Waarabu wamwekea Victor Osimhen Sh2.6 bilioni kwa wiki

Muktasari:
- Matajiri hao wa Saudia wanaamini kuwa kiasi hicho cha pesa ni kikubwa na bila shaka Osimhen atakubali kujiunga nao.
AL-Hilal ya Saudi Arabia imeboresha ofa kwa mshambuliaji wa Napoli anayewindwa na Manchester United, Victor Osimhen, 26, ambapo imeweka mezani mshahara wa pauni 819,230 kwa wiki ambazo ni sawa na Sh2.6 bilioni.
Matajiri hao wa Saudia wanaamini kuwa kiasi hicho cha pesa ni kikubwa na bila shaka Osimhen atakubali kujiunga nao.
Awali, ilielezwa kuwa Al-Hilal ilihitaji kumsajili ili iende naye katika mashindano ya Kombe la Dunia la klabu yanayofanyika kule Marekani lakini licha ya mpango wake huo kufeli bado inatamani sana kuipata huduma yake.
Staa huyu pia anahitajika na timu kibao za England ikiwamo Arsenal na Manchester United lakini haziwezi kutoa ofa kubwa ya mshahara kiasi hicho.
Osimhen mwenyewe awali alidaiwa kuwa na mpango wa kuendelea kusalia Ulaya na kucheza soka la kiushindani lakini hakuna uhakika ikiwa atakataa ofa hiyo nono aliyowekewa mezani kwa sasa..
Ibrahima Konate
REAL Madrid inatarajia kumsajili beki wa Liverpool, Ibrahima Konate mwenye umri wa miaka 26, kwa uhamisho wa bure katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Konate ambaye mkataba wake wa na Liverpool unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu ujao Juni 30, 2026 ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Liverpool na anadaiwa kuwa katika mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya.
Ollie Watkins
MABOSI wa Arsenal wanadaiwa kuweka mpango mbadala wa usajili wa mshambuliaji katika dirisha hili ikiwa watashindwa kumpata straika wa Sporting Lisbon na timu ya taifa ya Sweden, Viktor Gyokeres, 29, kutokana na bei yake kubwa. Katika orodha ya mastaa ambao inahitaji kuwasajili, Arsenal imemweka katika rada zake mshambuliaji wa Aston Villa, Ollie Watkins, huku ikiongea pia na Benjamin Sesko wa RB Leipzig.
Alejandro Garnacho
CHELSEA, Aston Villa, na Tottenham zote zinamfuatilia winga wa Manchester United, Alejandro Garnacho 20, baada ya raia huyo wa Argentina kuambiwa atafute timu mpya katika dirisha hili.
Garnacho ambaye mkataba wake unamalizika mwaka 2028, ameambiwa atafute sehemu ya kucheza na kocha Ruben Amorim ambaye anaona haendani na mifumo yake.
Oleksandr Zinchenko
AC Milan imeanza mazungumzo na Arsenal kuhusu uwezekano wa kumsajili beki wa kimataifa wa Ukraine, Oleksandr Zinchenko, 28, katika dirisha hili.
Zincheko ni miongoni mwa mastaa walioonyeshwa mlango wa kutoka Arsenal ambayo ipo tayari kumuuza ikiwa itapatikana ofa sahihi.
Patrik Schick
INAELEZWA timu mbalimbali kutoka EPL na Serie A zimeulizia uwezekano wa kuipata huduma ya mshambuliaji wa Bayer Leverkusen na Jamhuri ya Czech, Patrik Schick, 29, katika dirisha hili.
Ripoti kutoka tovuti ya Skysports zinadai kuwa Leverkusen haitaki kumuuza staa huyo kwa sasa kwani wanaona watakuwa wanaivunja timu yao mazima kwa kuwa kuna kundi kubwa la wachezaji tayari wameshaondoka.
Ter Stegen
GALATASARAY imewasilisha ofa kwa kipa wa Barcelona, Marc-Andre ter Stegen, 33, ikihitaji kumsajili katika dirisha hili la majira ya kiangazi. Ripoti zinadai kuna uwezekano mkubwa Ter Stegen akaondoka katika dirisha hili kwa sababu tayari Barcelona imelipa pesa ya kuvunja mkataba wa kipa wa Espanyol, Joan Garcia ili ya kuziba nafasi yake.
Tyler Dibling
FC Porto ya Ureno inataka kumnunua winga wa Southampton, Tyler Dibling 19, katika dirisha hili na tayari imeshaanza mazungumzo kwa ajili ya kukamilisha dili hilo.
So’ton inaonekana kuwa haina mpango wa kumuuza ingawa mchezaji mwenyewe ndio analazimisha kuondoka ili kwenda kupata changamoto mpya sehemu nyingine.