Waamuzi wamchefua Neymar, Santos ikipokea kichapo
Muktasari:
- Tukio hilo lilitokea wakati Neymar akiiongoza Santos akiwa nahodha kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Brazil (Serie A) dhidi ya Coritiba, uliopigwa Mei 17, 2026 kwenye dimba la Corinthians.
MSHAMBULIAJI wa Brazil, Neymar Jr, alijikuta kwenye taharuki kubwa na kupandwa na hasira baada ya kufanyiwa mabadiliko ya lazima kufuatia kosa kubwa lililofanywa na mwamuzi wa akiba.
Tukio hilo lilitokea wakati Neymar akiiongoza Santos akiwa nahodha kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Brazil (Serie A) dhidi ya Coritiba, uliopigwa Mei 17, 2026 kwenye dimba la Corinthians.
Katika kipindi cha pili cha mchezo huo, Neymar (34) alipata jeraha kwenye misuli ya mguu wake wa kulia na kulazimika kupata huduma ya kwanza. Wakati huduma hiyo ikitolewa, kocha wa Santos, Cuca, alikuwa anajiandaa kufanya mabadiliko ya wachezaji uwanjani.
Mzozo ulianza pale mwamuzi wa akiba alipoinua ubao wa kielektroniki unaoonesha namba za wachezaji wanaotoka. Badala ya namba iliyokusudiwa, ubao huo ulionyesha namba 10 ya Neymar kwa rangi nyekundu, ikimaanisha yeye ndiye anayetakiwa kutoka.
Uamuzi huo ulimfanya nyota huyo wa zamani wa Barcelona na Paris Saint-Germain kulipuka kwa hasira. Viongozi wa Santos nao walivamia benchi la ufundi na kuanza kuzozana vikali na waamuzi.
Katika hali ya kuonyesha kukasirishwa, Neymar alinyofoa karatasi maalum ya mabadiliko kutoka kwa viongozi wake na kuionyesha mbele ya kamera. Karatasi hiyo ilionyesha wazi kuwa mchezaji aliyepaswa kutoka alikuwa ni namba 31, Gonzalo Escobar, na sio yeye.
Pamoja na ushahidi huo na malalamiko makubwa ya Santos, waamuzi waligoma kubadili msimamo wao. Neymar alilazimika kutoka huku nafasi yake ikichukuliwa na Robinho Jr.
Baada ya vurugu hizo, mambo yalizidi kuwa mabaya kwa miamba hiyo ya Brazil. Santos ilipokea kichapo kizito cha mabao 3-0 kutoka kwa Coritiba, huku Breno Lopes akifunga mabao mawili na Josue akipachika bao la tatu kwa mkwaju wa penalti. Santos pia walimpoteza mchezaji wao Alvaro Barreal aliyetolewa kwa kadi nyekundu.
Kufuatia matokeo hayo na uamuzi mbovu wa waamuzi, mashabiki wa Santos walipandwa na hasira kali baada ya kipyenga cha mwisho. Hali ilikuwa ya hatari kiasi kwamba waamuzi walilazimika kusindikizwa na jeshi la polisi kuondoka uwanjani, huku shabiki mmoja mwenye hasira akimrushia mwamuzi chakula aina ya 'hamburger'.
Tukio hili linakuja wakati Neymar akipambana kurudi kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Brazil kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia ya mwaka 2026. Nyota huyo hajaitwa kwenye kikosi cha Selecao tangu mwaka 2023 kutokana na kupata majeraha mfululizo.
Kocha mkuu wa Brazil, Carlo Ancelotti, anatarajiwa kutangaza kikosi chake rasmi leo Jumatatu. Licha ya matukio haya, Ancelotti hajawahi kufunga milango na ameweka wazi kuwa kuna uwezekano wa mshambuliaji huyo.