyo tunapaswa kujifunza namna ya kukabiliana nazo. Lakini wakati huohuo, tunapaswa kutengeneza kelele zetu wenyewe, ambazo ni kushinda mechi, kama tulivyofanya leo,” amesema Maresca.
Ameongeza kuwa lengo lao ni kuhakikisha mashabiki wanaendelea kuwa na sababu za kushangilia, badala ya kuruhusu mijadala ya nje ya uwanja kuathiri mwenendo wa timu.
“Baada ya mchezo, mashabiki wetu walikuwa wakiimba. Hivyo kelele zilitoka kwetu, siyo katika mazingira yaliyotuzunguka. Tunapaswa kufanya hivyo katika kila mchezo, hasa tunapokuwa ugenini,” amesema.
MAJIBU YA MARESCA
Akizungumzia muda ambao unaweza kuchukuliwa na mchakato wa rufaa ya kesi hiyo, Maresca alisisitiza kuwa hana wasiwasi kuhusu suala hilo.
“Huwezi kufikiria jinsi nilivyo na furaha. Sijali,” amesema kocha huyo, akionyesha kuwa kwa sasa akili yake imeelekezwa katika kuhakikisha City inaendelea kufanya vizuri ndani ya uwanja.
City imekuwa ikikabiliwa na ukosoaji kutokana na tuhuma zinazohusiana na ukiukaji wa kanuni za kifedha za Ligi Kuu England. Hata hivyo, mchakato wa kisheria na rufaa yake umeendelea kuwa gumzo katika soka la England.
Maresca pia alikiri kuwa changamoto hizo zinaweza kuwaunganisha zaidi wachezaji na mashabiki, ingawa hakutaka kutoa hitimisho la moja kwa moja kuhusu athari zake kwa timu.
“Pengine ndiyo, pengine hapana. Sijui. Inaweza kutuunganisha zaidi na mashabiki wetu. Tunachoweza kufanya ni kuzingatia kushinda mechi,” amesema.
MASHABIKI WA LIVERPOOL
Kabla ya mchezo huo, kikosi cha City kilikumbana na mazingira magumu baada ya maelfu ya mashabiki wa Liverpool kujipanga kando ya barabara kuelekea Uwanja wa Anfield, wakitoa maneno ya kejeli na matusi kwa wageni hao.
Katika mchezo huo, baadhi ya mashabiki wa Liverpool pia waliwashambulia kwa maneno wachezaji wa City, wakiwataja kuwa ni wadanganyifu na kuimba nyimbo za kuwakejeli kuhusu kushuka daraja.
Hali hiyo imeongeza mjadala kuhusu namna kesi inayowakabili mabingwa hao inavyoathiri taswira ya ushindani wa Ligi Kuu England.
Kwa upande wake, kocha wa Liverpool, Andoni Iraola, amesema hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu hatma ya kesi hiyo si nzuri kwa upande wowote, lakini akasisitiza kuwa hakuna wanachoweza kufanya zaidi ya kusubiri maamuzi.
“Kutokuwa na uhakika si jambo zuri kwa mtu yeyote. Lakini ndivyo ilivyo, hatuwezi kubadilisha hali hiyo. Tunapaswa kusubiri,” amesema Iraola.
Mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland, amesema siri ya timu hiyo kuendelea kufanya vizuri katika mazingira ya presha ni kubaki imara kisaikolojia, kushikamana na kuzingatia mambo wanayoweza kuyadhibiti.
Baba yake, Alf-Inge Haaland, alikuwa miongoni mwa mashabiki wa City waliofurahia baada ya mwanaye kufunga bao la kwanza katika ushindi huo.
“Ni muhimu kubaki imara kiakili, kushikamana na kufanya mambo ambayo tunaweza kuyadhibiti. Jambo pekee tunaloweza kufanya ni kucheza soka zuri na kupambana pamoja,” amesema Haaland.