Waamuzi EPL wakiri kosa la VAR bao la Haaland
Muktasari:
- Tukio hilo lilitokea katika dakika ya 60, wakati Haaland alipofunga bao lililoipa Man City uongozi.
Mamlaka ya Waamuzi wa Ligi Kuu England, Pro Ref, imekiri kuwa kulikuwa na kosa katika namna VAR ilivyotafsiri bao la mshambuliaji Erling Haaland, lililoipa Manchester City ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Manchester United, katika mchezo wa uliochezwa jana Jumapili kwenye Uwanja wa Old Trafford.
Tukio hilo lilitokea katika dakika ya 60, wakati Haaland alipofunga bao lililoipa Man City uongozi.
Mwamuzi msaidizi awali aliamua kuwa mshambuliaji huyo alikuwa ameotea, lakini baada ya VAR kufanya ukaguzi, uamuzi huo ukabadilishwa na bao kukubaliwa.
Ingawa Haaland mwenyewe hakuwa katika nafasi ya kuotea kutokana na nafasi ya beki wa United, Patrick Dorgu, utata mkubwa uliibuka kutokana na nafasi ya kiungo wa City, Enzo Fernández.
Fernández alikuwa katika nafasi ya kuotea wakati mpira ukielekea eneo hilo na alijaribu kuufikia, ingawa hakugusa mpira.
Kwa mujibu wa Pro Ref, suala la kama Fernández aliathiri mchezo lilipaswa kuchunguzwa zaidi.
Mamlaka hiyo imekiri kuwa, VAR ilipaswa kumshauri mwamuzi Michael Oliver, kwenda kwenye kifaa chakuonyesha picha za matukio, ili kujionea mwenyewe tukio hilo kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.
Kukiri huko kumetoa nguvu zaidi kwa malalamiko ya Manchester United, ambao waliona kuwa bao hilo halikupaswa kuhesabiwa.
Kocha wa Man United, Michael Carrick, alikuwa miongoni mwa waliokosoa uamuzi huo baada ya mchezo, huku mjadala kuhusu tafsiri ya sheria ya kuotea ukiendelea.
Utata huo unakuja baada ya Man City kucheza sehemu kubwa ya mchezo ikiwa na wachezaji 10, kufuatia kadi nyekundu aliyoonyeshwa Phil Foden dakika ya 23.
Pamoja na kuwa na faida ya mchezaji mmoja, Man United ilishindwa kutumia nafasi hiyo na hatimaye Haaland akaamua mchezo kwa bao lake.
Licha ya Pro Ref kukiri kosa la VAR, matokeo ya mchezo hayajabadilishwa.
Manchester City imeendelea kushikilia ushindi wake wa bao 1-0, huku Haaland akiendelea kuonyesha ubora wake katika Manchester Dabi na kuongeza rekodi yake ya mabao dhidi ya wapinzani hao wa jiji.
Tukio hilo limeibua tena mjadala mpana kuhusu matumizi ya VAR England, hasa katika matukio ambayo mchezaji aliye katika nafasi ya kuotea hagusi mpira lakini anaweza kuwa ameathiri hatua ya mchezo.
Kwa sasa Man United imepata majibu kwamba kulikuwa na dosari katika mchakato wa uamuzi, lakini pointi tatu zimeendelea kubaki kwa Manchester City.