Uganda yaanza na kipigo Kombe la Dunia
Muktasari:
- Korea Kusini ilitumia vizuri nafasi zake na kupata bao la mapema dakika ya nane kupitia Kim Ji-ho, kabla ya kuongezea bao la pili dakika ya 50 kufuatia kujifunga kwa beki wa Uganda, Mujad Mbalire. Kim Ji-woo aliyeingia akitokea benchi alihitimisha ushindi huo kwa bao la tatu dakika ya 84, akiipa Korea ushindi wa kujiamini katika mchezo wake wa ufunguzi
TIMU ya Taifa ya Uganda U-17, imeanza kampeni za Kombe la Dunia linaloendelea Qatar kwa kupokea kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Korea Kusini katika mechi ya kwanza ya kundi B iliyopigwa Uwanja wa Aspire Zone.
Korea Kusini ilitumia vizuri nafasi zake na kupata bao la mapema dakika ya nane kupitia Kim Ji-ho, kabla ya kuongezea bao la pili dakika ya 50 kufuatia kujifunga kwa beki wa Uganda, Mujad Mbalire. Kim Ji-woo aliyeingia akitokea benchi alihitimisha ushindi huo kwa bao la tatu dakika ya 84, akiipa Korea ushindi wa kujiamini katika mchezo wake wa ufunguzi.
Mchezo huo una uzito mkubwa kwa Uganda kwa sababu ni ushiriki wake wa pili mfululizo katika mashindano hayo. Ilianza safari yake mwaka 2025 nchini Qatar, ambako ilifika hatua ya 16 bora kabla ya kuondolewa. Hivyo, tofauti na Korea Kusini, ambayo ina historia ya ushiriki mara nane kabla ya mwaka huu, Uganda bado inajenga uzoefu wake kwenye jukwaa hilo.
Kipigo hicho kinaifanya Uganda kuwa na kazi kubwa katika mechi mbili zilizobaki za kundi hilo, hasa ikizingatiwa kuwa matarajio yake ni kurudia au kuvuka mafanikio ya mwaka jana.
Korea Kusini, kwa upande mwingine, imeendelea kuonyesha kuwa ni timu yenye uzoefu mkubwa katika mashindano hayo. Kabla ya mashindano ya mwaka huu, ilikuwa imeshiriki mara nane na mafanikio yake makubwa yalikuwa kufika robo fainali mara tatu, mwaka 1987, 2009 na 2019.
Rekodi hiyo inaonyesha kuwa ushindi dhidi ya Uganda ni muendelezo tu wa kile ilichowahi kufanya nyuma.
Uganda sasa italazimika kujipanga upya kabla ya mchezo wake unaofuata dhidi ya Ecuador utakaopigwa Novemba 22, huku ikihitaji matokeo mazuri ili kuendelea kuwa na nafasi ya kusonga mbele.
Kwa upande wa Korea Kusini, ushindi huo ni mwanzo mzuri wa safari yake ya kutafuta nafasi ya kufanya vizuri zaidi ya ilivyofanya mwaka jana, ilipofika hatua ya 32 bora kabla ya kuondolewa.
MATOKEO MENGINE
FT: New Caledonia 0-1 Equador
FT: Ufaransa 3-1 Haiti