Real Madrid yawaza kumuuza Vinicius JR
Muktasari:
- Vinicius, mwenye umri wa miaka 25, amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake wa sasa, huku mazungumzo ya kuongeza mkataba yakionekana kukwama.
MADRID, HISPANIA: HATMA ya mshambuliaji wa Brazil, Vinicius Jr, ndani ya Real Madrid imeanza kutia shaka baada ya taarifa kueleza kuwa mabingwa hao wa Hispania wanafikiria kumuuza nyota huyo kutokana na kuchelewa kufikiwa kwa makubaliano ya kuongeza mkataba.
Vinicius, mwenye umri wa miaka 25, amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake wa sasa, huku mazungumzo ya kuongeza mkataba yakionekana kukwama.
Kwa mujibu wa mchambuzi wa Radio Marca, Ramon Alvarez, viongozi wa Real Madrid wameanza kuona uwezekano wa kufanya uamuzi mkubwa wa kumuuza nyota huyo iwapo hautapatikana mwafaka wa haraka.
Inaelezwa kuwa Vinicius anataka mkataba mpya utakaomfanya kuwa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi ndani ya Real Madrid, jambo ambalo linaweza kuleta changamoto kutokana na uwepo wa mastaa wengine akiwemo Kylian Mbappe.
Tayari vigogo wa Ligi Kuu England, pamoja na Paris Saint-Germain, Bayern Munich, na klabu kadhaa kutoka Saudi Arabia, wanaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya Vinicius wakisubiri fursa ya kumsajili.
Wakati huohuo, macho mengi pia yataelekezwa kwenye uhusiano kati ya Vinicius na kocha mpya Jose Mourinho, kufuatia mvutano uliowahi kutokea kati yao baada ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Benfica bado wengine wanaamini kuwa kila kitu kinaweza kuwa sawa baadaye.
Licha ya Mourinho kusisitiza kuwa anamkubali Vinicius kama mchezaji wa kiwango cha dunia, kauli zake za awali kuhusu namna nyota huyo alivyosherehekea bao na sakata la ubaguzi wa rangi ziliibua mjadala mkubwa.
Sasa Real Madrid inakabiliwa na uamuzi mgumu wa kuamua kama itaafiki matakwa ya Vinicius au itafungua mlango wa mmoja wa wachezaji wake muhimu kuondoka Santiago Bernabeu.
Vini ambaye timu yake ya Brazil imeshaondolewa kwenye Kombe la Dunia amekuwa mmoja kati ya mihimili imara kwenye kikosi cha Madrid akiwa ametumika kwenye michezo 450 na kufunga mabao 146 katika misimu minane aliyohudumu kwenye timu hiyo kubwa duniani.